MHE. THOMAS K. MAGANGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Chuo cha VETA Halmashauri ya Wilaya ya Mlele – Katavi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Thomas Kampala Maganga, Mbunge wa Katavi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Mlele ambacho kinatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2026. Hadi sasa Serikali imeshatumia jumla ya Shilingi Bilioni 1.032 kati ya Shilingi Bilioni 1.6 zilizotengwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza. Mpaka sasa, ujenzi huo umefikia 73%.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga na kupokea fedha ili kuwezesha ujenzi wa chuo hiki kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa mafunzo kama ilivyopangwa.
MHE. THOMAS K. MAGANGA aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha malipo ya mkandarasi wa Mradi wa Bwawa la Nsekwa ili akamilishe kazi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Thomas Kampala Maganga, Mbunge wa Jimbo la Katavi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kufuatia ujenzi wa Bwawa la Nsekwa kufikia hatua nzuri, Serikali inaendelea na ujenzi wa mradi wa miundombinu ya kutibu na kusafisha maji yanayotokana na bwawa hilo lililopo Wilayani Mlele Mkoa wa Katavi. Utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa 10% na unatarajia kuwanufaisha zaidi ya wananchi 68,426 waishio katika vijiji 16 vya Wilaya ya Mlele.
Mheshimiwa Spika, mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.5, ambapo tayari Serikali imelipa fedha za malipo ya awali (advance payment) kiasi cha shilingi 226.5 kwa mkandarasi na yupo eneo la kazi akiendelea na utekelezaji wa mradi.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali itaendelea kupeleka fedha za utekelezaji wa mradi huo kadiri hati za madai zitakavyowasilishwa ili kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.