Contributions by Hon. Edibily Kinyoma Kazala (3 total)
Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii uliyonipatia na mimi nichangie kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kasulu Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninaipongeza Serikali kwa kuja na mpango mahususi wa kiungwana kabisa kwa Watanzania wazalendo wa kimkakati wa kuhakikisha Taifa letu linatoka hatua moja kwenda hatua nyingine kwa kipindi cha miaka mitano. Ninaona hapa projection ya uchumi kwa maana ya economic growth kwa mwaka 2025 imekuwa kwa asilimia tano nukta sita, lakini pia tunatarajia mwaka huu inaweza ikaenda asilimia sita halafu mwakani ikaenda kama asilimia sita nukta nane au around hapo saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona malengo ya Wizara na malengo ya Mpango wetu ni kutengeneza uchumi imara, uchumi ambao utakuwa jumuishi, lakini pia wa kiushindani. Nianze na kwenye uchumi imara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uchumi imara, hapa lazima maana yake kama Taifa tuwe na base ya Kitaifa ambayo itasababisha uchumi wetu kuwa stable katika kipindi chetu cha miaka mitano au kipindi cha miaka 25 mpaka 2050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushauri wangu, kama Taifa ni kweli tunatamani mambo yote yaende vizuri, sekta zote ziende vizuri, lakini ningetamani kama Taifa tuwe na vipaumbele vichache ambavyo kama tutajikita na halafu tujivunie kupitia vipaumbele hivyo kama Taifa la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kilimo. Ninashauri kama Taifa, tujikite sana kwenye kilimo kwa sababu kina tija kubwa sana kwa wananchi wetu mmoja mmoja na kwa Taifa kwa ujumla. Kwenye andiko hili inaonyesha kilimo, ndio wanaochangia sehemu kubwa ya pato la Taifa, wastani wa 20% mpaka 24%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningeshauri kama Taifa tuwe na mikakati madhubuti ya kimakusudi ya kuhakikisha tunaki-boost kilimo ili angalau tusiwe na kilimo ambacho kinaweza kikayumba kutokana na msimu. Maana yake hapa nashauri tuongeze mikakati ya umwagiliaji, mikakati ya uvuvi, mikakati ya kutumia vyanzo vyetu vya maji tulivyonavyo kama Taifa kuhakikisha wananchi wetu tunawahakikishia kilimo muda wote na mazao muda wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye kilimo hapa labda nizungumze, kwa mfano, Jimbo langu la Kasulu Vijijini tuna maeneo mengi sana ambayo yanafaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambayo kama yakitumika vizuri kwa kweli wananchi wangu kwa kweli ni neema ya pekee na utakuwa umegusa maisha ya almost robo tatu ya wananchi wangu wa Jimbo la Kasulu Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa ushauri wangu kama Taifa tungewekeza msukumo mkubwa tuka-boost kilimo pengine kichangie hata 30% pengine mpaka 40% kwenye uchumi wetu au pato letu la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie upande wa masoko. Changamoto nyingine iliyopo kwenye kilimo, ni masoko. Kwenye mchango wangu uliopita kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Rais, nilishauri kwamba ikiwezekana tuitumie TEHAMA vizuri ili kutafuta masoko ya uhakika kwa wananchi wetu. Tuje na mifumo ambayo mwananchi wa vijijini, mwananchi wa mbali anaweza akaangalia Soko la Dar es Salaam linasemaje kuhusiana na mazao yake yaliyoko kijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishauri kwamba ikiwezekana tuwe na mfumo software au application ambayo mwananchi aki-click kama ni Mchele, kama ni Pamba na kadhalika, ataona soko linasemaje hapa Dodoma, Kilimanjaro, au Babati na maeneo mengine. Vilevile, anaweza kuona mpaka nchi jirani kunasema nini kuhusiana na zao hilo kuhusiana na suala la bei?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri kwamba uwepo pia mkakati wa kimakusudi wa kufungua maeneo ya vijijini, kwa maana ya barabara zipitike kwa kiwango cha changarawe, kwa kiwango cha lami. Nilikuwa ninaangalia kwenye ujenzi wa mtandao wa lami waliojenga kwa barabara zilizoko TANROADS ni kama kilometa 100 na kidogo tu ambapo ukiangalia pale kwa kweli inasikitisha kama tuna makusudi kweli ya kuhakikisha kwamba tunafikia malengo yetu kwa kipindi cha miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia kuhusiana na upotevu wa mapato. Kama Taifa, nimeona hapa wanasifiwa watu wa Local Government Authorities kwamba wamechagiza sana performance ya ukusanyaji wa mapato, lakini kinachoendelea kwenye Serikali zetu za Mitaa pamoja na performance inayoonyeshwa hapa kwamba wamefanya vizuri kwa kweli kinasikitisha sana. Kinachotokea kule moja, kuna wakati kule wanajitengea bajeti ndogo yaani wanafanya underestimation ya vyanzo vyao vya mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano; kuna mahali fulani nilienda wameandika watakusanya pale milioni 50, lakini ukiangalia kile chanzo cha mapato yako mapato ya waziwazi kabisa ambayo wanaweza kukusanya mpaka milioni 150. Kwa hiyo, baadaye wakiweka ile kadirio la chini la milioni 50 wakishafikia milioni arobaini na kidogo wanajipongeza kwamba wame-perform sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ninafanya Masters yangu nimefanya utafiti kwenye Local Government Authorities hasa kwenye ukusanyaji wa mapato. Kule mapato mengi yanapotea ukilinganisha na kile ambacho tunakusanya yaani pengine inaweza ikawa ni nusu kwa nusu, yaani kinachopotea na kile tunachopata kama Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri kwamba, kama Serikali tujikite kwenye matumizi ya TEHAMA ya kisasa. Kwanza nipongeze kwamba point of sales imekuwa ikifanya vizuri, lakini baadhi ya maeneo haifanyi vizuri hasa kwenye stendi zetu. Kwa mfano stendi zile za Magufuli na stendi zingine kuna maeneo ukienda pale getini hali ni mbaya, ukienda vyooni hali ni mbaya, mtu anaingia hakuna chochote kinachokusanywa pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilienda mbali nilijaribu kuuliza baadhi ya watu wanasema wanatumia loopholes iliyopo kwa sababu mtu anaingia au anaweza akapitisha gari getini ikiishapita gari au ikapita pikipiki hachani karatasi ile yaani ha-print kwa maana ile risiti ya point yaani point of sales kwa maana ya POS hampatii risiti ili mradi tu amepita kama ni chooni ameenda amerudi, kwa hiyo, unakuta tunapoteza mapato mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niishauri Serikali tuangalie namna ya kuziba mianya hasa kwa yale mapato tutakayokusanya kama Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishauri kuhusiana na uchumi wa ushindani. Tunavyoangalia uchumi wa ushindani lazima tujipime na wenzetu. Sasa kwa Afrika Mashariki inaonekana uchumi kwa mwaka jana 2026 ulikuwa wastani wa 5.3, lakini uchumi wetu umekua kwa asilimia 5.6. Hapo hapo kuna mataifa mengine kama Rwanda yako saba lakini pia Uganda na yenyewe iko sita na kwa mujibu wa IMF inasema kwamba wakianza uzalishaji tu wa mafuta kama Uganda uchumi wao utakua mpaka kwa 10%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishauri hapa kama Taifa tuwe na mkakati wa kimakusudi tusijikute tunaburuza mkia kwa miaka mitano mingine inayokuja ukilinganisha pengine kwa Afrika Mashariki. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa muda.
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ili nichangie hotuba ya Mheshimiwa Rais. Awali ya yote ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa fursa hii ya uhai. Pia, kipekee ninamshukuru Mheshimiwa Rais kama Mwenyekiti wangu wa Chama Cha Mapinduzi Taifa kwa kuniteua ili niingie kwenye kinyang’anyiro cha Ubunge na hatimaye wananchi wa Kasulu Vijijini wakaamua mimi niwe Mbunge wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais. Ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kipindi chake cha miaka minne ambacho kimekuwa ni cha neema kwa Taifa letu la Tanzania. Kipindi ambacho tumeshuhudia safari ya kipekee, safari ambayo inafanana na ile safari ya wana wa Israel wanatoka Misri wanaelekea Kanaani. Sasa, Mheshimiwa Rais, ametukuta tuko jangwani hatimaye tunayo matumaini punde si punde tutafika Kanaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutoa hotuba nzuri, hotuba iliyojaa matumaini, hotuba ambayo ni dawa na hotuba ambayo imejaa dhamira ya dhati kama kiongozi, maana kama kiongozi wajibu wake wa kwanza anawaongoza wananchi wake, lakini pia atawasaidia wananchi kwa kupunguza changamoto zinazowakabili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa kipindi chake cha miaka minne ameonyesha mwelekeo wa kiuongozi wa Taifa ambao nimetangulia kusema tunaelekea Kanaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kiongozi pia ametatua changamoto zetu zinazotukabili kama Watanzania ambazo zingine zilikuwepo na zingine zimeibuka wakati tupo kwenye safari. Changamoto hizo Mheshimiwa Rais amepambana nazo kuhakikisha safari yetu inakuwa ni rahisi na nyepesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa kipindi chake cha miaka minne ametatua changamoto mbalimbali. Ukizungumzia nishati, umeme mpaka vijijini. Ukizungumzia afya, zahanati na vituo vya afya mpaka vijijini. Ukizungumzia elimu, shule zimejengwa, zikiwepo shule za kimkakati za wasichana. Pia, ukizungumzia kwa maana ya uchukuzi na ujenzi, barabara zimejengwa, pia kuna meli mpya zimejengwa. Kuna ndege mpya zimenunuliwa. Ukija kwenye kilimo utamkuta tena Mheshimiwa Rais pembejeo, wananchi wetu wanafurahia ni shangwe vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utazungumzia pia msukumo wa Serikali kuwekeza fedha nyingi kwenye kilimo ikiwemo kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji. Katika haya hivi ndivyo vilikuwa vikwazo vikubwa ambavyo ukiangalia vingetukwamisha sisi kwenye safari yetu kama Taifa kufika Kanaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumze pia kidogo kwenye baadhi ya vipaumbele vya Mheshimiwa Rais, lakini pia nishauri. Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake amezungumzia sekta ya uzalishaji. Kwenye hotuba yake amegusa kilimo, pia amezungumzia na viwanda. Ninamuunga mkono kwenye hili pia ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuziona sekta hizi mahsusi za uzalishaji kitaifa. Taifa letu na nchi yetu tunalo eneo kubwa la ardhi ambalo linakidhi kilimo, ufugaji, pia tuna maeneo ya kutosha ya kujenga viwanda vya kimkakati ambavyo vinaweza vikatutoa kama Taifa kutoka hatua moja kwenda nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nisisitize kwenye kilimo. Ningeshauri kama Taifa tuwe na vitu vichache vya kimkakati. Kwa mfano, tunaweza tukasema tunapambana na kilimo na viwanda kama Taifa, tuhakikishe tunasukuma sekta hizi mbili kufika mahali kama Taifa katika kipindi cha miaka mitano kama Mheshimiwa Rais alivyoeleza kwenye hotuba yake. Kwenye kilimo tunaweza tukaweka msukumo kwenye mazao ya kimkakati, tunaweza tukachagua mazao kadhaa ya biashara kwa mfano chai, pamba mkonge, lakini pia na tumbaku. Mazao haya yanaweza yakatupatia fedha nyingi ya kigeni kama Taifa, lakini pia itatusaidia kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia kwenye kilimo. Kuna changamoto nyingine kwenye issue ya masoko. Ninaomba niishauri Serikali ikiwezekana tujitahidi kuongeza nguvu kwenye matumizi ya TEHAMA ili kurahisha wananchi wetu ku-access masoko hata wakiwa vijijini. Kwa mfano, Wizara ya Kilimo inaweza ikawa na software application ambayo uki-click kwa mfano mahindi au uki-click mchele, utaona mchele Dodoma unauzwa kiasi gani, kama ni maharage utaona Dar es Salaam yanauzwa kaisi gani, utaona kama ni Kongwa au wapi maeneo mengine ili mwananchi atofautishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwenye Jimbo langu mimi ilifika sehemu maharage yanauzwa mpaka shilingi 1,000, lakini wakati huo huo ukija Dar es Salaam ni shilingi 3,500 na ukija Dodoma shilingi 3,000. Kwa hiyo, mwananchi aki-click mambo yanakwenda vizuri anaweza akajua kitu gani cha kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumaliza ninaomba nishauri pia kwenye suala la ajira na upotevu wa mapato. Ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kunijaalia kufikia siku ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninamshukuru Mheshimiwa Rais tena kwa kuniteua mimi kijana mdogo hapa Bungeni kwa Wabunge wa jimbo ukiachana na wale wa Viti Maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kuchangia kwa upande wa hali ya uchumi. Hali ya uchumi kwa ripoti za World Bank na pia hotuba ya Waziri Mkuu, ni ya kuridhisha hasa kwenye ukuaji wa uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi unakua kwa zaidi ya asilimia sita. Pia, hali ya umaskini inaonyesha unaelekea kupungua. Kwa ripoti ya mwisho, tulikuwa tumeshafika 26%, lakini pia, unemployment rate nayo inaonekana kwamba imepungua iko chini ya asilimia mbili nukta nane.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mazuri ambayo yanafanyika kwenye Taifa letu, nilitamani nishauri baadhi ya vitu hasa kwenye uchumi wa Taifa letu hapa. Ukiangalia kwenye ripoti kwa mujibu wa World Bank, pia na NBS (Shirika letu la Takwimu Tanzania), uchumi wetu umechangiwa kwa sehemu kubwa tatu, hasa primary activities zikiongoza zikiwa na 42.9%, lakini secondary activities zikiwa na 19.7%, lakini tertiary activities zikiwa na 37.4%.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, kwenye shughuli hizi za msingi ambazo zinaendesha uchumi wetu, ni pamoja na kilimo na madini, hasa shughuli zinazohusisha ardhi kama resource. Mimi ninafikiri nishauri hapa. Ukiangalia kwa uchumi wetu kwa takwimu za World Bank, uchumi wa dunia ulikua kwa wastani wa asilimia tatu nukta tatu kwa mwaka 2025, lakini uchumi huu ulikuwa hasa unaongozwa na sekta hasa za teknolojia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi uchumi wetu unaongozwa kwenye shughuli za msingi. Yaani hata ile secondary kwa maana ya manufacturing, ku-process zile raw materials, malighafi zinazotoka huko kwenye kilimo au kwenye madini, uchimbaji kule, huko inaonekana hali bado ni ndogo. Tuna 19.7% tu peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, hii nipongeze juhudi zinazofanyika kwenye kilimo. Tunapozungumzia kilimo ni pamoja na kufungua maeneo hasa ya vijijini kwa sababu 60% kwa takwimu zilizopo wananchi wengi wanajishughulisha na kilimo. Kwa Taifa hili tuna nguvu kazi zaidi ya milioni 32. Milioni 32 hii kuna zaidi ya 97% ambayo iko kwenye informal sector. Watu hawako kwenye sekta rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, yaani less than 10 percent, vijana wengi wanapata ajira kwenye formal. Maana yake tukichukua vijana ambao wana-graduate kama zaidi ya 700,000 mpaka kwenda 900,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka, chini ya 10% ndiyo wanaoweza kupata kwenye formal sector, lakini wengine waliobaki almost 90% plus, wote wanaenda kwenye informal sector.
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake hapa ukija kwenye Taifa letu maana yake ukija tena kwenye dependency ratio inaonyesha Taifa letu bado lina utegemezi mkubwa. Yaani tuna kundi kubwa ambalo linategemea kundi dogo. Zaidi ya 80% ni kundi ambalo bado ni tegemezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, mapato tunayojisifia kwa Taifa hili, maana yake mapato mengi yanakusanywa na kundi dogo, lakini liko kundi kubwa ambalo halichangii chochote, pengine hatujalitambua kama sekta rasmi. Ukijumuisha bodaboda na wengine, yaani kama Taifa, bado hatujapata utambuzi rasmi wa kuwatambua kundi hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie kwenye remittance. Kwa takwimu za World Bank bado zinaonyesha Tanzania sisi kwa Afrika Mashariki inaonekana ndiyo tunashika mkia kwa kupokea hela ndogo kutoka kwa diaspora kutoka nje ya nchi. Wameweka wazi kwamba sababu kubwa inayosababisha mpaka tunakuwa na kiasi kidogo ni gharama ya kutuma fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ndiyo tuna gharama kubwa, ni miongoni mwa nchi tatu zinazotoza kiasi kikubwa Barani Afrika. Kwa hiyo, ninafikiri kama Serikali kuna haja pia kuliangalia hili. Tupunguze gharama ili na sisi tuweze kushindana na Mataifa mengine ili watu walioko nje angalau wawe wanaweza kutuma chochote kwenye Taifa letu na sisi tuweze kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna issue ya consumption kwenye matumizi. Kwenye Government Consumption, matumizi ya Serikali inaonekana yanaongezeka kutoka kwenye Real GDP, lakini ukija kwenye private kwa maana ya personal, mtu mmoja mmoja inaonekana matumizi yanapungua. Mara ya mwisho inaonekana ilikuwa 3.4 percent of Real GDP.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hiki kitu nacho tena inaonyesha kwamba wananchi wa kawaida kule hali inazidi kuwa mbaya, hawana fedha mfukoni. Kwa hiyo, nini kinatokea? Maana yake pengine wananchi hawa, wengine ndio ambao wamefanya tender hawajalipwa, wengine labda wamefanya mambo fulani fulani kwa Serikali bado hawajalipwa. Kwa hiyo, kama Serikali, lazima tuangalie pia namna ya kuhakikisha wananchi wanakuwa na chochote kitu mfukoni ili consumption iweze kwenda vizuri iendane na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Serikali inakuwa na fuko la kutosha kufanya matumizi, pia watu binafsi nao wawe na fedha mfukoni za kufanya matumizi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Malizia Mheshimiwa, muda wako umeisha.
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, okay. Kwa kumalizia, ninaomba nizungumzie issue ya NIDA na Force Account. Kwa ...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, usianze jambo jipya, malizia tu sentensi ya mwisho.
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Wakati ninamalizia ninaomba niishauri Serikali pia iongeze issue ya suala la NIDA kwenye majimbo yetu hasa, ni changamoto kubwa sana. Kwa hiyo, Serikali ipambane.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)