Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Moshi Selemani Kakoso (4 total)

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Karema, Kituo cha Afya cha Kasekese na Kituo cha Afya cha Mwese kuna tatizo kubwa la ukosefu wa Jengo la Mama na Mtoto, Maabara na nyumba za watumishi. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha,ili iweze kukamilisha hivyo vituo vya afya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali kwamba, zaidi ya vituo 532 vimeishatengewa bajeti ya shilingi bilioni 102.08. Kwa hiyo, pamoja na vituo ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameviainisha vimo katika ukarabati huu mkubwa na kuweza kujenga majengo mengine ambayo yanahitaji, kama maabara, ili kuendelea kupata huduma kwa wananchi wetu.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mvua zilizonyesha zimeharibu barabara nyingi kwenye eneo la Wilaya ya Tanganyika, ikiwemo Barabara ya kutoka Kapanga – Bujombe – Kalia, je, ni lini Serikali itakwenda kufanya ukarabati kwa barabara nyingi zilizoharibika kwenye eneo la Wilaya ya Tanganyika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika jimbo la Tanganyika, kama ambavyo ipo katika majimbo takribani yote kote nchini, kumekuwa na uharibifu mkubwa wa barabara zetu za TARURA. Serikali imeshafanya tathmini ya mahitaji ya fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo linafanyika sasa, kwanza maeneo mengi bado mvua zinaendelea kunyesha kwa hivyo, siyo rahisi kufanya matengenezo ya uhakika katika kipindi hiki cha mvua. Tunasubiri kwanza hali ya hewa ikae vizuri, mvua zipungue, na baada ya hapo, taratibu za fedha zinaendelea kufanyika ili tuendelee kujenga barabara hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Kakoso kwamba suala hilo liko kwenye pipeline na tutakwenda kuhakikisha kwamba tunajenga barabara hizo.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa wilaya ambazo hazina kituo cha Polisi na halmashauri ya wilaya ilianzisha ujenzi, na mimi kama Mbunge, nimechangia kwenye hicho kituo; na Serikali iliahidi kutoa shilingi milioni 20, lakini mpaka sasa ni mwaka wa tatu. Ni lini Serikali itakamilisha Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Tanganyika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Selemani kwa swali lake la msingi na ninawapongeza sana kwa kuchangia fedha kwenye ujenzi wa vituo vya Polisi ambao ni uhitaji mkubwa kwa usalama wa raia na mali zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumpongeza Mheshimiwa Selemani, nimjibu tu kwamba vituo ambavyo havijamalizika nilitoa maelezo ya jumla hapa kwenye maboma 77 na nimeeleza kwamba tutaendelea kusaidia ili kukamilisha vituo hivyo kikiwemo kituo chake Mheshimiwa Selemani na tumhakikishie tu kwamba tutajitahidi mwaka wa fedha 2026/2027 tuweze kumsaidia na kukamilisha hiyo fedha ambayo tumeahidi kutoa ili tuweze kukamilisha kituo hicho. Ahsante sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Serikali iliahidi kuanza ujenzi wa kuleta maji kutoa Ziwa Tanganyika kuyaleta Mpanda Mjini. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi huo ili wananchi waweze kunufaika?

SPIKA: Mheshimiwa Waziri.

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kama sijamsikia vizuri kwenye hilo.

SPIKA: Unaweza ukarudia tena Mheshimiwa Kakoso swali lako?

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kuleta maji kutoka Ziwa Tanganyika kuyaleta Makao Makuu ya Mkoa wa Katavi Mpanda Mjini. Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, katika mpango mahususi wa ujenzi wa gridi ya Taifa ya maji, moja ya maziwa na vyanzo vya uhakika ni pamoja na Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa, pamoja na mito mingine mikubwa mikubwa kama Malagarasi, Momba, Pangani na mingineyo. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba maji tunayatumia kwa kuyapeleka katika makazi ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tayari imeshampata mtaalamu mshauri kwa ajili ya kuanza kufanya feasibility study ya kuyatumia maji ya kutoka Ziwa Tangayika ili yaende Kigoma, Mpanda, mpaka Rukwa. Lengo ni kuhakikisha kwamba wananchi wote wanaunganishwa na huduma ya maji yenye vyanzo vya uhakika, likiwemo Ziwa Tanganyika. Nakushukuru sana.