Supplementary Questions from Hon. Hemed Sumry Haidary (4 total)
MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Barabara ya Stalike – Mpanda mpaka Mpanda Ndogo imejengwa mwaka 2012, lakini bado wananchi wa maeneo hayo hawajalipwa fidia. Ninauliza ni lini wananchi hawa ukizingatia muda huo kuanzia 2012 watalipwa fidia yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama afuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema toka mwaka 2012, nitamwomba Mheshimiwa Mbunge tuweze kuonana naye ili kujua changamoto ni nini, kwa sababu 2012 ni muda mrefu. Nimuombe tu Mbunge baada ya hapa tuweze kuona ni wananchi wapi ambao hawajalipwa na wanastahili hayo malipo yake. Ahsante.
MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Manispaa ya Mpanda ni miongoni mwa Manispaa ambazo zilipata mradi wa TACTIC na katika mradi huo tulikuwa na miradi miwili; mradi wa barabara, na mradi wa soko la kisasa pale Kazima. Mradi wa barabara tayari tulishaanza, na mradi wa soko bado haujaanza.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kuiuliza Serikali, ni lini mradi wa soko la kisasa la Kazima utaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, kama alivyotangulia kuuliza, Serikali imefanya kazi kubwa sana kupitia mradi huu wa TACTIC. Kwenye eneo analotoka Mheshimiwa Mbunge, zimejengwa barabara za lami karibu kilomita 13 kwa zaidi ya shilingi bilioni 23.
Mheshimiwa Spika, awamu ya pili itakayofuata itakuwa ni ujenzi wa soko, na tumefanya hivyo kwenye TACTIC awamu ya kwanza, maeneo ambayo tulianza na barabara awamu ya pili tulianza na ujenzi wa soko. Maeneo ambayo tulianza na ujenzi wa masoko awamu ya pili tulianza na ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Ninaomba kumwuliza swali Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, je, ni lini Skimu ya Umwagiliaji ya Kakese ambayo iko kwenye Jimbo la Mpanda Mjini itaanza kujengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Skimu ya Kakese iliyopo katika Jimbo la Mpanda Mjini, tulikuwa tumeshamaliza upembuzi yakinifu na sasa tunakwenda katika hatua ya kuutangaza ili kupata mkandarasi na ianze kujengwa. Kwa hiyo, nimwondoe shaka tu kwamba ninaamini katika mwaka wa fedha unaokuja shughuli hiyo itaanza.
MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Jimbo la Mpanda Mjini, Kituo cha Polisi cha Wilaya kilikuwa katikati ya Mji wa Mpanda na baadaye Jeshi la Polisi wakajenga kituo kipya nje ya mji. Nilitaka kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini sasa pale katikati ya Mji wa Mpanda ambapo ndiyo kuna shughuli nyingi za kiuchumi watatuwekea kituo kidogo ambacho kitaendelea kusaidiana na kile kituo kikubwa ambacho kiko umbali wa kilometa sita mpaka 10 kutoka kwenye baadhi ya kata?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge wa Mpanda Mjini kwa hoja yake ya msingi na muhimu. Kwanza ninadhani tumshukuru kwa kupongeza jitihada za Serikali za ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Jimbo la Mpanda Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuhusu ni lini kituo kidogo kitajengwa kwenye karibu na maeneo ya makazi ya watu ambapo kuna mkusanyiko, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakaa pamoja, tuone namna gani tunaweza kushirikiana na wananchi kwenye eneo hilo, kwa vile ni kituo kidogo cha daraja C ili kusudi tuweze kukijenga kwa haraka zaidi.