MHE. MGORE M. KIGERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Je, Serikali haioni wakati sahihi umefika kuhakikisha wanakamilisha makubaliano na kusaini mkataba na mwekezaji huyo ili kuweza kutekeleza ahadi yake kwa wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini, kukuza ajira na uchumi wa Musoma Mjini kupitia kiwanda hiki cha MUTEX?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Ni lini Serikali itawalipa waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho cha MUTEX kwani tangu mwaka 1994, wafanyakazi hao wamekuwa wakiidai Serikali fedha zao? Ninashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninachukua nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Mgore Miraji Kigera, Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, kwa kuendelea kufuatilia kwa ukaribu sana kuhusu hiki Kiwanda cha MUTEX ambacho kimsingi, kama kitafufuliwa, kitakuwa na tija sana kwa wananchi wa Musoma Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme, Mheshimiwa Mbunge amekuwa akitusumbua sana na amefuatilia kwa karibu sana kuhusu hiki kiwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, ninaomba kujibu maswali mawili yaliyoulizwa na Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nia na dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunavutia wawekezaji, na sisi kama Serikali tumejipanga, maeneo yote yale ambayo kimsingi yapo idle, hayafanyi kazi, tunatafuta wawekezaji ili tuweze kuhakikisha tunawekeza. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa Dira yetu ya 2050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia hilo, na sisi tumeona kuna haja sasa ya ku-fast track process ya kuhakikisha kwamba huyu mwekezaji anasaini mkataba kwa haraka. Pia tutamsimamia, tutampa performance contract, ili ndani ya muda mfupi tuone uwekezaji unaanza katika Jimbo la Musoma Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo vikubwa ambavyo tunaviweka kwa sasa hivi, kwanza tunataka mwekezaji atakaposaini mkataba, atoe commitment, ni lini ataanza kuwekeza katika eneo la Musoma Mjini? Pili, ni kiasi gani cha ajira atakuja kuzalisha? Tatu, tunataka achangie katika mnyororo wa thamani, hususan katika Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Ni kweli kulikuwa kuna wafanyakazi ambao walikuwa wanafanya kazi katika kiwanda cha MUTEX, takribani 935. Kati ya hao, wafanyakazi 856 walishalipwa mafao yao na wafanyakazi 79 walikuwa bado hawajalipwa mafao yao. Hawa 79 hawakujitokeza wakati wa uhakiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii sasa kuwataka wale wote 79 ambao hawakujitokeza, wakati tunafanya uhakiki, wapeleke nyaraka zao kwenye ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, wahakikiwe na baada ya kuhakikiwa Serikali itakuwa tayari kuwalipa. Ahsante.
MHE. MGORE M. KIGERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninapenda kutoa pongezi nyingi sana na shukrani kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwathamini wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini, kwani tunategemea sana Ziwa kuliko kitu chochote. Hivyo, kwa kuwezesha vijana wetu kupata mikopo ili waweze kufanya ufugaji kwa weledi mzuri, wataenda kufungua fursa ya ajira na mzunguko wa fedha na uchumi utakuwa Musoma Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: Je, ni nini kauli ya Serikali kuhakikisha inawathamini wafugaji wa samaki kwa kupitia vizimba? Kwani wamekuwa na changamoto kubwa sana kwenye suala zima la upatikanaji wa vifaranga vyenye ubora pamoja na chakula. Kwa kuwa changamoto ya chakula huwa ni shida, inapelekea samaki wengi waweze kudumaa na wafugaji hawa kupata hasara kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, samaki anafugwa kwa miezi nane, wanatarajia apate kilo moja and above, lakini kwa sasa hivi samaki wanafubaa na kupata 0.6 kg mpaka 0.8 kg. Kwa hiyo, ni nini mpango wa Serikali kuwawezesha wafugaji hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Je, kauli ya Serikali ni ipi kuhakikisha inawasaidia vijana kupata ujuzi pamoja na mikopo ili waweze kuanzisha upatikanaji wa chakula wenyewe katika Manispaa ya Musoma na waache kutoa chakula Kenya pamoja na Kibaha? Kwani ni mwendo mrefu na gharama ya chakula inakuwa ni kubwa sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Ninarudia tena kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa bidii yake kubwa ambayo anaendelea nayo kufuatilia miradi hii ya vizimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la vifaranga na chakula, kama nilivyozungumza hapo awali, tunaendelea na harakati za utatuzi wa changamoto hizi tulizokuwanazo mwanzo. Moja, tumeendelea kuhamasisha sekta binafsi katika kuwekeza, kuzalisha vifaranga na kutengeneza viwanda vya chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakiri kwamba tumekuwa na ongezeko kubwa sana la vifaranga pamoja na chakula ambacho kimesaidia wafugaji wetu kwa njia ya vizimba kuweza kupata kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tunaendelea kuwapa vijana wetu elimu ya utambuzi ili pale wanapoona vifaranga na chakula sokoni waweze kutambua kile kilicho bora against kile ambacho hakipo bora. Pia, tumeendelea kurekebisha mifumo yetu ya utoaji wa mikopo ambapo hapo awali tulikuwa na wazabuni wa moja kwa moja ambao tulikuwa tunaelekeza vijana wetu kwenda kwao kwa ajili ya kujipatia vifaranga na chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa vile tumeongeza upatikanaji wa vifaranga na chakula, tumeongeza uwazi ili kijana aweze kuingia sokoni na kuchagua kifaranga na chakula kilicho bora kwa ajili ya samaki wake aweze kupata samaki walio bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, kuhusu uwezeshaji wa vijana kujipatia ujuzi na mitaji ya kuwekeza katika uzalishaji wa chakula, hiki ndicho ambacho tunafanya mpaka sasa. Tunaendelea kuhamasisha vijana wetu kuandaa maandiko ili ile elimu tunayowapatia tunapokuwa tunawaandaa kwa ajili ya kuingia kwenye ufugaji wa vizimba kupitia taasisi zetu za FETA na programu zetu za BBT-Uvuvi, waweze kuitumia kwa ajili ya kuzalisha chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, waandae maandiko wapeleke katika Halmashauri zetu waweze kunufaika na fedha za 10% na pia waandae maandiko wapeleke katika taasisi zetu za fedha ili waweze kupata mikopo ya kuwekeza katika uzalishaji wa chakula kwa sababu ni fursa kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, Wizara tumeandaa mwongozo wa utengenezaji wa chakula cha samaki ili kila anayetaka kuwekeza katika sekta hii ya uzalishaji wa chakula cha samaki aweze kupata wepesi wa uwekezaji huo, na sisi kama Wizara tunaendelea kutoa msaada wa utaalam na maelekezo kwa yeyote ambaye anahitaji kufanya uwekezaji katika uzalishaji wa chakula cha samaki ili tuongeze upatikanaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)