MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha maslahi na stahiki za Walimu wanaosahihisha Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne na Sita?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniteua na kuniamini katika nafasi hii ya kumsaidia Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Suleiman Mohamed Rashid, Mbunge wa Mwera. Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne na Sita ni mitihani muhimu ambayo usahihishaji wake hufanyika kwa baadhi ya walimu kukusanywa katika vituo maalum kwa ajili ya jukumu hilo unaozingatia muda maalum, usalama, usiri, mazingira wezeshi na ubora wa kazi.
Mheshimiwa Spika, stahiki za Walimu wanaosahihisha Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne na Sita hulipwa kwa kuzingatia miongozo ya usahihishaji wa Mitihani kwa kipindi husika. Ili kuleta ufanisi wa kazi hiyo, miongozo hiyo imeendelea kuboreshwa mara kwa mara. Serikali itaendelea kuboresha maslahi na stahiki za walimu katika usahihishaji wa mitihani ya Taifa ili kuimarisha na kuongeza ufanisi wa kazi hiyo.
MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID aliuliza:-
Je, Serikali imejipangaje katika utekelezaji wa Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la 2023?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Suleiman Mohamed Rashid, Mbunge wa Mwera kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejipanga kikamilifu katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 sambamba na mitaala iliyoboreshwa kwa kufanya yafuatayo:-
(i) Kuongeza miundombinu kwenye shule zilizopo;
(ii) Kuendelea na ujenzi wa shule mpya zikiwemo shule za mkondo wa Amali;
(iii) Kutoa mafunzo kazini kwa walimu ili kuendana na mahitaji ya mtaala mpya;
(iv) Kuimarisha uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari; na
(v) Kutoa ajira mpya za walimu ambapo katika mwaka 2024/2025 kibali cha ajira mpya 12,678 kilitolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali imezindua rasmi Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu na Mpango wa Pamoja kati ya Waajiri, Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Vyuo Vikuu ili kuwawezesha wahitimu kuwa na ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa. Aidha, Serikali inafanya mapitio ya Sheria ya Elimu Sura 353 ili kuendana na mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023.