Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ZAINAB ABDALLAH ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ukisoma maandiko yanasema, mshukuruni Mungu kwa kila jambo, maana moyo usiokuwa na shukurani hukausha mema yote, lakini ukisoma Quran Surat Sabayi aya ya 13 inasema, "Wa Qalilun Min 'Ibadiya sh-Shakuru" (na wachache ni miongoni mwa wale wenye shukrani).
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya, na ndani ya siku 100 za uongozi wake ahadi ambazo ameziahidi ameweza kuzitekeleza ikiwemo ahadi ya uzinduzi wa bima ya afya kwa wote ambapo tayari imeshaanza kwa awamu ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ameahidi shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo. Fedha hizo tayari zimekwishatolewa, lakini ameahidi mpango wa pamoja wa mafunzo kati ya waajiri, VETA pamoja na vyuo vikuu. Jambo hili tayari limeshafanyika pamoja na gridi ya Taifa ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunasema tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na juzi tumeshuhudia Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano ikisaini mikataba mitano mikubwa kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupata ajira nje ya nchi. Hili ni jambo kubwa sana, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, sisi wote ni mashuhuda, amekuwa akifanya ziara mkoa kwa mkoa, wilaya kwa wilaya, jimbo kwa jimbo, na kote alipopita ametekeleza majukumu yake ipasavyo, na amejenga matumaini makubwa sana kwa Watanzania. Kwa hiyo, sisi tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee tunawapongeza Wizara ambazo zipo ndani ya ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu: Wizara ya TAMISEMI; Kazi, Ajira na Mahusiano; Sera, Bunge na Uratibu, wanafanya kazi kubwa na kazi nzuri sana, hongereni sana viongozi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu, sasa hivi tunatekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, na kwa sasa tunatekeleza Dira ya 2025/2026 kwenda 2030/2031 na msingi wa miaka hii mitano ni ujengaji wa uchumi shindani pamoja na kuzalisha ajira kwa maana ya tunaenda kufanya transformation, economic growth and job creation.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama tunaenda kwenye uchumi shindani, imani yangu kubwa ni kwamba TAMISEMI ni moyo wa Serikali. TAMISEMI iki-paralyse, Serikali ina-paralyse; TAMISEMI ikifanya vizuri, Serikali inafanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaongea hivyo kwa uzoefu. Alhamdulillah nilipata heshima ya kuhudumu kama Mkuu wa Wilaya kwa miaka tisa na nusu. Ninajua kwamba Wizara ya TAMISEMI ni Wizara ambayo inashughulika na sekta zote za maendeleo. Ukienda kwenye mikoa na wilaya, niwapongeze sana Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Ma-RAS, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Ma-DAS, na Maafisa Tarafa, wanafanya kazi kubwa na nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya, maji ya kwake, umeme wa kwake, barabara za kwake, afya ya kwake, na elimu ya kwake. Ndiyo maana nikasema TAMISEMI ni moyo wa Serikali. Kwa hiyo, ninapongeza kazi kubwa na nzuri ambayo imefanyika, lakini yapo maeneo ambayo ninatamani nishauri yaweze kuboreshwa na kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni eneo la uwajibikaji. Hayati Mzee Benjamini William Mkapa alisema uwajibikaji ndiyo msingi wa maendeleo. Wengi waliozungumza, wameelezea ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, na yapo mambo ambayo yalipaswa kushughulikiwa chini, lakini yameenda kwake. Tuna haja ya kufanya reforms kwenye halmashauri zetu. Kama ambavyo tunataka economic reforms katika nchi, ipo haja ya kufanya reforms kwenye halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametuhakikishia kwamba hakutakuwa na business as usual, kutakuwa na business unusual; ili twende kwenye business unusual ni lazima watu waache kufanya kazi kwa mazoea. Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata, na Maafisa Tarafa, hawa watu chini huku wakitimiza wajibu wao vizuri Mkuu wa Wilaya, DAS, Mkurugenzi, Mkuu wa Mkoa, na RAS watakuwa na kazi nyepesi sana ya kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni lazima TAMISEMI sasa ishuke chini kule kwa watendaji kuhakikisha wanawabana kama ni kwa mujibu wa sheria, haiwezekani mtu aharibu hapa apelekwe pale. Watu wanafanya kazi kwa urasimu, jambo la kufanyika kwa siku moja linaweza likachukua miezi mitatu. Haya mambo ni lazima tukubali kuyabadilisha ili tuweze kupiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni eneo la ukusanyaji wa mapato. Ninadhani ndiyo focus kubwa ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba halmashauri zetu zinakusanya mapato. Kwa bahati mbaya sana, ukiangalia ile Idara ya Mapato kwanza watumishi ni wachache, lakini professionalism ni changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta unazungumza na Afisa Mapato wa Halmashauri, hata vipaumbele vyake vitano vya mapato havifahamu. Unamwambia nioneshe Ledger Book, nioneshe Cash Book hana. Unamwuliza, vyanzo hivi vya mapato mara ya mwisho vimekusanywa lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wafanyabiashara wamekaa miaka mpaka 10 hawajawahi kutozwa baadhi ya tozo ambazo ziko kwa mujibu wa sheria za halmashauri. Kwa hiyo, tunaona kabisa hii Idara ya Mapato ifanye reforms, tufanye mageuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunaweza kufanya mabadiliko zaidi kuhakikisha kwamba aidha tunaunda kampuni ambayo itakuwa specific kwa ajili ya kubeba ajenda za kiuchumi, kwa sababu leo hii tunasema tunataka uchumi shindani lakini hatuna blue print ya uwekezaji kwenye wilaya zetu. Ukienda kwa Mkurugenzi, ukimwambia nioneshe maeneo ya uwekezaji, atakutajia kwa mdomo, lakini hatuna blueprint ya uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kongani za viwanda, maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kujenga hoteli, maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kilimo kikubwa cha kisasa, hayo mambo digitalized hayapo. Kwa hiyo, ni muhimu sana kuangalia jinsi gani tunaweza kuimarisha Idara ya Fedha ili tubebe ile ajenda ya Mheshimiwa Rais ya kusema kila wilaya tuwe na viwanda vya kimkakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini huku chini tukiweka vizuri, tutakuwa na viwanda kwenye kila wilaya, na bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa ndani, tutazizalisha sisi wenyewe. Hatuna sababu ya kuagiza vitu nje ya nchi ilhali sisi kama Watanzania ndani ya nchi tuna uwezo wa kuvizalisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameahidi ajira 8,000,000 kama tukiwa na business mind tukawa strategically located. Ninawahakikishieni, tuna uwezo wa kukusanya fedha nyingi sana kupitia Serikali za Mitaa. Shilingi trilioni moja hii ni ndogo kulingana na uhalisia wa vyanzo vilivyopo, mipango miji wakifanya kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tuna issue ya (PPP) Public Private Partnership. Tukishirikisha wadau wa sekta binafsi kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya kimkakati ndani ya halmshauri zetu, tuna uwezo wa kukusanya mapato makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, John F. Kennedy aliwahi kusema: “Don’t ask what America has done for you? Ask how much you have done for the Americans?” Nami ninairudisha kwetu Watanzania, tusiulize Tanzania imetufanyia nini? Hebu sisi tujiulize tumeifanyia nini Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono, ahsante sana. (Makofi)
Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. ZAINAB ABDALLAH ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Spika, wewe Naibu Spika, pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania kwa kuaminiwa na kwa kazi kubwa na nzuri ambayo mnaendelea kuifanya katika kututumikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nichukue fursa hii kuwashukuru sana, vijana kutoka mkoa wa Kaskazini Pemba na pia Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Taifa kwa kunichagua, pia, Kamati Kuu kupitia Mwenyekiti wetu wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kunithibitisha kuwa Mbunge wa Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka niwaahidi vijana, nitaendelea kuwa msemaji wao, daraja lao na Serikali, lakini kuhakikisha changamoto zao tunazifikisha na zinapatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma Surah Ar-Rahman, Aya 55:60 inasema: “Hal jaza ul ihsan illal ihsan.” Je, kuna malipo ya wema kwa mtu anayekutendea mema zaidi ya wewe kumtendea mema. Ukisoma Zaburi 136:1 inasema, “Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema kwa maana Fadhili zake ni za milele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kwa niaba ya vijana, kutoa shukrani zetu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anayoifanya kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu, na kwa kasi kubwa ya miradi ya maendeleo katika Taifa letu. Leo sisi ni mashuhuda, hakuna kijiji, hakuna kata, na hakuna wilaya utakayoenda usikute miradi iliyoachwa kama alama na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, iwe kwenye elimu, iwe kwenye afya, iwe kwenye maji, iwe kwenye miundombinu ya umeme, barabara, mawasiliano, Uchumi wa Buluu, utalii, kila sekta kama hujakuta alama ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, basi wewe utakuwa hujaizunguka Tanzania na hujatembelea vijiji kuona hayo maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mwanadiplomasia na nimekuwa nikifuatilia hotuba za viongozi mbalimbali ndani ya Afrika na hata nje ya Afrika. Ninataka niwathibitishie Wabunge kwamba hotuba ambayo ameiwasilisha Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 14 Novemba, 2025 ni kati ya hotuba bora kabisa kuwahi kutokea ndani ya Bara la Afrika. Mheshimiwa Rais ana mapenzi makubwa sana na Watanzania. Mheshimiwa Rais kupitia hotuba ile ameonesha uzalendo na utu wa kuwatumikia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama kijana ninapata faraja kwa sababu hii inaonesha kwamba Mheshimiwa Rais anatambua kwamba 76% ya Watanzania iko chini ya umri wa miaka 36 ambao ni vijana. Kupitia hotuba ile Mheshimiwa Rais ameonesha mahaba na mapenzi makubwa sana kwa vijana wa Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia hotuba ile, kwa mara ya kwanza kwenye historia ya nchi yetu, Mheshimiwa Rais ameunda Wizara ambayo ipo chini ya Ofisi ya Rais inayohusika na Maendeleo ya Vijana. Kwa kweli leo tunaye Waziri wa Vijana Mheshimiwa Joel Nanauka, ninaomba nimpe maua yake, anafanya kazi kubwa na kazi nzuri sana kuwatumikia vijana wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Mheshimiwa Rais ameenda mbali kusema kwamba ataweka washauri chini ya Ofisi ya Rais watakaoshughulikia maendeleo ya vijana. Ninataka niseme jambo moja, katika maeneo ambayo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais yamenigusa sana moyo wangu ni pale Mheshimiwa Rais alipoonesha kwamba anataka uwajibikaji, na uadilifu Serikalini. Anatamani kuona watendaji wetu wakiwa na nidhamu wakiwajibika na wakiwatumikia Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia hotuba ile, Mheshimiwa Rais amesema: “Ninawaelekeza Mawaziri hadi Maafisa Tarafa wawe karibu na wananchi waende kusikiliza na kutatua kero za wananchi,” na watakaposhindwa kufanya hivyo, yeye atachukua hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inanikumbusha kauli ya Baba wa Taifa mwaka 1961 pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema yafuatayo: “Those of you who have received this privilege, therefore have the duty to repay sacrifices which others have made.” Ninyi ambao mmebahatika kupata fursa hii, mna jukumu la kuhakikisha mnawajibika ili kujitoa kwa wale ambao wamejinyima ili ninyi leo muwe hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka niwaambie viongozi na watendaji wenzangu, Watanzania tupo 60,000,000, lakini leo wewe umepata heshima ya kuwa Waziri, leo umepata heshima ya kuwa Mkuu wa Mkoa, leo umepata heshima ya kuwa Mkuu wa Wilaya, leo umepata heshima ya kuwa Mkurugenzi, Afisa Tarafa, au Mtendaji Kata, ninataka utambue dhamana ambayo umepewa, una wajibu wa kuhakikisha unarudisha fadhila kwa wale ambao wamejinyima ili wewe uwe hapo kwenye hiyo nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kupitia mabaraza ya kazi anayoyaendesha, ametoa mwelekeo wa namna Serikali itakavyojipambanua. Amesema siku ya leo hapa, watumishi wote wanaofanya kazi kwa mazoea, watumishi wote ambao hawatimizi wajibu wao, na watumishi wote ambao badala ya kuwa suluhu ya kutatua migogoro, wao ndio wanakuwa sehemu ya kuongoza migogoro. Hawa watumishi hawatavumiliwa na Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kwenda mbali zaidi na kutaka tu-review sheria zetu ili wale ambao wanadhani wakiharibu sehemu moja wana uwezo wa kupelekwa sehemu nyingine hao waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Hao watu ndio wanaotia doa Serikali yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa na nzuri sana, lakini baadhi ya watumishi, baadhi ya viongozi wasioitakia mema nchi yetu, wasiokuwa na utayari wa kulitumika Taifa letu, ndio wanaomhujumu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri ambao mmepewa dhamana, tunawaamini na hatuna mashaka na ninyi. Nendeni mkawasimamie watumishi ili waweze kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama Mbunge ambaye ninawakilisha kundi la vijana, ninatambua ya kwamba changamoto kubwa ya vijana ni ajira, lakini ninataka niwaambie vijana wanaonisikiliza huko mitaani, hakuna nchi duniani ambayo imemaliza tatizo la ajira. Maendeleo ni hatua, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipambanua leo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kupitia hotuba yake kwamba atahakikisha kunakuwa na kongani za viwanda kwenye kila wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia viwanda hivi, vijana watapata ajira, Serikali itakusanya mapato, na nchi yetu itapiga hatua kimaendeleo. Mheshimiwa Rais ameahidi kutoa shilingi 200,000,000,000 kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake. Mitaji hii itaenda kuwakwamua vijana kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Mheshimiwa Rais ameahidi ujuzi kuhakikisha kwamba, kwa sasa tuna VETA 64 kwenye wilaya 64. Ahadi ya Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha kila wilaya kwenye wilaya 139 nchini kutakuwa na Vyuo vya VETA na vijana watafungamanishwa na miradi ya kimkakati ili waweze kupata ujuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameahidi kutakuwa na kampasi kila mkoa ili tunapokuwa na Vyuo Vikuu kwenye mikoa hii, vijana wetu waweze kupata elimu na ujuzi, lakini kuweza kuchagiza uchumi kwenye mikoa husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, ninaomba nihitimishe kwa nukuu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema haya yafuatayo: “Kwa wanangu vijana wa Taifa la Tanzania, nchi hii imejengwa kwenye misingi ya amani na utulivu wa kisiasa; sisi wazazi wenu tungeshawishika kuyafanya mliyoyafanya wakati huu nchi hii isingekuwa na neema na maendeleo mnayoyaona hii leo. Hivyo, ninawasihi wanangu vijana, nchi hii ni yenu, kwa shida zozote zile zinazowakabili, msikubali hata siku moja kushawishiwa kuichoma nchi yenu wenyewe. Msikubali kukata tawi la mti ambalo mmeukalia. Msikubali kabisa. Ninyi ndio walimu na wajenzi wa Taifa hili, ninawasihi vijana, kamwe msiwe wabomoaji wa Taifa lenu.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)