MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha kimkakati ndani ya Mji wa Tarime?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Viwanda na Biashara naomba nijibu swali namba 10 la Mheshimiwa Esther Matiko.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunafanya kazi, na tumeandaa mpango wa ujenzi wa Viwanda nchini katika kuongeza thamani ya bidhaa zetu ikiwemo Mji wa Tarime ambapo itazingatia uongezaji wa thamani katika mazao ya kilimo, mifugo na madini ambayo yanapatikana huko.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje katika ujenzi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vyenye mkakati kupitia Taasisi za TISEZA na SIDO. Wakati huo huo tunahamasisha balozi zetu, wadau mbalimbali na wananchi wote wa Tanzania kwa pamoja kutangaza rasilimali na vivutio ambavyo vipo katika Mji wa Tarime na Mkoa wa Mara kwa ujumla ili hamasa hiyo iende sambamba na kutoa vivutio vya kikodi na visivyo kikodi ambavyo vinaendelea kutolewa chini ya Taasisi ya TISEZA.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.