MHE. ASMA ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, na pia ahsante sana Waziri kwa majibu yako mazuri uliyonipa. Ninaomba niongezee maswali mawili kama yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mkakati gani mahususi wa kuhakikisha kuwa ushirikiano katika Bodi hizi mbili za Utalii wa Tanzania na Kamisheni ya Utalii wa Zanzibar inaleta chanya ya moja kwa moja ya ongezeko la ajira kwa vijana wa Tanzania hususan vijana na wanawake, lakini kipekee vijana wa Jimbo la Welezo?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ninaomba kuuliza. Je, Serikali italeta lini viashiria vya mafanikio (KPIs) vinavyopima ongezeko la utalii, mapato na ajira katika kupitia ushirikiano katika Bodi hizi mbili ya Utalii wa Tanzania pamoja na Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze kwa maswali mazuri ya msingi Mheshimiwa Asma Ali Mwinyi Mbunge wa Welezo. Pia nimthibitishie tu kama nilivyojibu katika swali la msingi, moja, Serikali ya Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika swali la msingi tumeshaonesha kwamba tumeshasaini mkataba wa makubaliano kwa maana ya MoU katika kukuza Sekta ya Utalii nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la makubaliano hayo ni kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya watalii, na watalii wengi wanakaa muda wa kutosha hapa nchini. Kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza ajira kwa vijana, hususan katika maeneo kama ya kuongoza watalii, malazi, usafiri, pamoja na sanaa (uchongaji wa vinyago pamoja na picha).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hayo tu ni sehemu ya mambo ambayo tunayafanya katika kuongeza ajira hususan kwa vijana na wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kuhusu viashiria vya mafanikio ambavyo Serikali imekuwa ikifanya, kupitia taasisi zetu za Kiserikali ndani, kwa maana ukiangalia taasisi ya Benki Kuu ya Taifa, Uhamiaji, Bodi ya Utalii na Kamisheni ya Utalii Zanzibar zimekuwa zikitoa chapisho la kila mwaka kwa maana linalotoa zile taarifa za mwenendo wa utalii hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, tumekuwa tukitumia kitu kinaitwa Visitor Tourism Exit Survey (utafiti mdogo pale watalii wanapotoka nchini) ambayo imekuwa ni sehemu ya kuonesha ule mwenedo na viashiria vya watalii hapa nchini. Kwa hiyo, hayo ni maeneo ambayo unaweza kwenda ukapata hizo KPIs ambazo Mheshimiwa Mbunge amezieleza.