Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Esther Nicholas Matiko (7 total)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Tarime ni miongoni mwa maeneo ambayo yanapata mvua ya mara kwa mara, na hivyo kusababisha barabara kuharibika na kuathiri shughuli za maendeleo na uchumi za Mji wa Tarime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kujua, nini mkakati wa Serikali wa kulingana na mazingira ya Halmashauri ya Mji wa Tarime ya mvua ya mara kwa mara, kujenga barabara ambazo zitastahamili hali ya hewa ya Mji wa Tarime ili wananchi wa pale waweze kupita muda wote kwenye barabara zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya Barabara za Tarime ni kama ilivyo hali ya Barabara za Mji wa Morogoro. Mpango ambao tumeuweka kwenye Mkoa wa Morogoro, vivyo hivyo tutau-extend kwenda Tarime. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, Barabara ambayo inaanzia keep left inakwenda mpaka Mogabiri yenye kipande cha takriban kilometa 9.3 iliyopo Tarime Mjini imeharibika sana kiasi cha kupelekea ajali mbaya sana na wakati mwingine vifo. Hata hivyo, kwa sababu tayari mkandarasi yupo na yupo tayari kuanza kazi anasubiri tu malipo ya awali, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kupeleka fedha hizi ambazo ni takriban shilingi bilioni 7.9 ili barabara hii iweze kutengenezwa na kuunganishwa na ile barabara inayoenda mpaka Nyamwaga ambayo tayari imeshakamilika? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninaomba nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kwamba kipande hicho ni kweli kimeharibika, kilikuwa na lami, lakini barabara ilitangazwa yote. Ilibidi tuanze mbele ili baadaye tuweze kufumua kipande hiki ambacho amekiongelea Mheshimiwa Mbunge. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunajua kwamba hatuwezi tukatoka na barabara ya vumbi kutoka Tarime halafu tukaenda kuipata lami mbele. Kwa hiyo, nimhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tunaandaa malipo ili mkandarasi aweze kulipwa na kuanza kuikarabati, ambayo ni sawa na kuijenga upya hiyo barabara ambayo ina zaidi ya kilometa tisa. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Tarime una Miradi mitatu ya TACTIC, ambayo ni Stendi ya Kimange, barabara za lami ikiwepo Barabara kutoka Lebu – Kebaga mpaka Biyambu, ambayo ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa Tarime pamoja na Mradi wa Dampo. Ninataka kujua ni lini sasa miradi hii itaanza na kukamilika kwa manufaa mapana ya wananchi wa Tarime Mji? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Tarime ni miongoni mwa miji inayokua kwa haraka. Nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyoupambania huu Mji wa Tarime; tupo katika mpango wetu wa kutekeleza huu Mradi wa TACTIC Awamu ya Tatu na ngazi ya usanifu wa dhana, pamoja na usanifu wa awali tuko mwishoni kuukamilisha. Tutakwenda kutangaza zabuni, kuanza ujenzi mara moja. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ambao unakaribia kukamilika mwaka huu Septemba kuna wananchi ambao walipisha huo mradi. Sasa ningetaka kujua hawa wananchi waliopisha mradi huu mkubwa ni lini wanaenda kulipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana na ninamshukuru sana Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge kwa kuendelea kuwapigania. Kwanza kuhitaji wa wananchi wapate huduma ya majisafi na salama, lakini pia wale ambao wanapisha mradi wahakikishiwe kwamba wanapewa haki yao ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali, kabla hatujalipa tunafanya tathmini na kujiridhisha wanastahili kulipwa kiasi gani? Yupi anayestahili kulipwa, na yupi ambaye hastahili kulipwa? Baada ya kujiridhisha, Serikali inakwenda kufanya malipo kulingana na haki ya kila mwananchi ambaye atakuwa sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza miradi ya maji.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, kufuatia majibu ya Serikali, kwanza kabisa ningependa kusema wazi wawekezaji wengi hasa wale wakubwa wanapenda kuwekeza Mkoa wa Pwani, labda kwa sababu kupo karibu na Dar es Salaam. Huku pembezoni na kama ilivyo Mji wa Tarime, siyo rahisi sana kuweza kuvutia wawekezaji wakubwa kuja kuwekeza.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru Serikali imekiri kwamba kwa jiografia ya Mji wa Tarime, tuna upatikanaji mkubwa wa malighafi za kilimo, mifugo pamoja na madini. Pia, Mji wetu wa Tarime uko mpakani, na hivyo kuifanya Tarime Mji kuwa kituo kizuri tu cha kiwanda cha kuzalisha thamani.

Mheshimiwa Spika, sasa ningependa kujua kwa kuwa hasa bidhaa za ujenzi ni ghali sana kwa kule kwetu Mkoa wa Mara, na asilimia kubwa inatoa Kenya, Serikali haioni kwamba ni wakati mwafaka kuhakikisha kwamba inavutia wawekezaji wakubwa wa vifaa vya ujenzi kama uzalishaji wa mabati, nondo, vifaa vya maji ili waje kuwekeza kule ili kupunguza watu kwenda Kenya au kupata bidhaa Tanzania kwa gharama kubwa zaidi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa malighafi za kilimo zinapatikana, na pia tungependa kupata mwekezaji mkubwa ambaye anaweza kuchakata na kuwa na Kiwanda cha Biskuti kwa sababu tuna viazi vingi sana vinasafirishwa kuja huko mikoani au crips ambazo zinatokana na ndizi. Serikali haioni pia kuna haja sasa ya kumleta mwekezaji huyu mkubwa kuacha wale wadogo ambao umeeleza kwenye jibu lako la msingi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, kwanza nikiri maelezo ya Mheshimiwa Mbunge. Tarime ni Wilaya ya kimkakati na hasa tunapozungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki iko mpakani na iko kimkakati, na ndio maana mkakati ambao tunao sasa hivi ni kuimarisha biashara katika mtengamano huu wa Jumuiya ya Afrika Mashiriki na kutumia Tarime na mikoa ya mipakani kama maeneo ya kimkakati wa Tanzania ku-access masoko katika Jumuiya hiyo.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana Serikali inatoa rai kwamba tunatangaza vivutio ambavyo ni vya kikodi na visivyo vya kikodi hususan kwenye miradi ya kimkakati ambayo inaweza kuwekezwa katika maeneo maalum ya kiuchumi na hii ikiwemo misamaha na nafuu ya kikodi ili kuhamasisha wawekezaji kwenda nje ya maeneo ambayo tumeyazoea hasa katika mikoa ya Pwani ili ku-access soko kubwa zaidi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Tarime ambalo ni eneo la kimkakati ku-access masoko hayo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kuhusiana na suala la kutafuta wawekezaji wakubwa. Kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Dira ya 2020-2050, lengo letu ni kuongeza thamani ya mazao, thamani ya madini yetu ambayo tunazalisha nchini, viwanda vya kimkakati ambavyo vinatoa ajira na kutuhakikishia pia uwepo wetu katika Jumuiya na ku-access masoko ya SADC pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Shule ya Amali ya Nyandoto iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime imeshakamilika miundombinu ya madarasa, ofisi, vyoo na nyumba ya Mwalimu, lakini shule hii ilijengwa nje ya mji, hivyo tunahitaji tupate fedha kwa ujenzi wa bweni na karakana, ili shule ianze. Sasa ni lini Serikali itapeleka fedha hizi kwa haraka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli kwamba, shule hii imejengwa awamu ya kwanza na tunafahamu kwamba katika mpango wa ujenzi wa shule zote 103 za amali mabweni, karakana na mitambo yote ya kihandisi ni sehemu ya ujenzi wa shule zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga awamu ya kwanza, zimeanza kutoa huduma kama shule za kutwa; awamu ya pili inakwenda kujenga mabweni, karakana pamoja na miundombinu yote ya uhandisi ili kuhakikisha shule hizo zinatoa huduma inayotakiwa. Kwa hiyo, tupo kwenye hatua za mwisho za kupata fedha kwa ajili ya kwenda kujenga miundombinu hiyo.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Wananchi wa Mji wa Tarime wana adha kubwa sana ya maji, na tegemeo lao kubwa; na wanaishukuru Serikali kwa Mradi mkubwa wa Maji Ziwa Victoria wa shilingi bilioni 134 lakini mradi huu ulianza mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu. So far wamepeleka shilingi bilioni 24 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kujua mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba hizi shilingi bilioni 110 zinaenda ili mradi huu ukamilike ndani ya muda na kuweza kupunguza adha ya maji kwenye Mji wa Tarime? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kabisa kwamba Mheshimiwa Esther Matiko ameendelea kupigania sana wananchi wake wa Tarime Mjini, na pia ameendelea kuhakikisha kwamba mradi huu anausukuma ili uweze kupata fedha na uweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba mradi huu unaenda kuwa mwarobaini, lakini mkakati wa Serikali sasa wa namna gani mradi huu unaenda kukamilika, ni kupunguza utitiri wa kutangaza miradi mingi wakati tuna miradi ambayo bado haijakamilika na haijaanza kutoa matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa tunaenda kuhakikisha kwamba badala ya kutangaza miradi mingi na kuzigawanya fedha ambazo zingeenda kukamilisha miradi kama hii, sasa tunaenda kuweka hitimisho katika utaratibu wa namna hiyo, na mkakati wetu ni kumaliza miradi viporo. Tukishamaliza baadaye tutaendelea na miradi mingine ambayo tutaweza kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, mradi huu ni kipaumbele kwa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na tuna uhakika mradi huu utakamilika na wewe mwaka 2030 utarudi, ahsante sana.