Supplementary Questions from Hon. Dr. Regina Christopher Malima (3 total)
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti,
kwanza kabisa nishukuru kwa majibu mazuri ya Wizara, na
niipongeze Serikali kwa sababu kuna uwekezaji mkubwa sana
umefanyika katika sekta ya elimu. Kuna mikakati mingi imefanyika
na Serikali ya Awamu ya Sita, lakini nina maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na miradi
hii ya kimkakati kutoa ajira kwa vijana, je, Serikali ina mpango wa
kuweka Sera au miongozo itakayolazimisha miradi yote ya uwekezaji kutenga asilimia maalumu ya ajira za kitaalamu kwa
wahitimu hawa wa vyuo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA
MAHUSIANO (MHE. RAHMA R. KISUO): Mheshimiwa Mwenyekiti,
ninakubaliana na mwuliza swali 100% kuwa miradi ya kimkakati
imeonesha uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira. Hata hivyo, Sera za
Ajira zinaelekeza ajira zitolewe kwa ushindani bila kutoa
upendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri
Mkuu, Wizara ya Kazi, Ajira, na Mahusiano inaendelea kusimamia
utekelezaji wa Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni (Na.1) ya
Mwaka 2015, ambapo pamoja na mambo mengine inaelekeza
wafanyakazi wa kigeni yaani wataalamu kurithisha ujuzi kwa
wazawa katika ajira za kitaalamu ili pale kibali cha kazi cha
wageni kitakapokwisha, mzawa aweze kuchukua nafasi husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali itaendelea kutoa
kipaumbele kwa wafanyakazi wazawa katika miradi ya kimkakati
kwa nafasi za kazi ambazo utaalamu wake siyo adimu katika soko
la ndani ya ajira. (Makofi)
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Nina swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri kuhusiana na Bandari ya Nansio katika Kisiwa cha Ukerewe. Bandari hii pia, imechakaa, imechoka, haijawahi kufanyiwa ukarabati tangu uhuru. Wakati mwingine hali ya hewa ikiwa ni mbaya meli pia zinapata shida kuweza kupaki. Kwa hiyo, ninaomba kujua, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa Bandari hii ya Nansio katika Kisiwa cha Ukerewe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka anapoingia madarakani Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 2021, takribani bandari 80 zilikuwa zinatambuliwa na kurasimishwa. Kutokana na umuhimnu wa sekta ya bandari, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo maalumu na mahususi kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Wizara ya Uchukuzi kwanza, tufanye urasimishaji. Tumekamilisha urasimishaji na bandari zimeongezeka mpaka 142.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili ni kuanza kutafuta fedha, kuboresha bandari moja baada ya nyingine. Namwomba Mheshimiwa Malima awe na Subira, Bandari ya Nansio ni moja kati ya bandari muhimu kwenye Taifa letu. Tutakwenda kuifikia pindi fedha zitakapokuwa zimepatikana.
MHE. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaunganisha wahitimu wa vyuo vikuu na fursa za mikopo hii ya 10%, ili na wao waweze kujiajiri pindi wanapomaliza masomo yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mbunge ni swali muhimu sana, lakini Serikali ilishaanza kutekeleza. Ninakumbuka miaka miwili iliyopita nilifanya ziara katika Halmashauri ya Nyamagana ambapo vijana wahitimu walijiunga pamoja, wakaanzisha kituo cha afya na wakapewa mkopo wa 10% na wakaendelea kuendesha kituo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Dar es Salaam imefanya hivyo, wapo walimu ambao wamekopa, wamefungua tuition center na wanaendelea kufanya hivyo. Kwa hiyo, Serikali inawapatia fursa kupitia dirisha la mikopo ya 10% kwa vijana kupitia Halmashauri zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwahamasisha vijana wahitimu kote nchini kwamba waunde vikundi vyao, waende kuomba mikopo kwenye Halmashauri kulingana na taaluma zao, waanzishe shughuli zao kwa sababu dirisha lipo wazi kwa ajili yao, na lina faida kubwa kwa sababu wao wenyewe wanapata ajira, na pia wanaajiri vijana wengine katika maeneo hayo.