Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. SILVERY L. SALVATORY: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na kwa kunijalia afya njema kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu asubuhi hii ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niwashukuru wananchi wa Jimbo la Misungwi kwa kuniamini na kunichagua kuwa mwakilishi wao. Ninaomba niwaahidi utumishi uliotuka, na sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kunidhamini kuweza kupeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi kwenye Uchaguzi Mkuu na hatimaye kuwa Mbuge wa Jimbo la Misungwi. Aidha, ninawashukuru wananchi, kila mmoja kwa kadiri alivyohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa ninawashukuru wazazi wangu; Marehemu baba yangu Mzee Salvatory, na Marehemu mama yangu Letisia. Mwenyezi Mungu awape pumziko la milele. Ninaamini kwa imani yangu huko waliko wananiombea, kwani mafundisho ya imani yangu yananiambia mwili pekee ndio unaokufa, lakini roho zipo na wanaona kinachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, kwa vile ni mara yangu ya kwanza kuzungumza, lakini nimekuwemo humu Bungeni tangu Mheshimiwa Rais alipozindua Bunge la Kumi na Tatu Tarehe 14 Novemba. Kwa hiyo, nitapita kwenye nyaraka mbalimbali nikianza na hotuba ya Mheshimiwa Rais, Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2026/2027 na Dira ya Taifa ya 2050 pamoja na hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji waliozungumza huko nyuma walisisitiza kwamba mawasilisho ya Serikali yamenyooka na yametulia na yanajieleza, shida ni utekelezaji. Kwa muda mfupi ambao nimekuwa hapa, nimefanya utafiti mdogo nikatafuta Ma-CEO wanne. Ma-CEO wawili wanapatikana kwenye nyumba hii, ma-CEO wawili wako nje ya jumba hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ma-CEO wawili ninaomba niwapongeze, maana kupitia hizi nyaraka mbalimbali ninaona wanaenda kwa vitendo. Mmojawapo, sisi wote Wabunge ni mashahidi, tukiamka asubuhi tunakutana na message inatuelekeza leo tutaanza na nini na tutamaliza na nini? Ninaomba nipongeze sana taasisi ya Bunge, kwani tangu niingie humu nime-appreciate huduma zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, CEO wa pili, niipongeze Wizara ya Nishati. Siku chache nikiwa hapa Bungeni nilipata taarifa ninambiwa nini kinaendelea kwenye jimbo langu kuhusiana na suala la nishati, ambapo kwenye Jimbo langu la Misungwi nilipewa vitongoji 121 na kufanya tubakiwe na vitongoji 280 pekee kati ya vitongoji 724. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Wabunge wenzangu, kama Watanzania watafanya kazi kwa mifano hiyo miwili niliyoitolea, kuanzia hotuba ya Mheshimiwa Rais, Mpango wa Maendeleo wa Taifa pamoja na hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu vinaweza vikatekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza, ndani ya huo muda nimeenda mahali nikawa ninatafuta huduma. Kutolewa tu barua, na wakijua mimi ni Mbunge na ni mwenzao, imechukua mwezi mmoja, na hiyo taarifa nilimpa Mheshimiwa Prof. Shemdoe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haikuwa nia yangu kuyazungumza hapa. Nikaenda kwa ma-CEO wengine ambao wana chain ambayo inaungana, nikahitaji huduma ambayo ilikuwa inahusu pia nilipe kodi ya Serikali, lakini tunavyoongea leo ni miezi minne utekelezaji wake haupo. Maana yake ni nini? Kama vitu tunavyoviongea humu haviwezi vikatekelezwa kwa vitendo, hatuwezi tukatoboa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nipongeze hotuba zote hizi tatu kama ambavyo nimeziainisha, kwa maana ya kwamba hizi hotuba zinasomana kuanzia hotuba ya Mheshimiwa Rais, na hotuba ya mipango hadi hotuba ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba nijielekeze kwenye hotuba ya Waziri Mkuu. Kwenye ukurasa wa 176 hotuba ya Waziri Mkuu inaelekeza kwamba tunaenda kusambaza maji vijijini kwenye vijiji 225 ambapo shilingi bilioni 449 zinaenda kutumika. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, na kwa maelezo yangu niliyoyatoa kwa namna ambavyo hatuwajibiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninao mradi wa Ilujamate – Buhingo ambao una vijiji 16. Chanzo cha maji kilizinduliwa mwaka 2009 na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne. Leo ni miaka 17 maji hayajafika kwenye vijiji vya jirani ambavyo viko karibu na chanzo, haizidi kilometa tano mpaka 20, ilhali maji yanapatikana kilometa 600 kutoka kwenye chanzo. Hiyo siyo haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mmoja wetu aliyepewa dhamana kwa nafasi yake aweze kutekeleza wajibu wake, kwani mwenye macho haambiwi tazama, lakini pia mwenye akili hawezi kuambiwa jiongoze. Hapo kuna dosari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba kupitia hotuba ya Waziri Mkuu, tunao mradi wa maji wa Ukiliguru unaopita kwenye vijiji 19 vya Bulemeji, Ngudama, Nyang'holongo, Nyamle, Usagara, Idetemya, Nyangomango, Ntende, Koromije, Ibondo ya A na B Mamaye hadi Bugomba. Vijiji hivi viko connected na chanzo cha maji, hakihitaji hata usumbufu wa aina yoyote. Kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba miradi hii sisi Wana-Misungwi ikaweze kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti ...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa Silvery Salvatory, kengele ya pili imeshalia.
MHE. SILVERY L. SALVATORY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba dakika moja. Tunayo miradi ya kimkakati ambayo imetajwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kutokana na jiografia ya Mwanza, tunaomba basi upanuzi wa barabara ya njia nne kutoka Usagara kwenda Mjini ukaweze kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia barabara inayotoka Kaluluma kupitia Mwasonge hadi Buhongwa yenye urefu kilometa 6.6 nayo ijengwe kwa kiwango cha lami, bila kusahau njia inayotoka kwenye Dry Port, Fella inayopita Ngeleka - Fella hadi Nyashishi nayo ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. SILVERY L. SALVATORY: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba niunge mkono hoja. (Makofi)