Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. KELLEN R. RWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha hapa siku ya leo na kunisimamisha hapa mbele yenu ili niweze kuchangia kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ni kwa mara yangu ya kwanza ninasimama kwenye Bunge hili Tukufu ili niweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninachukua nafasi hii kuishukuru Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wetu kwa kuweza kunichagua na kuniamini ili niweze kugombea Ubunge kwenye Jimbo la Mlimba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kuwashukuru Wananchi wa Jimbo la Mlimba kipekee kwa kumchagua Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kura nyingi sana za kishindo wakati wa uchaguzi ule ili awe Rais wetu. Pia, ninawashukuru wananchi kwa kunichagua mimi kuwa Mbunge wao wa Jimbo la Mlimba. Ninawaahidi kwamba sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa. Pia, ninampongeza kwa ziara ambazo anazifanya, ni ziara za tija, ziara zenye kuonesha vitendo. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri Mkuu anaenda site, anatufundisha hata sisi tuweze kwenda site na kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua pale tunapoweza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpongeza sana, sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu, kwa juhudi kubwa anazozifanya kutuletea maendeleo kwenye nchi yetu hususan kwenye Jimbo langu la Mlimba. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuletea bima ya afya zaidi ya watu 2,800 wameshapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru pia tumeletewa ajira 158 ambazo ni ajira kwenye section ya elimu na afya, kwa hilo tunashukuru. Mikopo ya 10%, Jimbo la Mlimba tumepata zaidi ya shilingi bilioni moja kwa 10%. Hizo zimeenda kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kutokana na pesa hiyo ambayo wamepokea, ajira zaidi ya 10,000 zimepatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo, Mlimba tuna changamoto, changamoto yetu ni barabara, barabara, barabara. Kama vile ambavyo wenzangu wameshasema, hili ni janga la kitaifa lakini nikiongelea Jimbo la Mlimba, barabara hii ni kipaumbele katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Barabara ya kutoka Ifakara – Mlimba – Njombe ni muhimu kwa sababu inaunganisha mikoa miwili ambayo ni Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Njombe. Kwa hiyo, imebeba uchumi wa mikoa hii miwili na ndiyo inayotumika kusafirisha mazao yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua, wananchi wa Mlimba na wananchi wa Njombe uchumi wao unategemea ukulima, tunalima mchele ambao ndiyo mpunga. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali iiangalie barabara hii kwa umuhimu wake ili iweze kujengwa kwa haraka zaidi kutokana na umuhimu wa barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea sasa hivi barabara imepata mkandarasi, mkandarasi yuko site lakini anadai advance payment. Ninaiomba Serikali impatie advance payment ambayo imebaki, imempatia kidogo partial payment. Kwa hiyo, tunaomba aweze kupata full payment ile ya advance payment aweze kuanza kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa barabara za TARURA, ninapenda kuishauri Serikali iongeze pesa kwenye bajeti ya TARURA ili kuhakikisha barabara za vijijini nazo zinapitika kwa wakati wote. Pia, halmashauri niwashauri TARURA wapate pesa za dharura ili barabara hizi zilizoathiriwa na mvua hizi zinazoendelea kunyesha ziweze kutengenezwa angalau pia ziweze kupitika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kwenye Jimbo langu la Mlimba, Barabara ya Mpanga – Kikowe – Ngalimila ambayo inaunganisha Wilaya ya Mlimba na Wilaya ya Malinyi, haipitiki. Barabara ya Namwawala – Mofu haipitiki. Barabara ya Kamwene – Matema – Uchindile haipitiki. Barabara ni nyingi jamani ninazosema. Barabara ya Mlimba – Mwembeni – Msolwa pia haipitiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hapo madaraja pia yamekatika. Daraja la Chiwachiwa, Daraja la Mfuji, Daraja la Mto Londo, yote yamekatika na hayapitiki. Kwa hiyo, ninaomba Serikali yetu Tukufu iziangalie hizi barabara kwa jicho la ziada ili ziweze kutengenezwa na wananchi wetu waweze kuendelea na mawasiliano na kazi zao za kuinua uchumi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa afya, tunashukuru sana Serikali yetu Tukufu ilitujengea hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba. Hospitali inafanya kazi, lakini ina changamoto. Changamoto yetu katika upande huu wa hospitali yetu ni ukosefu wa watumishi wa maabara, ukosefu wa wataalam wa mionzi na ukosefu wa jengo la emergency. Pia, tuna ukosefu wa jengo la theatre na jengo la mama ngojea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali yetu Tukufu ituletee watumishi hawa na pia itujengee haya majengo ili wananchi waendelee kupata huduma na wapate huduma kwa karibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, ninashukuru kwa nafasi hii na ninaunga mkono hoja. (Makofi)