Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon Silvery Luboja Salvatory (2 total)

MHE. SILVERY L. SALVATORY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa wananchi wa vijiji 16 vya Gukwa Buhunda, Mwagimagi, Kifune, Busongo, Nyambiti, Kabale, Buhingo, Seke, Songiwe, Mwasagela, Mbalama, Nyamayinza, Gulumungu, Ng’hamve pamoja na Itogwang’holo viko kwenye Mradi wa Maji wa Ihelele unaopeleka maji Mikoa ya Shinyanga na Tabora, na unaanzia kilometa zero kutoka kwenye chanzo cha maji; Tangu uzinduliwe mwezi Juni, 2009 wananchi hawa hawajawahi kupata maji ilhali maji yananyewa Sikonge. Je, sasa Serikali haioni ni wakati umefika wananchi hawa na wao waweze kupewa maji kwa haraka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa maji ni uhai, je, Serikali ina mkakati gani wa dharura wa kuwapatia wananchi hawa maji kwa haraka ili kuokoa afya zao? Ninakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salvatory, Mbunge wa Misungwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kwenye upande wa Misungwi Serikali imefanya kazi kubwa sana. Upatikanaji wa maji wa sasa wa Misungwi ni 68%, lakini Serikali imetekeleza zaidi ya miradi 15 na yenye gharama ya shilingi bilioni 15.6, lakini miradi inayoendelea kwa sasa ni nane yenye gharama ya shilingi bilioni 69. Hii ni kazi kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Jimbo la Misungwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba kazi ya Serikali ni kuhakikisha kwamba vijiji vyote vinapata huduma ya majisafi na salama, lakini kati vijiji 94 vyote tayari vina maji na vijiji vinane ndivyo ambavyo bado tunahakikisha kwamba mradi huu unaoendelea utakapokamilika pamoja na vile vijiji 16 vyote vitapata huduma ya majisafi na salama. Tunafahamu kwamba maji ni uhai, lakini maji ni uchumi. Tunafahamu kwa kuwawezesha wananchi wa Misungwi wataweza kufanya shughuli zao za kiuchumi, lakini pia wataweza kutumia majisafi na salama kwa ajili ya kunywa, ahsante sana.
MHE. SILVERY L. SALVATORY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza ninakubaliana na mpango wa Serikali wa kutengeneza barabara kwa awamu kwa sababu za kibajeti, lakini majibu ya Mheshimiwa Waziri ni tofauti kabisa na hali halisi iliyoko site kwa kuwa Serikali haijasema kweli. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kwenda kujionea hizo 40% za ujenzi wa kilometa tatu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Ninaomba Serikali sasa iwaambie wananchi wa Mwanangwa, Misasi, Buhingo, Busongo, na Nunduru, ni lini barabara yao itaanza kujengwa kiukweli? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mkandarasi alishafanya kazi na ndiyo maana alishaomba hata malipo baada ya kufanya kazi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tulichoandika hapa, niko tayari kwenda na Mheshimiwa Mbunge kuona kile ambacho kimefanyika, lakini huku Serikali ikiwa inaandaa malipo ya huyo mkandarasi ili aweze kuendelea na kazi.

Mheshimiwa Spika, pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni dhamira ya Serikali na ndiyo maana tumeanza kuijenga kwa awamu tukisubiri kupata fedha nyingi ambayo tutakamilisha kuijenga barabara hiyo ya Misungwi mpaka Kahama.

Mheshimiwa Spika, tusingekuwa na dhamira ya dhati tusingeanza, lakini tumeona wakati tunapata fedha kiasi, basi tuendelee kupunguza kazi, lakini tutakapokuwa tumepata fedha yote, mpango wa Serikali ni kujenga barabara yote kutoka Misungwi hadi Kahama kwa kiwango cha lami, ahsante.