Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Suleiman Mohamed Rashid (2 total)

MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID: Mheshimiwa Spika, ahsante nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini pamoja na majibu hayo nina swali la nyongeza. Serikali haioni haja kuandaa mwongozo wa dharura wa uboreshaji ambao utaweza kuzingatia kulipwa kwa posho ya kujikimu pamoja na posho maalum kwa walimu ambao wanasahihisha mitihani hiyo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiboresha maslahi ya walimu wanaosahihisha mitihani kulingana na upatikanaji wa fedha ambapo pamoja na posho wanazolipwa Serikali pia hulipa malazi, chakula, matibabu wakati wote wa kazi. Hata hivyo, ushauri wa Mheshimiwa Mbunge tumeupokea. (Makofi)
MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini kipekee nimpongeze yeye pamoja na Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo wanamsaidia Mheshimiwa Rais kwenye hili suala la elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na mahitaji ya taaluma ya akili unde, Serikali imejipangaje ili taaluma hii kuweza kusomeshwa katika maskuli (shule)?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na kwa ruhusa yako ninaomba nimjibu Mheshimiwa Suleiman Mohamed Rashid, Mbunge wa Jimbo la Mwera, swali lake la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile ambavyo Serikali imejipanga katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, ndivyo ambavyo Serikali imejipanga katika kuhakikisha kwamba kwa upande wa elimu ya akili unde, mikakati mbalimbali imeendelea kuchukuliwa. Kwa mfano, matumizi ya TEHAMA na teknolojia nyingine miongozo mbalimbali imetolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miongozo imetolewa katika kutekeleza teknolojia za kidijitali katika elimu msingi, vyuo vikuu na vyuo vya ualimu. Pia kuna utekelezaji wa AI katika masomo, lakini pia Serikali imekuwa ikitoa ufadhili wa fursa za masomo ya nje ya nchi, lakini pia tumeendelea kuimarisha miundombinu ya elimu ya juu ili kuona kwamba mazingira ya watoto wetu ya kujifunzia yanaendana na mahitaji halisi ya teknolojia ikiwemo elimu ya akili unde. (Makofi)