Contributions by Hon. Thomas Maganga Kampala (3 total)
Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. THOMAS K. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ili niweke mchango wangu kwenye hoja mahususi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa letu. Kwanza, nichukue fursa hii kumpongeza sana Waziri, kaka yangu Profesa Alexander Kitila Mkumbo, kwa wasilisho zuri, lakini pia nichukue fursa hii kumpongeza Waziri wa Fedha naye kwa andiko zuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika hakuna Taifa duniani liliwahi kuendelea bila kuwa na mpango. Mzee wangu Profesa Muhongo amechangia vizuri sana mchana hapa; ametupitisha tulikuwa wapi, tumetoka wapi, tumefika wapi na wapi tulianguka na akatoa suluhisho la tutanyanyukaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mpango huu ninataka nijielekeze moja kwa moja kwenye kilimo. Ni ukweli usiopingika kilimo ndicho kinaajiri Watanzania wengi nchi hii. 70% ya Watanzania wameajiriwa kwenye kilimo. Ni lazima Serikali ichukue hatua za makusudi kuwekeza kwenye kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ndiyo njia pekee ya kutusaidia kuweka mazingira mazuri ya kusababisha vijana wengi wanaotoka vijijini wasitoke vijijini kukimbilia mjini. Tukiwekeza vizuri kwenye kilimo na vijana wengi vijijini wakavutika na kilimo, mjini kutapunguza wimbi kubwa la vijana ambao hawana ajira. Niwaombe sana, kaka yangu Profesa Kitila Mkumbo ninamshukuru na ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameanza kwa mfano kuwekeza kwenye kilimo. Ni lazima Serikali iamue kwa makusudi kufanya proper investment kwenye irrigation schemes. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule Jimbo la Katavi tuna maeneo 13 ambayo yanafaa kwa kilimo cha umwagiliaji na imefanyika study, wamekuja watu wa kilimo wamefanya study na wakathibitisha kuwa kweli yanafaa. Ninamwomba Waziri atakapokuja wakati anafanya majumuisho atueleze ana mpango gani kwenye eneo la kilimo. Ameeleza vizuri kabisa, Mpango huu unaokwenda unakwenda kubadilisha kilimo kutoka kwenye kilimo cha kujikimu kuja kwenye kilimo cha biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana naye, sisi Katavi tuna zao la tumbaku ambalo linafanya vizuri. Leo hii ninavyoongea mwaka jana wakulima wa tumbaku wa Jimbo Katavi wamelima kwa kiwango kikubwa na wamepata fedha nyingi sana wakahamasika kulima. Hivi ninavyoongea wakulima wa tumbaku wa Jimbo la Katavi wamejipanga kulima badala yake imekuja notice kwenye vyama vya ushirika wapunguze kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo tunajipanga kwenda kwenye kilimo cha biashara, wakati huo huo wakulima wetu wanakatishwa tamaa, tunakwenda wapi? Niiombe Serikali sisi Katavi wale wakulima wanalima na ile tumbaku tutalima tutavuna. Wasipotengeneza mpango mzuri wajipange watwambie ile tumbaku wataikoroga juice. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo na mpango wowote ni lazima ujielekeze kwenye miundombinu. Nimeongea mara nyingi na nimeongea na Waziri wa Ujenzi kuhusu Barabara inayotoka Inyonga – Majimoto – Kibaoni – Sumbawanga – Tunduma – Zambia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni ya kimkakati. Barabara hii ni fupi, ambayo itarahisisha Wakazi wa Mkoa wa Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora wanaotaka kwenda Zambia kuliko kupita njia ndefu, ambayo itawalazimisha watoke Mwanza, waje Shinyanga, waje Tabora, waende Singida, waje Dodoma, waende Iringa, waitafute Mbeya kwenda Tunduma mpaka Zambia; badala yake barabara hii ikitengenezwa vizuri mkazi wa Mkoa wa Mwanza atatoka Mwanza – Shinyanga – Tabora, Tabora atakata Sikonge, Sikonge anaingia Inyonga, anaingia Majimoto – Sumbawanga – Tunduma – Zambia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini faida yake? Faida yake ni itawapunguzia wananchi safari ndefu na mlolongo wa safari, ili kwenda Zambia, kwa ajili ya kujiletea maendeleo. Tutapunguza urefu wa safari na wananchi wetu watatumia muda mfupi, kwa ajili ya shughuli za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nichangie tena upande wa VETA. Kama ambavyo wenzangu wamechangia, VETA ni suluhisho pekee litakalowasaidia vijana ambao hawakusoma na waliosoma ili kujipatia ajira. Wakati ambapo sikuwa Mbunge niliwahi kumsikiliza Mbunge mmoja amechangia hapa, alisema mitaala ya VETA ibadilishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuna mafundi simu, mafundi wa gereji, mafundi wa pikipiki na kila kada ina maeneo yake. Wale watu wengi kule hawakusoma, lakini wakipata mafunzo mazuri ya VETA, wakakusanywa vizuri, wale wote watakuwa na certificate ambazo zitawawezesha kwenda mahali na ku-apply kazi wakapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba, tunalo tatizo hapa, kama ambavyo nimesema mwanzo, hakuna nchi ambayo inakwenda bila mpango. Amechangia jana kaka yangu, Mheshimiwa King, akasema tunapopitisha mpango huu ni vizuri tukaweka na Sheria. Usipoweka Sheria maana yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata tatizo, alifariki Rais wetu mpendwa, Dkt. John Pombe Magufuli akaingia Mama Samia Suluhu Hassan, isingekuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ana utashi akakuta hii miradi mikubwa, mama huyu angekuwa ni mvivu, akaacha miradi hii leo tusingekuwa tunaongelea SGR imeanza, leo tusingekuwa tunaongelea Bwawa la Mwalimu Nyerere limeanza, leo tusingekuwa tunaongelea Kigongo Busisi. Haiwezekani miaka yote tunayokwenda tukapata Rais kama Mama Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, atakuja kutokea Rais hapa, wametengeneza mpango hauna sheria na kuna miradi mikubwa kama hii iliyokuwepo, anaamua kuacha anaanzisha ya kwake. Watambana na nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba sana na ninaiomba Serikali yangu, mawazo haya yanayotolewa na Wabunge ni vizuri yakazingatiwa. Kama ambavyo ukirudi kwenye Hansard kule kuna michango mizuri iliwahi kutolewa na Wabunge wakati tunatengeneza BRT Phase 1. Wapo Wabunge waliwahi kuchangia wakasema na wakashauri kuwa, hapa tunapotengeneza, tunapopitisha Jangwani hapa hapafai kuweka terminal panatakiwa kuwekwa daraja, lakini watu hawakusikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wasipokuwa na mpango watakuwa wanakwenda na kurudi. Badala yake sasa leo Jangwani tunajenga Daraja, kwa nini? Hatukusikiliza ushauri na hatukuwa na mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. THOMAS K. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mungu wa Mbinguni kwa kunipa kibali cha kusimama siku ya leo ili nichangie kwenye hotuba nzuri ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo kwa msingi mkubwa inatupa mwelekeo wa tulipotoka na wapi tunakwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; lakini kwa sababu ni mara yangu ya kwanza, ninaomba kuwapongeza sana na kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Katavi kwa kura nyingi za kishindo walizonipa ambazo zimeniwezesha mimi leo kuwa mbele yako hapa kuchangia katika Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais anakuja kwenye Jimbo la Katavi tulimwambia Mheshimiwa Rais kakae kwa kutulia sisi Jimbo la Katavi tutakupigia kura kama tumechanganyikiwa, tulikuwa tunazo sababu. Katika kipindi cha miaka minne tangu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameingia kwenye nafasi 2021 – 2025, Jimbo la Katavi tulipokea fedha shilingi bilioni 27.665 kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Wakati Mheshimiwa Rais anaingia, katika nafasi yake ya urais, Jimbo la Katavi fedha hizi nyingi tuliziwekeza kwenye shughuli za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya elimu, wakati Mheshimiwa Rais anaingia, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele tulikuwa na shule za msingi 13. Katika kipindi cha miaka minne tumetoka shule 13 hadi 29. Tunaposimama hapa tunampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hatuji kufanya mbwembwe, tunapongeza yale ambayo mama huyu amyafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda upande wa elimu hapohapo, elimu ya sekondari amekuta shule za sekondari tano. Hadi mwaka 2021 – 2025, tumetoka kwenye shule za sekondari tano mpaka 11 katika kipindi cha miaka minne. Hizi tano ninazoziongea ni tangu uhuru, hizi sita ni katika kipindi cha miaka minne; kwa nini tusimpongeze mama huyu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya afya, wakati mama huyu anaingia 2021 – 2025 tulikuwa na vituo vinavyotoa huduma za afya tisa; leo katika kipindi cha miaka minne vituo vya afya vinavyotoa huduma za afya viko 17. Kwa ongezeko la zahanati sita, kituo cha afya kimoja, hospitali ya wilaya moja, magari ya kubebea wagongwa manne ndani ya miaka minne. Kila anayefanya kazi anastahili kupongezwa. Tunaposimama kumpongeza mama huyu, hatusimami kumsifia, tunampa moyo kwa kazi alizofanya ili aendelee kufanya zaidi na zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo, kulikuwa kuna changamoto nyingi sana. Hivi leo tunavyoongea wakulima wa Jimbo la Katavi wanapata mbolea ya ruzuku. Nikija kwenye kitabu hiki cha Hotuba ya Mheshimiwa Rais, ninaomba ninukuu; ukijikita kwenye sekta ya uzalishaji ukurasa wa 20, Mheshimiwa Rais; hapa ninataka kuweka msisitizo; Mheshimiwa Rais amesema:
“Katika miaka mitano ijayo tunakwenda kufanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta za uzalishaji tukianza na kilimo. Tutaongozwa na dhana ya kilimo ni biashara ni mwekezaji. Lengo letu ni kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta hii kutoka asilimia nne ya sasa hadi kufikia 10% ifikapo 2030. Kwa kufanya hivyo tunalenga si tu kujihakikishia utoshelevu wa chakula bali pia tunawekeza kwenye mnyororo wa thamani ili kuwanufaisha Watanzania wengi walioajiriwa kwenye sekta hii. Tunakusudia kufanya Watanzania wengi kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mazao ya mahindi, mchele na mbogamboga (horticulture) Barani Afrika. Tutafanya hivyo kwa kujielekeza kwenye kilimo cha kisasa kwa kuongeza pembejeo kama mbegu bora, mbolea, viatilifu kwa ruzuku. Tutaongeza upatikanaji wa maji kuhakikisha kuongezeka eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka ekari milioni 3.4 hadi milioni tano”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninataka kusisitiza; kwenye upande wa kilimo cha umwagiliaji, sisi Jimbo la Katavi tuna maeneo mengi yanayofaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji si tu kinakwenda kutuongezea mazao ya chakula na ya biashara, kinakwenda kutoa suluhu ya ajira kwa vijana na kuwazuia vijana wanaotoka vijijini kukimbilia mijini. Serikali ikifanya proper investment kwenye irrigation scheme vijana watavutika kuingia kwenye kilimo cha umwagiliaji na badala yake hawatatoka vijijini kuja mjini. Tunaiomba sana Serikali kufanyia mkazo maneno haya ya Mheshimiwa Rais. Maneno haya yakifanyiwa kazi vizuri, hata wimbi la vijana kwende mjini hawatakuja kuwaona tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea mafanikio ya eneo lolote lile na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, wapo viongozi kwenye maeneo yetu wanafanya kazi vizuri sana. Kwenye eneo langu la Jimbo la Katavi kwa mahsusi ninaomba kuchukua fursa hii kuwapongeza viongozi wafuatao, Alhaj DC Majid Mwangala na Mkurugenzi dada yangu Singlida Mndema. Ninawapongeza hawa makusudi. Haya yote tunayoyaona yamefanyika kwenye eneo letu, wamesimamia vizuri fedha zilizokuja kwenye Jimbo la Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, safari bado ni ndefu; mama huyu anayo dhamira ya dhati ya kuwatumika Watanzania. Tusimame tumsemee, hakuna kiongozi anaweza kusimama akasema mwenyewe, twende tukamsaidie mama huyu kusema yale yaliyofanyika. Ninataka niwaambie, katika kipindi cha hii miaka mitano tunayoianza na kwa hotuba hii tunakwenda kuona matokeo makubwa katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia ninataka pia kuwashukuru sana viongozi wenzangu na ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kumtia moyo. Mama aendelee kufanya kazi, sisi viongozi na Waheshimiwa Wabunge tuko nyuma yake na tutamlinda kwa gharama yoyote ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. THOMAS M. KAMPALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Ninaomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima na afya aliyonijalia na kupata nafasi ya kuja kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza sana Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Leo wakati ninajiandaa kuchangia moja ya mchango wangu ilikuwa ni suala la mafuta. Nimpongeze Mheshimiwa Rais, ametoa ufafanuzi wa changamoto ya mafuta kwa kinagaubaga. Mheshimiwa Rais ametoa historia fupi ya changamoto ya mafuta na akatoa mwelekeo. Ninataka nichukue fursa hii kumpongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza sana Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania home boys ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Madelu Nchemba kwa hotuba nzuri aliyoitoa, hotuba ambayo kwa kweli imegusa kwenye kila idara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. Sisi kwenye Jimbo la Katavi mwaka wa fedha uliokwisha tumepata fedha nyingi sana. Eneo la afya tumepata milioni 928, ukienda upande wa elimu msingi tumepata milioni 674, ukienda upande wa elimu sekondari nako jumla ya fedha zote zilizokuja kwenye Jimbo la Katavi ni 2,688,000,098, fedha hizi ni nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nichukue fursa hii; wakati mwingine tunaposimama hapa kumpongeza Rais wapo watu wengine wanadhani tunafanya mzaha mzaha. Tunampongeza Rais kwa kazi anazozifanya. Sisi kule Jimbo la Katavi, ukifika leo Katavi ukitoka hapa na basi usiku mtu akakushusha kwenye Jimbo la Katavi usiku akakufungua macho akakwambia uko Katavi utashangaa. Imefanyika kazi kubwa na nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kwenye Jimbo la Katavi upande wa elimu tumefanya vizuri sana. Ninataka nichukue fursa hii na kaka yangu Profesa, Waziri wa TAMISEMI yuko hapa; tumefanya kazi kubwa na nzuri ya kujenga shule za msingi na sekondari mpya. Hata hivyo, bado tunayo kazi ya kufanya upande wa elimu. Kazi kubwa tumeifanya ya kujenga shule nzuri mpya na za kisasa, lakini tumesahau; kwamba wakati tunajenga shule mpya huku tunazo shule za zamani ambazo kwa kweli hali yake siyo nzuri. Ni vizuri Wizara ya TAMISEMI ikaja na mpango kabambe wa kwenda kukarabati shule hizi za primary na secondary ambazo ni kongwe ili ziendane na kazi ya shule hizi mpya tunazozijenga, zifanane walau hata kidogo na hizi shule mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende upande wa TARURA, fedha za road funds. Kule kwetu mvua zinanyesha kweli kweli. Kama kuna eneo linapata mvua nyingi na kutosha; na tunamshukuru Mwenyezi Mungu; ni Jimbo la Katavi. Nafuu hii ya kupata mvua nyingi hiyo hiyo imetuletea matatizo makubwa upande wa barabara. Tunaomba fedha za road fund zifike kwa wakati na zisifike kwa kusuasua.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru na ninataka nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati anazindua Bunge hapa alipigiwa makofi mengi sana na Waheshimiwa Wabunge wote baada ya kuongelea suala la TARURA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA wanazo barabara nyingi na zote ni za kiwango cha changarawe. Kwa maana hiyo kinapokuja kipindi hiki cha mvua barabara zote zile zinakuwa ni mbovu na hazipitiki. Hivi tunavyoongea, leo ukienda kwenye Jimbo la Katavi hakuna mawasiliano kati ya Kati za Mapili, Ilela, na Inyonga; hakuna mawasiliano kutoka Uzega kwenda Kijiji cha Mazelizeli. Maeneo mengi kwenye nchi nzima tatizo ni barabara. Tunaomba sana, sana sana kupitia Hotuba hii Serikali ikajipange kuhusu suala la TARURA kuongezewa fedha; hakuna mjadala
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nikwambie, hakuna Mbunge hapa ambaye atasimama ambaye ametoka kijijini akasema barabara zake zina afadhali, barabara zote ni mbaya na zimechoka kweli kweli. Ninataka niwaambie Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wa TAMISEMI, asikae hapa Mzee aka-relax akafikiri huko kuko shwari; kuna hali mbaya, barabara hazipitiki. Wajipange kweli kweli baada ya hizi mvua za masika kukata waende wakarudishe mawasilinao kwenye vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka niongelee suala Mipango Miji. Wakati mwingine ukikaa unajiuliza, hawa watu wa mipango miji; hawa hawa Maafisa Mipango Miji unaweza kufikiri kama wamezaliwa na baba mmoja. Hawa watu matatizo yote ya mafuriko kwenye miji yetu mikubwa ukitazama chanzo chake kikubwa ni mipango miji. Hawa watu wa mipango miji (TAMISEMI) wanasomea vyuo gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, ukitazama mafuriko ya Mkuyuni pale, mimi nimesoma Shule ya Msingi Mkuyuni; wakati tunakua sisi pale Mkuyuni hakukuwa na mafuriko lakini leo, ukienda kutazama pale kwenye Kata ya Mkuyuni kila mwaka mvua zinaponyesha kunakuwa na mafuriko ya kutosha; kwani tatizo ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo watu wa Mipango Miji wamekwenda kutoa vibali vya ujenzi maeneo ambayo wanajua kabisa hapa kuna mto unatoa maji milimani kupeleka Ziwa Victoria. Wao wamekwenda kumpa mtu kibali cha kujenga ghorofa kwenye daraja. Sasa unajiuliza, Mwenyezi Mungu amrehemu kaka yangu Marehemu Didas Massaburi, aliwahi kusema na watu wakamnukuu, hao watu sijui wanafikiri kwa kumtumia Massaburi? Sitaki kuendelea Mwenyezi Mungu amrehemu.
Mheshimiwa Naibu Spika, unajiuliza hawa watu wanafikiri kwa kutumia nini? Hapa kuna daraja, anaona kabisa huu ni mkondo wa maji, hapa anatoa kibali cha kujenga ghorofa. Maji yakija unategemea yapite wapi? Kwa kawaida maji huwa yanatafuta njia yake ya asili. Lazima kama yalipita mwaka huu, yatakuja yatapita hata baada ya miaka 100, lakini unakuta watu wa Mipango Miji wanakwenda kutoa vibali, maeneo ya mito wameweka viwanda, wameweka gereji, matokeo yake maji yanakosa njia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka niende kwa haraka haraka sana kuzungumzia barabara yetu inayotoka Inyonga – Majimoto – Kibaoni – Sumbawanga. Niliwaeleza mwanzo, sisi kule ni wakulima wakubwa kweli kweli. Ili tuweze kufanya biashara vizuri, ni vizuri barabara hii ikatengewa fedha, na kila mwaka barabara hii inawekwa kwenye mpango na fedha kidogo, lakini hakuna ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali, mwaka huu mnapokuja kufanya majumuisho, mtueleze mna mpango gani na Barabara ya Inyonga – Majimoto – Kibaoni. Sitaki kuhangaika na mshahara wa Waziri yeyote, ninawaonea huruma watoto wake. Aje na mpango, atueleze ana mpango gani kuhusu Barabara ya Inyonga – Majimoto – Kibaoni? (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kampala.
MHE. THOMAS M. KAMPALA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache ninaomba niunge mkono hoja. Ahsante. (Makofi)