Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ahmed Mabkhut Shabiby (1 total)

MHE. YOHANA S. MSITA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON na kwa kuwa Tanzania utaratibu wetu ni kuwa na wachezaji wa kigeni 12 kwenye kila timu, sasa ninataka kujua, nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha wachezaji wazawa wanapewa nafasi ya kucheza muda mwingi ili kuimarisha timu yetu ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Msita kwa swali zuri. Ni kweli kumekuwa na ongezeko la wachezaji wa kigeni kwenye vilabu vyetu ambavyo vinacheza ligi kuu, lakini nimhakikishie uwepo wa wachezaji hao wa Kimataifa, moja ya mambo ambayo wamekuja kufanya ni kuongeza viwango vya ushindani na kuongeza ubora wa wachezaji wetu wa ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama unaweza kuona kwenye timu zetu kubwa, wachezaji wa ndani ambao wameweza kuwa wana uwezo wa kupata namba na kuziwakilisha timu hizi, wamekuwa wanatumika sana kwenye timu ya Taifa kwa vile viwango vyao vinakuwa vya kiushindani zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa wachezaji wa Kimataifa vilevile umefanya timu zetu kufanya vizuri kwenye mashindano makubwa ya vilabu Barani Afrika na hivyo vimesaidia kukua kwa kiwango cha soka letu. Kwa hiyo, kunazo juhudi mbalimbali ambazo tunaendelea kuzifanya ikiwamo mpango wa kuanzisha ligi ya wachezaji wa ndani pamoja na kuanzishwa kwa ligi ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika, tunaendelea kuimarisha mashindano ya UMISSETA, UMITASHUMTA pamoja na timu zetu za vijana ili kuhakikisha tuna wachezaji wa ndani ambao wana uwezo wa kushindana kuiwakilisha nchi yetu kwenye michezo ya Kimataifa.