MHE. KELLEN R. RWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Je, ni lini Serikali imejipanga kukamilisha hayo malipo ya awali (advance payment) ili ujenzi uanze kufanyika kwa speed, kwa sababu wananchi wa Mlimba wamesubiri sana kwa muda mrefu?
Je, ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri atapanga muda ili tuambatane kwa pamoja ili kujionea mwenyewe mazingira na hali halisi ilivyo ya barabara za Jimbo la Mlimba zilivyo? Mvua zinanyesha kwa wingi, barabara zina makorongo, hazipitiki na wananchi wanapata taabu sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeshapata mkandarasi, tunajua athari ya kutokumlipa malipo ya awali. Malipo ya awali yanaandaliwa ili aweze kuanza kazi ya ujenzi kwa kipande hicho cha kilometa 37.5. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba mkandarasi ameshapatikana na atalipwa malipo ya awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutembelea hiyo barabara, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, niko tayari. Ninakuhakikishia nimeshaitembea hiyo barabara mara mbili, kuanzia Ifakara – Mbingu – Mlimba – Kibena Junction. Kwa hiyo, ninaifahamu, ni barabara muhimu ambayo inaunganisha Njombe na Morogoro. Kwa hiyo, niko tayari, ahsante. (Makofi)