MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jimbo la Malinyi lina Miradi ya Maji katika Kijiji cha Misegese – Ihowanja na Mtimbira na miradi hii imekaa muda mrefu zaidi ya miaka mitatu sasa bila kukamilika. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha ili kukamilisha miradi hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Malinyi, ni Mbunge mahiri, na pia ni Mjumbe katika Kamati yetu ya Maji na Mazingira, tunaendelea kutambua mchango wake mkubwa sana katika kuishauri Serikali na kuisimamia. Katika kuwatetea wananchi wake, sisi tutaendelea kumpa ushirikiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo madai ya wakandarasi ndani ya Jimbo lake, na tayari yameshaletwa na yameshafika kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu, wanayafanyia kazi. Tunaamini kabisa kwamba ndani ya kipindi cha miezi miwili mitatu hii, tutapeleka fedha ili wakandarasi hawa walipwe ili miradi hii ambayo imekaa kwa muda mrefu iweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali, siyo hiyo miradi pekee, miradi yote inayoendelea kutekelezwa nchini tunayo maelekezo mahsusi ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba tunakamilisha kwanza hii miradi ambayo imeishaanza badala ya kuanza miradi mipya ili kuhakikisha kwamba tunaanza kupata matokeo kabla ya kuanzisha miradi mingine mipya. Ninakushukuru sana.