MHE. SILVERY L. SALVATORY aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza Mradi wa Maji Bonde la Lujamate –Buhingo ambao umesimama kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Silvery Luboja Salvatory, Mbunge wa Jimbo la Misungwi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Maji wa Ilujamate – Buhingo uliopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza unahusisha ujenzi wa matanki matatu yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 800,000, ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 67, sambamba na ujenzi wa vituo 60 vya kuchotea maji. Utekelezaji wa Mradi huo umefikia wastani wa 40% na unalenga kunufaisha zaidi ya wananchi 84,000 waishio kwenye vijiji 16 vya Wilaya ya Misungwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha miradi hiyo inayotekelezwa kwa kupelekewa fedha kadiri zinavyopatikana katika mwaka huu wa fedha 2025/2026 ili ikamilike na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa ukiwemo Mradi wa Maji Ilujamate – Buhingo.
MHE. SILVERY L. SALVATORY aliuliza:-
Je, lini Serikali itamrejesha mkandarasi wa ujenzi wa Barabara ya Mwanangwa – Misasi – Salawe – Kahama kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Silvery Luboja Salvatory, Mbunge wa Misungwi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mwanangwa – Misasi – Salawe – Kahama yenye urefu wa kilometa 149 unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha kwa kuanza na sehemu ya Mwanangwa hadi Manawa kilometa tatu ambapo utekelezaji wake umefika 40%. Kwa sasa, Serikali inaendelea na taratibu za kupata fedha ili kumlipa mkandarasi madai yake aweze kuendelea na kazi, ahsante.