Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia sisi sote fursa ya kuwa hapa leo na kufanya Shughuli za Bunge. Kipekee kabisa ninapenda nimpongeze Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Makamu wa Rais Dkt. Emmanuel John Nchimbi kwa ushindi mkubwa walioupata katika uchaguzi uliopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kipekee kabisa ninawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushinda kwa kishindo Uchaguzi Mkuu uliopita na leo hii kuwa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwanza kwa kutoa pole nyingi kwa wananchi wa Jimbo la Morogoro Kusini. Kwa sasa tumepata baraka ya mvua mfululizo kwa wiki tatu. Mvua hii sasa imesababisha mafuriko makubwa kiasi ambacho mawasiliano yamekuwa magumu kwa wananchi wa Jimbo la Morogoro Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni katika kipindi hiki takwimu za vifo vya mama na mtoto inakuwa inaongezeka kwa kiasi kikubwa jimboni kwetu kwa sababu mawasiliano kutoka kwenye makazi ya watu kwenda kwenye zahanati yanakuwa magumu kwa sababu mito imejaa na hawawezi kuvuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni likizo maalumu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, watakuwa nyumbani kwa kipindi cha takribani miezi miwili kwa sababu pia ya kushindwa kuvuka kwenda kupata elimu. Kwa sababu hiyo pia takwimu za ufaulu katika Jimbo la Morogoro Kusini zinakuwa ziko chini sana. Moja ya sababu ni kwamba tuna mito mingi, lakini hatuna vivuko. Kwa hiyo, tunashindwa kupata huduma za afya na tunashindwa kupata elimu kwa sababu ya changamoto hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata huku katika maeneo ya bondeni, watu wengi wanaliwa na mamba, kwa sababu hata wanapojaribu kuvuka kwenda kutafuta mahitaji, wanakutana na changamoto hiyo. Ninaiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa iliangalie jambo hili kwa namna ya kipekee kabisa na hasa kutuangalia katika vivuko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa nilete agizo aliloniagiza Mheshimiwa Waziri Mkuu tulipokutana katika Bwawa la Kidunda pale, wakati wanafanya malipo ya wananchi wa Kijiji cha Bwira Chini, pamoja na Kiburumo, ili wahame kupisha ujenzi wa Bwawa la Kidunda, waliwahamisha na kuwapeleka eneo linaoitwa Mji Mpya na kuvifuta vijiji vile. Tangu wawe hapo hawana huduma yoyote ya msingi ya Serikali za Mitaa, Serikali za Vijiji hazipo. Kwa hiyo, tulipeleka ombi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu ya kwamba, tunaomba Kijiji cha Bwira Chini na Kijiji cha Kiburumo virejeshwe katika mji mpya kwa majina yaleyale, pamoja na vitongoji vilevile, ili waweze sasa kupata huduma na Serikali pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliniambia nililete Bungeni na nilieleze hapa na leo nimelileta na ninalieleza, nikiomba Ofisi Waziri Mkuu ilichukuwe liende likalifanyiwe kazi. Pia kama haitoshi, vijiji hivi ambavyo viko katika Kata ya Selembala kuna vijiji vingine vitatu, ambavyo ni Bwila Juu, Kiganila na Magogoni; hivyo navyo sasa vinamezwa na mafuriko na mmomonyoko wa Mto Ruvu, wanaomba kwa sababu, wanapakana na Hifadhi ya Mkulazi, basi Serikali ione namna inavyoweza kuwahamisha katika sehemu ya hifadhi, ili kuepukana na adha hiyo. Kwa taarifa nilizonazo watu wawili wameliwa na mamba wiki moja nyuma kutokana na hali hii ya mafuriko na maji kuingia huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia Ofisi ya Waziri Mkuu, naipongeza Serikali, inafanya kazi kubwa sana, lakini pia, sisi sote humu ni mashahidi kwa sababu, kila aliyesimama ametambua juhudi kubwa anayofanya Mheshimiwa Rais katika kutuletea maendeleo, lakini sisi tunamsahau Mheshimiwa Rais. Mimi ni Mbunge ambaye miongoni mwa wananchi ninaowawakilisha katika Bunge lako Tukufu ni pamoja na Dkt. Samia Suluhu Hassan. Yeye ni mkulima katika Jimbo la Morogoro Kusini, analima katika Kata ya Mvuha, lakini yeye na wananchi wenzake katika kata ile hawana maji, pamoja na sifa kubwa ya pesa nyingi anazopeleka katika Wizara ya Maji, lakini hana maji katika Kata ya Mvuha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nafikiri alipokea taarifa ya ku-erect minara zaidi ya 750 ya mawasiliano, lakini akiwa katika shamba lake pale Kijijini Msonge, huwezi kumpata kwa simu, hana mawasiliano ya simu. Kwa hiyo, ninaiomba Wizara sasa ika-elect mnara kule, kama kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazozifanya katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anapotoka Dar es Salaam kwenda shambani kwake, kutoka kwenye Kata ya Tununguo, ni kilometa tano, ili afike Kijiji cha Msonge, lakini haiwezekani kwa sababu, eneo hilo halijaunganishwa kwa daraja. Inambidi Mheshimiwa Rais asafiri kilometa 60 zaidi, ili kuweza kufika sehemu ambayo ndiyo anafanya shughuli zake za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba basi, wale wenye dhamana ya ujenzi wa madaraja na barabara wawafikirie wananchi wa Kijiji cha Msonge, lakini zaidi wamsaidie pia, Mheshimiwa Rais. Anakwenda kustaafu, muda mwingi atakuwa yuko shamba, basi awe na usafiri mwepesi na wa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine...
MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umemalizika.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)