Answers to Primary Questions by Hon. Denis Lazaro Londo (3 total)
MHE. JOHN J. NCHIMBI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha kukoboa Kahawa Nyasa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, ninaomba nijibu swali namba 79 la Mheshimiwa John John Nchimbi, Mbunge wa Nyasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Nyasa inazalisha kahawa aina ya Arabica kwa wastani wa tani 2193 kwa mwaka. Kutokana na uzalishaji huu, Mheshimiwa Rais aliona umuhimu wa kuwa na kiwanda katika eneo hili. Hivyo, Serikali kupitia Halmashauri ya Nyasa imetenga eneo lililopo Kitongoji cha Ndanda, Kijiji cha Kingirikiti Kata ya Kingirikiti kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kukoboa kahawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili lina ukubwa wa hekta nne na lina miundombinu wezeshi kama vile barabara, maji na umeme. Aidha, eneo hili linamilikiwa na Serikali na lipo tayari kwa ajili ya uwekezaji kwa kujenga kiwanda cha kukoboa kahawa. Serikali inaendelea kuhamasisha wawekezaji kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kukoboa kahawa katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha kimkakati ndani ya Mji wa Tarime?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Viwanda na Biashara naomba nijibu swali namba 10 la Mheshimiwa Esther Matiko.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunafanya kazi, na tumeandaa mpango wa ujenzi wa Viwanda nchini katika kuongeza thamani ya bidhaa zetu ikiwemo Mji wa Tarime ambapo itazingatia uongezaji wa thamani katika mazao ya kilimo, mifugo na madini ambayo yanapatikana huko.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje katika ujenzi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vyenye mkakati kupitia Taasisi za TISEZA na SIDO. Wakati huo huo tunahamasisha balozi zetu, wadau mbalimbali na wananchi wote wa Tanzania kwa pamoja kutangaza rasilimali na vivutio ambavyo vipo katika Mji wa Tarime na Mkoa wa Mara kwa ujumla ili hamasa hiyo iende sambamba na kutoa vivutio vya kikodi na visivyo kikodi ambavyo vinaendelea kutolewa chini ya Taasisi ya TISEZA.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. DICKSON N. LUTEVELE aliuliza: -
Je, lini malipo ya waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Karatasi (SPM Mgololo) yatafanyika, ukizingatia kuwa ni ya muda mrefu sana?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara ninaomba nijibu swali namba 35 kutoka kwa Mheshimiwa Dickson Nathan Lutevele, Mbunge wa Mafinga Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Southern Paper Mills Ltd. (SPM) ilibinafsishwa mwezi Februari, 2004 kwa mwekezaji aitwae RAI Group kutoka Kenya. Baada ya ubinafsishwaji, wafanyakazi wapatao 760 wa kiwanda hicho walifungua Shauri Na.162/2017 la madai katika Mahakama Kuu Tanzania Divisheni ya Kazi dhidi ya Serikali wakidai mafao ya utumishi wao kabla ya kubinafsisha kiwanda hicho. Suala hili la madai ya wafanyakazi hawa bado lipo ngazi ya Mahakama.