MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
SPIKA: Mheshimiwa ni swali moja tu.
MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Spika, sawa. Ninaomba majibu kutoka kwa Serikali kuhusiana na Barabara ya Kasulu, barabara ambayo itakwenda kuwasaidia wananchi wa Kata za kama Machinjioni, Rubuga, Kagera pamoja na Kata ya Majengo. Barabara iliyopo sasa hivi inawalazimisha wananchi hawa wakitaka kwenda kwenye kata zao lazima wafike mjini halafu warudi nyuma. Ikijengwa Barabara hii ya Kasulu kuanzia pale Msimba kuelekea Ujiji itasaidia wananchi hawa wasiingie mjini wapate shortcut ya kwenda kwenye makazi yao. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge Baba Levo, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tuna wakala mbili za barabara, TANROADS na TARURA. Mheshimiwa Mbunge, Barabara tunazozijenga sisi ni kuanzia Ujiji hadi Kigoma Mjini, Mwanga kwenda Mwandiga, pale kwenye Sanamu ya Sokwe kwenda Simbo na Mwandiga. Hizi barabara nyingine tutahakikisha kwamba tunawasiliana na wenzetu wa TARURA ili kuhakikisha hizo barabara zinajengwa na wananchi wasipate changamoto kama alivyozielezea Mheshimiwa Mbunge. Ahsante. (Makofi)
MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu kutoka kwa Naibu Waziri wa Kilimo, mimi ninasikitishwa sana na hiki kinachoendelea katika huu mradi wa Bonde la Mto Luiche.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zimekopwa Kuwait tangu mwaka 2018. Ukienda pale mpaka leo hii ninavyoongea na wewe, anavyosema Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba mradi umeanza, wako wanafyagia miaka nane. Miaka nane tangu tumekopa fedha mpaka leo hii wako wanafyagia tu, wanasema wanakusanya vifaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri, kama itampendeza, twende wote akajionee vituko vinavyoendelea pale katika Bonde la Mto Luiche. Fedha tumekopa, tumechukua Kuwait, tena fedha hizi alizipambania Mheshimiwa Zitto Kwabwe, alikuwa ndio Mbunge. Mheshimiwa Zitto kamaliza muda wake, mradi haujatekelezwa, kaja Mheshimiwa Ng’enda Kilumbe...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, uliza swali la nyongeza.
MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la nyongeza, ninaomba Serikali, tufunge nayo safari kwenda kwenye Bonde la Mto Luiche wakaone kwa macho waache maneno ya kuhadithiwa. Twende naye Naibu Waziri aende pale akaone kwa macho yake nini kinachoendelea pale katika Bonde la Mto Luiche. Hilo ndilo ombi langu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Baba Levo, Mbunge wa Kigoma Mjini kwa concern yake, na sisi kama Wizara tunaelewa hayo anayoyaeleza. Jambo moja tu nimthibitishie, tutaenda kabla hili Bunge halijaisha, tutaongozana, tutakwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutapanga moja ya weekend tutafika eneo la mradi, lakini kwa kifupi tu nieleze kwamba, kwa nini mradi huo umechelewa? Hayo anayoyaeleza ni kwamba changamoto ilikuwa ni upatikanaji wa fedha na ndiyo maana Tume ya Umwagiliaji mwaka 2025 ilifanya mapitio upya ya huu mradi, na sasa hivi mradi huu tunautekeleza sisi wenyewe kupitia fedha za ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza hivi sasa ni kwamba kuna kama shilingi bilioni 8.89 ambazo tutazitoa kwa mkandarasi kama sehemu ya malipo mengine ya awali ili kuhakikisha kwamba mradi huu unaenda kwa wakati. Matarajio yetu kabla mwaka 2030 mradi huu utakuwa umekamilika na Baba Levo atawaeleza wananchi kwamba moja ya jitihada zake kubwa alizozifanya Bungeni ni kuhakikisha mradi huu umekamilika kwa vitendo. (Makofi)