Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Edward Olelekaita Kisau (4 total)

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Kibaya – Kisima kilometa 50 walisema wataijenga kwa kiwango cha lami. Kipindi hiki cha mvua wananchi wa Kiteto wamesumbuka sana. Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? Ninakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge, barabara hii ambayo ni ya kipande cha kutoka Handeni – Kibirashi – Kibaya kwenda kwa Mtoro kilometa 50 Kibaya – Kisima, tunachosubiri tu sasa hivi ni kumpa mkandarasi malipo ya awali ili aweze kukijenga kipande hicho cha kilometa 50.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkandarasi yupo tayari, tumeshapeleka maombi yetu Hazina ili aweze kulipwa malipo ya awali aanze kazi, ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Bajeti ya Mwaka 2025/2026 tulipitisha Barabara ya kutoka Kibaya – Kisima kilometa 50 zijengwe. Je, ni lini barabara hii inaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, barabara hii tunategemea kupatikana kwa fedha. Tayari sisi tumeshaomba fedha za awali ili mkandarasi aweze kulipwa, na akishalipwa, basi kazi hiyo ya kuanza kuzijenga hizo kilometa 50 itaanza.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi. Mheshimiwa Naibu Waziri Mradi wa Nchinilai – Engusero umechukua muda mrefu sana na unasuasua sana. Ni lini Naibu Waziri yuko tayari, kwa siku ambazo siyo nyingi sana tutembelee mradi huu ili tupate majibu ya uhakika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Olelekaita, na hakika tunapokuwa katika ziara jimboni kwake anatupatia ushirikiano mzuri sana, na pia tunapohitaji taarifa za maendeleo ya miradi yetu ndani ya jimbo lake anatupatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hivyo, nipo tayari kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji kwenda kutembelea mradi huu na kuupa push ili uweze kukamilika na wananchi wake wa Kiteto wapate huduma ya majisafi na salama, ahsante sana.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kiteto ina Mahakama kongwe sana ya muda mrefu. Tumeshaleta maombi na tukaambiwa ipo kwenye bajeti ya 2024/2025. Nini kauli ya Serikali kuhusu majibu ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya kisasa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Olelekaita Edward ambaye amekuwa akifanya ufuatiliaji wa mambo mengi sana katika sekta hii muhimu ya sheria.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake kuhusu ujenzi wa Mahakama hii ya Wilaya ya Kiteto, kama nilivyotangulia kusema, kwa wakati huu Mahakama inatekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Mahakama ikiwemo Mahakama za Wilaya. Mahakama hii ya Wilaya ya Kiteto ipo katika mpango huu wa pili na tayari tenda ilishatangazwa kwa ajili ya kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hii.

Mheshimiwa Spika, kwa wakati huu bado majadiliano yanaendelea kwa ajili ya kusaini mkataba ili sasa ujenzi wa Mahakama ya kisasa kabisa uweze kuanza na wananchi wa Mheshimiwa Mbunge wapate majengo mazuri kwa ajili ya huduma za Kimahakama.