Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Edibily Kinyoma Kazala (2 total)

MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, bado nina swali moja la nyongeza la kuiomba Serikali kama Mheshimiwa Waziri yuko tayari tuambatane naye kuelekea jimboni akaone na kujidhirisha namna zoezi lilivyotekelezwa na kusaidia kutatua migogoro inayoambatana na kitalu hiki cha Makere Forest Reserve Uvinza Open Area.

Mheshimiwa Spika, kitalu ambacho kinasabaisha mgogoro wa wananchi; wananchi kufyekewa mazao, kupigwa na kuna mgogoro wa kimapato na halmashauri kwa mfano kwa DCC ripoti tuliopata wanapata kama 1,900,000 tu. Pia kuna mgogoro wa Kacheri na Luguvu Relini ambao nao wameambiwa kuhamishwa, kuna mgogoro wa wananchi wenyeji nao wamechukuliwa maeneo yao na wakati walikuwepo pale tangu miaka ya 70.

Mheshimiwa Spika, pia kuna mgogoro wa TFS na wananchi wa kimpaka, wananchi wamewekewa beacon mpaka katikati ya vijiji. Ninaomba ikiwezekana Mheshimiwa Waziri aambatane nami twende jimboni kupunguza changamoto zinazokabili jimbo langu. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi niko tayari hata tukimaliza Bunge twende kwa wananchi wetu kuweka tabasamu kuondoa migogoro ambayo inawakabili. (Makofi)
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kuna baadhi ya majibu hapo naona kama si sahihi ikiwemo shilingi milioni 166 ambazo ziligaiwa kwenye halmashauri kwenye huduma ya macho, DMO amekataa kwamba hizo fedha hazijawahi kufika. Pia hivyo visima sita vinavyotajwa hapo, kati ya hivyo visima sita vipo viwili tu na kimoja ndicho kinachofanya kazi vizuri, lakini pia baadhi ya hizo shilingi milioni nne zinazotajwa hapo nazo zinaonekana baadhi ya vijiji bado wanakiri kutokupokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji huyu…

MWENYEKITI: Maswali Mheshimiwa.

MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niulize; mwekezaji huyu amekuwa akiwa na changamoto nyingi kwa jimbo langu la Kasulu Vijijini ikiwemo kufyeka zaidi ya hekari 200, kuzuia wananchi kuvua kwenye Mto Malagarasi na kuzuia wananchi kuweka mizinga kwenye miti.

Je, Serikali haioni haja ya kuleta mwekezaji mwingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa mwekezaji amekuwa akigombana sana na wananchi wa Jimbo langu la Kasulu Vijijini; je, Serikali haioni kuwa ipo haja ya kukikata kipande kile ambacho kipo mwekezaji anapopakana na wananchi kimilikiwe na halmashauri ili iongezee mapato na kuepusha migogoro ya Serikali na wananchi?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Mbunge, ameomba kupelekewa mwekezaji mwingine kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la kitalu cha Makere Uvinza Open Area lipo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ambako Mheshimiwa Mbunge ni sehemu ya Baraza la Madiwani. Sisi kama Wizara tulipokea ombi kutoka kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kuhusu kutenga eneo hili kwa ajili ya eneo la uhifadhi na utalii. Hivyo, mamlaka haya yapo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu. Kama watakaa chini na wakaamua tena kama Baraza la Madiwani sisi kama Wizara ya Maliasili na Utalii hatuna kipingamizi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili la kumega eneo na kuwa sehemu ya halmashauri, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya swali lake la nyongeza la kwanza, eneo hili lipo chini ya miliki ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu na wao ndio waliotuomba sisi kama Wizara tuweze kutoa miongozo ya jinsi ya kuendesha eneo hili kwa ajili ya uhifadhi na utalii. Hivyo kwa kuwa eneo hili lipo chini ya miliki ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ninaomba nimshauri Mheshimiwa Mbunge arejee kwenye Baraza la Madiwani na waweze kuketi kuona jambo gani wanaweza kufanya kwa maslahi mapana ya halmashauri yake ya Kasulu. (Makofi)