Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Ukiniuliza swali la haraka haraka nimegundua nini kwenye hotuba ya Waziri Mkuu? Nimegundua ni hotuba ambayo kama hujaijua, Serikali ya Chama cha Mapinduzi unaweza ukasahau tabu zote. Ni hotuba moja, kwa kuizungumza ni hotuba nzuri sana, unaweza ukasahau tabu zote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naweza nikasema neno moja kabla sijaenda kwenye hoja yangu. Kama hotuba hiyo itaenda kutekelezwa, ukiilinganisha na hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyohutubia Bunge kwa mara ya kwanza, sijui huwa kinatokea nini hapa katikati, sijui ndio machawa wanaharibu mchongo! Kwa sababu speech ni nzuri, lakini njoo kwenye utekelezaji, tunapoteana, matatizo ndio yanaanzia hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitasema kwa nini speech ni nzuri na utekelezaji wake ni mgumu kwa hoja zangu zifuatazo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza, tumesema dira yetu inasema uchumi na ajira lengo ni kukuza uchumi na ajira. Leo hii utakuzaje uchumi na ajira ya nchi hii wakati changamoto yoyote ikitokea mtu wa kwanza kumtazama wa kufidia ile changamoto ni mwananchi wa kawaida?
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ukianzisha hata biashara ya maandazi, umefungua kioski hapo kesho, utakutana na Osha, utakutana na watu wa afya, utakutana na TRA, utakutana sijui na mtu anaitwa Mipango Miji, utakutana na mtu wa Leseni ya Halmashauri, kodi zaidi ya sita. Huyu kijana ambaye mmempa shilingi milioni mbili unamtoaje hapo? Swali dogo tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tuna wawekezaji ambao wanakuja kuwekeza kwenye nchi hii. Wale tunawapa grace period, yaani eti tunawapa miaka 10 ya kuchechemea wajitafutetafute. Wakishachuma miaka 10 imeisha, wanaondoka anauza kampuni, ameenda na fedha zetu, tunapiga hesabu gani? Tunapiga hesabu gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, issue za kodi ambazo kimsingi nimeshazungumzia kidogo hapo, nchi hii inakodi nyingi, na kama ina kodi nyingi, nilitarajia kwenye changamoto za ghafla zinazojitokeza kwenye nchi hii, kwa sababu Mungu ametujalia kila kitu kwenye nchi hii, kila kitu hata ukitaka mwanamke mzuri, mdada mzuri, mbaba mzuri, wapo; ametupa madini, ametupa mito, ametupa maziwa, ametupa madini kila kona; Njombe ndio kuna madini haijawahi kutokea; lakini leo wafadhili wametoka kufadhili UKIMWI, tumechukua ile kodi, mimi nimenunua gari. Ndiyo maana najua, mwananchi wa kawaida anayenunua gari ndio akafidie gharama za matibabu ya Virusi vya UKIMWI na kudhibiti UKIMWI, kisa USA wamejiondoa kwa 100%.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ni kwamba tunahitaji kuwasaidia hawa watu, je, kama Serikali, ndiyo limekuja ghafla, wafadhili wametoka, kwa nini tufikirie mtu wa kufidia ni mwananchi? Kwa nini tusifikirie kwamba zile akiba zetu, yale madini yetu ya Njombe tukayachimbe yafidie hiki kitu? Mmeingiza kodi, mmeingiza gharama za madawa ya UKIMWI kwenye kodi tena za wananchi, yaani huyo huyo anaumwa, huyo huyo mnajidai mnamsaidia, halafu mnamchukua hela yake yenyewe mkamnunulie dawa.! Tunafanya kitu gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kilimo. Sisi Mkoa wa Njombe Mungu ametubariki tuna kila kitu. Sasa Mungu ametubariki zaidi; ninavyozungumza hivi, Waziri wa Kilimo anatokea Njombe, lakini Mwenyekiti wa Kamati ya Biashara na Viwanda ni Mheshimiwa Deo Mwanyika Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, lakini ndiyo mkoa pekee unaoongoza kwa migogoro ya ardhi, unaoongoza kwa wawekezaji wa viwanda. Kunyanyasa wananchi wa Njombe, hawalipi, kuna huyo Mwekezaji wa Chai anaitwa DL, kila siku ni kelele.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amekuja Njombe akamwagiza yule mwekezaji kuwalipa wale wafanyakazi, na akampa masharti nafuu ya kuchukua fedha CRDB benki, lakini mpaka leo hawajalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliangalia muda wangu, sihujumiwi leo. Niliangalia, nilianza na dakika 27, kwa hiyo, zimeisha dakika nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa jambo lingine…
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sigrada, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Taletale.
TAARIFA
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mwongeaji, Wenyeviti na Mawaziri wapo kwa niaba ya Bunge na Kamati, siyo kwa niaba ya mikoa yenu, ahsante.
MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa subiri. Taarifa unaipokea?
MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, siwezi kuipokea kwa sababu hakuna nilichokosea. Hatuwezi kukataa kwamba Waziri ni Serikali, lakini Mwenyekiti wa Bunge ana maamuzi kwenye jambo hilo. Kwa hiyo, siwezi kuipokea taarifa na muda wangu unilindie.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hoja nyingine ni ardhi. Tunalalamika hapa migogoro ya ardhi. Kwenye speech ya Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumzia migogoro ya ardhi. Mnatatuaje migogoro ya ardhi, hampangi miji, na mna Maafisa Mipango wa Miji, mna Maafisa Ardhi wa Miji, mnatatuaje changamoto ya ardhi ambayo Njombe mpaka leo Hakimu wa Mahakama ya Ardhi mkoa mzima yupo mmoja? Ukianza kesi yako leo, mpaka unajifungua mtoto miezi tisa, anazaa na vijukuu na vijukuu kesi yako Mahakamani haijaisha mnatatuaje? Hamtaki kupima ardhi, hati leo hii kutafuta ardhi kwenye nyumba yako ni bora kutafuta mwanamke wa kuoa kuliko kutafuta hati. Utatafuta hiyo hati miaka mitatu. Mchumba unamwahidi tu, keshokutwa nakuoa, unampata, kwenye nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilindie muda wangu. Jambo lingine ni elimu. Hii Tanzania ni moja, tuna mifumo ya elimu miwili. Mtu mwenye hela kidogo, na siku hizi kwenye nchi hii ukiwa na hela unafuatiliwa kuliko maskini. Yaani badala ya kujadili maskini tunamsaidiaje ajinyanyue, tunajadili hivi hili gorofa huyu mtu amelitoa wapi? Yaani natamani Serikali iumize kichwa kujadili kwa nini Tanzania ina umaskini na si…
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu.
KUHUSU UTARATIBU
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, hili Bunge lina utaratibu wa kuzungumza. Sasa humu ndani utafikiri tunagombana. Tunaomba anayetoa hoja azungumze kiustaarabu, tutamwelewa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, endelea.
MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nafikiri ni sauti ambayo Mwenyezi Mungu amenijalia. Mwombe Mwenyezi Mungu, amekujalia kitu kingine, pengine amekupa mwenzangu mwili, mimi amenipa sauti, lakini nina maana nzuri. Kila mtu Mungu amempa karama yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tumezungumzia utawala bora. Nakumbuka Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano aliahidi issue ya Katiba mpya. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge, tusimchocholeshe, naye anataka kuacha alama kwenye nchi hii, lakini sasa hivi mmembana mmembana, mnamsogelea sogelea ili ajisahaulishe, ili itakavyofika 2031 mje hapa mseme watu wote waliahidi Katiba hawakuleta, ila wewe umeleta; atakayekuja, tunawajua! Tunawajua!
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba, mimi binafsi na wananchi wa Mkoa wa Njombe, tunaomba msimamo wa Mheshimiwa Rais wa kufanya nchi hii iwe na utawala bora, na kwenye hili naomba asiyumbishwe. Hiyo ndio legacy pekee itakayomfanya Mheshimiwa Dkt. Samia akumbukwe na siyo kusikiliza watu. Eti mkileta Katiba mpya tutatoka madarakani! Aliyesema mtatoka, ni nani? Ni ninyi mtekeleze mlichoahidi, hakuna mtu atatoka kama mtatekeleza. Simple tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, issue nyingine…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sigrada, muda wako umeisha naomba umalizie.
MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie. Wengine walikuwa wanapewa grace period, nipendelee tu yatima mimi.
NAIBU SPIKA: Malizia Mheshimiwa, muda umekwisha.
MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi zisizotekelezeka …
NAIBU SPIKA: Usianze jambo jipya Mheshimiwa, malizia tu.
MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ahsante, naheshimu kiti, ahsante sana nitaongea siku nyingine.
Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii ili niweze kuchangia kwa ufupi sana Mpango wa Maendeleo 2025/2050. Mimi nina mambo machache sana ambayo yamekuwa yakisumbua kwa muda mrefu sana. Kuna issue ya vijana na akinamama na hiyo mikopo ya 10%. Kuna changamoto kubwa sana kwenye hii mikopo na changamoto siyo kwamba fedha hazipo, lakini pia changamoto siyo kwamba wananchi wanashindwa kukidhi vigezo
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ambayo nimeiona ni complications za namna ya kuipata hiyo mikopo. Hiyo mikopo imekuwa na complications nyingi sana. Complication ya kwanza walengwa kabisa watu wa chini hawaipati hiyo mikopo, lakini ukweli ni kwamba hiyo mikopo vinaundwa vikundi hewa vya watu wenye access ya kuifikia hiyo mikopo kwa kutanguliza watu ambao siyo walipaji na ndiyo maana ikija kusumbua, halmashauri zinapoanza kufuatilia zile fedha haziwaoni wahusika, ndiyo maana wanakutana na kitu kinaitwa vikundi hewa. Huo ndiyo ukweli, kwa sababu taarifa za hizi fedha haziwafikii watu ambao ni walengwa kule chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu kwenye huu Mpango ambao unaendelea ambao unahusisha na haya mambo pia; kuna mtu alishauri hapa, hizi fedha ziwe na mlango maalum. Nimeona sasa hivi Serikali imepitisha hela upande wa wanawake na watoto kupitia Waziri wa Mambo ya Wanawake na Watoto; pia na Vijana; kuna fedha zimepitia kwa Waziri wa Michezo na Utamaduni (Mheshimiwa Makonda); kuna fedha zimeenda huko CRDB na NMB; na kuna fedha zinapitia halmashauri. Hivi vitu vinatuchanganya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia masharti ya hizi fedha, Wizara ya Michezo ina masharti yake; halmashauri wana masharti yao na ukija hizi fedha za NMB zina masharti yake. Kuna watu wamesema ni fedha ambazo hazina riba. Ukiangalia ule mwongozo unasema zile fedha zina riba ya asilimia saba. Ushauri wangu, kwa nini Serikali isitoke na format ya pamoja ili kusiwe na lugha tatu utafikiri kuna Serikali saba kwenye nchi moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hizo fedha ambazo zinapatikana NMB, kwanza kuna mwongozo ulitolewa na Serikali kwamba watu wanaotakiwa kukopa hizo fedha ni watu ambao mtaji wao ni chini ya shilingi milioni nne. Ukiangalia hao watu maana yake ni watu ambao ni wajasiriamali na ninakumbuka kipindi cha Hayati Magufuli alitoa formula nyepesi sana kwamba watu ambao mitaji yao ni shilingi laki mbili, tatu, nne na tano (chini ya shilingi milioni nne) wawe na vitambulisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ni hii hii miaka 65, lakini ule mpango ule baada ya Mheshimiwa Magufuli kufariki ule mpango nao haupo. Wale wajasiriamali wadogo wadogo wamerudishwa tena kwenye shilingi elfu sita kila mwezi, kitu ambacho tunawachanganya watu. Unavyowaambia tena hawa watu wawe na leseni wakati ukiangalia sheria ya kodi inamtambua mfanyabiashara ambaye ana mtaji wa kuanzia shilingi milioni nne kwenda juu. Hawa watu wamesema wawe na mtaji wa chini ya shilingi milioni nne. Huyu tax clearance anaitoa wapi? TIN Number anaitoa wapi? Leseni ya biashara anaitoa wapi? Wakati huyu wamemchukulia kama ni mjasiriamali mdogo ambaye analipa ushuru wa halmashauri husika. Kwa hiyo, kuna contradiction ambazo zinafanywa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu, tuwe na formality iliyo wazi ambapo watendaji wa vijiji na mitaa watawaambia direct watu wao. Hizo hizo fedha, kwa mfano za halmashari, wale wakopaji wa vikundi wawe wamechapisha mpangokazi wao. Baadaye watu wamechapisha wameenda kukopa fedha wakawaambia hapana hatutaki mpango uliochapishwa tunataka mpango ambao umeandikwa kwa mkono. Halafu hizo hizo fedha wanakopesha hawa watu wenye ulemavu. Masharti waliyoyaweka kwa watu wa kawaida wameweka na kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mtu hawezi hata kutembea, yeye amekaa tu pale kutembea hawezi unamwambia atoke kule Makete, nilikutana na walemavu Mheshimiwa Festo wanatoka kilometa karibu kumi na kitu kwenda halmashauri kupeleka hizo documents. Masharti ni yaleyale tofauti yake ni kwamba mlemavu anaweza kukopa peke yake, lakini masharti ya mwanasheria, sijui iandikwe. Mtu haoni unataka aandike ataandikaje na asaini mwenyewe kwa mkono wake? Kwa hiyo, issue siyo fedha, fedha ninaamini zipo, issue ni complications za namna ya kuzipata hizo fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, sisi Njombe Mungu ametubariki sana. Ninapata shida kuona Taifa kama la Tanzania ambalo tumebarikiwa kila kitu eti tunakosa fedha. Tunakosaje fedha nchi ambayo Njombe pale wilaya zaidi ya nne zina madini. Sisi kule Makete kuna madini, Ludewa kuna madini, Njombe Mjini pale kuna madini, lakini ukiangalia kwenye taarifa zenu nchi nzima wamefanya survey 16% tu ya sehemu ambazo tunamiliki madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi leo hii Njombe hatukutakiwa kuwa na miradi yenye miaka sita haijakamilika. Haikutakiwa Njombe tukose hela za kukamilisha eti Barabara ya Ludewa – Njombe. Mimi huwa ninatafakari kwamba, hivi kweli huwa tunakaa mezani na kutafakari kwamba hii nchi tumebarikiwa? Ile Njombe ile, tuna miradi ya maji 2008 imekwama. Njombe ambayo ukiitazama kila kona, kila baada ya kilometa moja unakutana na mto, kila baada ya kilometa unakutana na mto. Huku mto, huku mto na huko mto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kampeni nilitafakari kitu kimoja. Wananchi wamefanikiwa kutoa maji bondeni kwenda kwenye vipalila. Sisi kule tuna kilimo maarufu kinaitwa vipalila, viazi vya kumwagilia. Mwananchi ndani ya siku 10 ameshatega maji mtoni ameyapandisha juu kwenye mashamba yake eka 20.
(Hapa kengele ya kwanza ililia)
MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika zangu zimeisha?
MBUNGE FULANI: Endelea.
MHE. SIGRADA W. MLIGO: Okay sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikawa ninajiuliza inawezekanaje mkulima wa viazi tena darasa la pili anapandisha maji kutoka mtoni ndani ya siku kumi amesambaza kwenye shamba lake la viazi halafu Serikali ina mradi wa 2008 na haujakwisha mpaka leo! Hivi inawezekanaje? Nikagundua, unajua Mheshimiwa Musukuma kuna vitu anaongea lakini ukimsikiliza vizuri unakuta kuna logic ingawaje huwa tunamcheka kidogo. Iko hivi, unakuta mkulima wa kawaida ambaye hana shule ana maarifa kuliko sisi ambao tuna PhD na degree. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikasema basi inawezekana tuwe tunajifunza basi hata kwa hao watu ambao wao hawakwenda shule ila ni wakulima. Kwa hiyo, ninavyozungumza hivi na ninaipa ushauri Serikali kwamba, tunavyokwenda kutekeleza hii mipango basi tuangalie hata ile miradi ambayo ilikuwepo toka enzi hizo za Kikwete na Magufuli. Kuna miradi hiyo Njombe labda kama hamna taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Mradi wa Maji unaitwa Igongwi wa 2008. Haya ukija kwenye issue nyingine, kwa mfano uwanja wa ndege, mimi nimekuwa Diwani 2015 niliukuta uwanja wa ndege upo kwenye mipango kwamba tunataka Uwanja wa Ndege Njombe. Sasa hivi Njombe tuna wawekezaji wakubwa sana wanahitaji hiyo ndege ili waweze kusafirisha mazao yao na kuwahi issues zao. Mtu wa Njombe unaweza ukamkuta amevaa ndala lakini ana billions. Kwa hiyo, kupoteza shilingi milioni moja kwenda Dar es Salaam akawahi deal la shilingi milioni 800 haoni shida. Njombe wanahitaji ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkatuambia Baraza la Madiwani litafute eneo, mwaka 2015 hiyo. Tukatafuta eneo, na lipo mpaka leo, lakini mkatuambia tusimamishe wale wanaopatikana katika maeneo ya karibu, na hilo eneo ambalo tumehama, sasa wasiendeleze maeneo yao. Maskini, tukawasimamisha watu wanaoishi karibu na uwanja wa ndege kwa hoja kwamba, tunataka kuupanua. Miaka zaidi ya mitano wanasubiri tupanue uwanja, hatujawahi kupanua. Baada ya hiyo miaka mitano kwisha tumerudi tena, tunasema aah, aah, hapa hatupanui, tumehama, tunaenda Uwanja wa Ndege Kibena huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninavyozungumza hivi, hii issue ya Uwanja wa Ndege wa Njombe aliyoizungumzia Mheshimiwa Deodatus siyo ya jana, labda kwa sababu hawa Mawaziri ni wapya. Mimi nimeingia kwenye Baraza la Madiwani mwaka 2015, nimeikuta. Kuhamisha Uwanja wa Ndege tumepitisha sisi, na eneo tumetafuta sisi. Kwa hiyo, ninashauri, tunaomba uwanja wa ndege haraka, siyo stori mpya. Ni miaka 18 sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninaishauri Serikali…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda umeisha, ahsanteni sana. (Makofi)