Supplementary Questions from Hon. Zainab Rashid Kawawa (3 total)
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Katika Mkoa wa Lindi, Halmashauri za Wilaya za Liwale, Nachingwea, Ruangwa, Mtama pamoja na Kilwa, hazina masoko ya kisasa. Je, ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba Halmashauri hizi zinajengwa masoko ya kisasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, utaratibu wa masoko ya kimkakati huwa yanaanza na andiko kutoka kwenye Halmashauri husika. Andiko hilo huwasilishwa TAMISEMI, nasi kwenye Wizara yetu hufanya mapitio na baadaye kulipeleka kwenye Wizara ya Mipango ambao wakiridhia hulifikisha Wizara ya Fedha kwa ajili ya kupatiwa fedha na kuanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, hivyo, kwa uhitaji alioutaja Mheshimiwa Mbunge wa Mkoa wa Lindi, ninawaelekeza Wakurugenzi wa maeneo yote yaliyotajwa kuwa na ushirikiano na wawakilishi wa wananchi ili kufuata hatua hizo na hatimaye Serikali iweze kuwahudumia wananchi wa maeneo hayo.
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Wilaya ya Liwale katika Mkoa wa Lindi wanatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa kutuletea fedha za ujenzi wa barabara ya kilometa 10 kwa Barabara ya Liwale – Nangurukuru. Barabara hii ina jumla ya kilometa 231. Pia barabra hii ndiyo kitega uchumi kikubwa sana kwa wanachi wa Liwale pamoja na wa Wilaya ya Kilwa...
SPIKA: Mheshimiwa twende kwenye swali.
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Rais sifa moja kubwa aliyokuwa nayo ni kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa zaidi ya 100%, je, ni lini sasa tutafuta kilio cha wananchi wa Wilaya ya Liwale kwa kutukamilishia ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami ili sasa Wilaya ya Liwale iweze kuunganishwa na wilaya nyingine kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Lengo la Wizara, na kama alivyosema Awamu ya Sita ni kujenga barabara zote na hasa zinazounganisha barabara kuu na makao makuu ya wilaya ama makao makuu ya wilaya na makao makuu ya mkoa, ikiwepo hiyo Barabara ya Nangurukuru – Liwale kilometa 231.
Mheshimiwa Spika, tumeshaanza kutoa hizo kilometa 10, lakini kikubwa zaidi katika hiyo barabara Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami, kulikuwa na changamoto kubwa sana za madaraja. Sasa tumejenga madaraja mengi sana katika huu mpango wa dharura ambao unaendelea kukamilisha ili kuhakikisha kwamba wakati tunatafuta fedha ya kujenga barabara yote wananchi hawa wawe na uwezo wa kupita kipindi chote cha mwaka.
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Liwale katika Mkoa wa Lindi haina kituo rasmi cha Polisi na wilaya hiyo ilishatenga eneo kubwa na zuri kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya. Je, ni lini sasa Serikali itatujengea kituo cha Polisi cha daraja A?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Zainab kwa swali lake la msingi la kuomba Kituo cha Polisi cha Wilaya ambapo kwa sasa hakipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuweke vizuri kumbukumbu; kwa kuwa ni Kituo cha Polisi cha Wilaya, maana yake hakitakuwa daraja A, kitakuwa ni daraja B. Kwa hiyo, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunachukua hoja yake, na kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi ni kwamba katika vituo 75 vya wilaya na cha kwake kipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutatoa umuhimu kwenye maeneo ambayo hayana kabisa vituo vya Polisi vya wilaya ili kusudi naye tuweze kumjengea.