MHE. THOMAS K. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kulingana na umuhimu wa chuo hiki, je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha ili kukamilisha ujenzi huo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kabla sijaja Bungeni, nilitembelea mradi huo wa ujenzi, mradi huo hauridhishi. Je, Waziri yuko tayari kwenda kujionea halisi ya mradi na kutoa msukumo ili mradi ukamilike kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako ninaomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa ufuatiliaji wake juu ya maendeleo ya Chuo hiki cha Mlele, lakini pia nimpongeze nimepata taarifa kwamba yeye ndiye Mwenyekiti wa Wabunge wapya katika Bunge hili. Kwa hiyo nimpongeze kwa nafasi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya awali, kwamba kati ya bilioni 1.6 ambazo zilizotengwa, bilioni 1.032 tayari zimeshatumika. Kwa hiyo bakaa iliyobaki siyo kubwa sana na Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya kumalizia vyuo hivi na kuanza ujenzi pia wa vyuo vingine. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Maganga kwamba, fedha zitaenda na chuo hicho kitamalizika katika awamu ya pili. Ahsante
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, niko tayari kwenda na kuangalia maendeleo ya chuo hiki.
MHE. THOMAS K. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Kwa mujibu wa mkataba wa mradi huo, mkataba unatarajiwa kukamilika Juni. Kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, mpaka sasa mradi uko 10%, je, Serikali ina kauli gani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza kwa ufuatiliaji wa karibu sana wa utekelezaji wa mradi huu; na pili, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu utekelezaji huu unaenda sambasamba na kukagua huu mradi mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika, mradi huu ulichelewa kwa sababu ya changamoto ya kifedha, na sasa Serikali imeshatatua changamoto hiyo. Baada ya kuwa wamepelekewa fedha, wakandarasi wameanza kwa kasi kubwa.
Mheshimiwa Spika, tutatendelea kufuatilia kwa ukaribu sana, na vyombo vyetu vya usimamizi viko kule vinasimamia vizuri, wataalamu wetu, watendaji wakuu, Mheshimiwa Waziri pia anaendelea kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika kwa wakati na wenye thamani halisi ya fedha, kwa kuhakikisha kwamba ubora wake uendane na mahitaji halisi ili wananchi wa Jimbo la Mheshimiwa Kampala wapate huduma ya maji iliyokusudiwa.