MHE. SALUM K. SALIM aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka na wa kudumu wa kuzuia tembo kuvamia Vijiji vya Meatu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Salum Khamis Salum, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za haraka katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, hususan tembo, kwenye maeneo mbalimbali nchini, vikiwemo Vijiji vya Wilaya ya Meatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua hizo ni pamoja na kujenga vituo vinne vya askari wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu na kuwawezesha rasilimali watu pamoja na vitendea kazi muhimu. Kupitia vituo hivyo, kati ya mwezi Julai, 2025 hadi Machi, 2026 doria imefanyika na kuwezesha kudhibiti matukio 352 katika Wilaya ya Meatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia na mbinu mpya, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi katika mwaka wa fedha ujao, inatarajia kujenga uzio wa umeme wenye urefu wa kilometa 104 kwenye mpaka wa hifadhi ya Pori la Akiba Maswa kwa upande wa Magharibi unaopakana na makazi ya wananchi katika Wilaya za Meatu, Itilima na Bariadi. Uzio huo utawezesha kudhibiti tembo kutoka nje ya hifadhi. Ahsante sana.