MHE. MGORE M. KIGERA aliuliza: -
Je, upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha mwekezaji wa Kiwanda cha MUTEX anaanza uzalishaji kwa haraka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgore Miraji Kigera, Mbunge kutoka Musoma Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Musoma Textile Mills Tanzania Limited (MUTEX) kilianzishwa kwa lengo la kuongeza thamani ya pamba iliyozalishwa nchini, kutoa ajira na kuchangia maendeleo ya viwanda katika Ukanda wa Ziwa Victoria na Tanzania kwa ujumla. Hata hivyo, hadi sasa kiwanda hiki hakifanyi kazi, na hivyo kinasimamiwa na Msajili wa Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika juhudi za kufufua kiwanda hiki, Serikali ilipokea maombi ya mwekezaji mwenye nia ya kuwekeza kwenye eneo hili. Hivyo basi, Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, walianza mara moja mchakato wa kufanya majadiliano na mwekezaji huyo ambapo pande zote mbili zilifikia makubaliano kuhusu masharti mapya ya uwekezaji. Kufuatia makubaliano hayo, rasimu ya mkataba iliandaliwa na kuwasilishwa kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya mapitio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa mchakato wa kufanyia kazi maboresho yaliyopendekezwa kwenye mkataba unaendelea na mara tu utakapokamilika, mkataba utasainiwa rasmi kati ya Serikali na mwekezaji. Hatua hiyo itafuatiwa na kukabidhiwa kwa kiwanda pamoja na nyaraka zote za umiliki kwa mwekezaji ili aweze kuanza utekelezaji wa uwekezaji na kurejesha uzalishaji wa kiwanda hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. MGORE M. KIGERA aliuliza: -
Je, Serikali ipo tayari kutoa mikopo kwa wafugaji wa samaki wa vizimba Musoma ili kutoa ajira kwa vijana?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ninaomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Mgore Miraji Kigera, Mbunge wa Musoma Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) inaendelea na zoezi la utoaji wa mikopo ya pembejeo za ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ambapo katika mikopo ya awamu ya kwanza jumla ya vizimba 47 vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.126 vimetolewa, kama mikopo ya masharti nafuu isiyo na riba kwa wanufaika 130 nchini ikiwemo vijana kutoka Musoma Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa kuongeza ushiriki wa vijana katika ufugaji wa samaki kwa vizimba, Wizara inatekeleza Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT-Uvuvi) kwa kutoa mafunzo kwa vitendo na mikopo yenye masharti nafuu. Lengo ni kuongeza uzalishaji na kutoa ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara imepokea kiasi cha shilingi bilioni saba kutoka Hazina kwa ajili ya kuwezesha vijana kupata mitaji kupitia mikopo yenye masharti nafuu. Fedha hizo zitatumika kukopesha vijana 308 waliohitimu mafunzo hayo wakiwemo vijana 14 kutoka Musoma Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Wizara inatarajia kupokea sehemu ya shilingi bilioni 200 ambazo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ndani ya siku 100 zitakazoelekezwa katika kuwezesha mikopo ya vizimba. Katika mgao wa fedha hizo, vijana wa Musoma watafaidika na mikopo hiyo. Aidha, Wizara inaendelea kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kuendelea kutoa mikopo ya ufugaji wa samaki kwa vizimba katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.