MHE. MOSES C. BUJAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria kuja Mji Mdogo wa Malya umesimama. Swali langu ni kutaka kujua, ni lini mkandarasi atalipwa fedha ili arudi kazini na kukamilisha mradi huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Moses Charles Bujaga, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa mradi ule unaopita Hungumalwa – Malya kwenda kule Sumve, na pia mradi huu unaenda mpaka kwa Mheshimiwa Mashimba Ndaki. Mheshimiwa Mbunge tulishakaa pamoja na mkandarasi kwa pamoja tukakubaliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninaomba sasa nimhakikishie kwamba ule mpango wa kuhakikisha kwamba analipwa, tumeweka kipaumbele katika kipindi hiki cha miezi miwili ili mkandarasi aweze kulipwa na arudi site, kwa sababu tunajua kuna matanki ambayo tayari ameshayajenga, lakini kuna kilometa kadhaa za kulaza mabomba ili aweze kumalizia na kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo hayo wanaweza kunufaika na huduma ya majisafi na salama. Ninakushukuru sana.
MHE. MOSES C. BUJAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, ningependa kuongeza maswali madogo mawili. Kituo cha Afya Budushi kina daktari mmoja, Kituo cha Afya Kadashi kina daktari mmoja, na Kituo cha Afya Isunga hakuna daktari. Ningependa kujua Serikali ina mpango gani wa dharura kuhakikisha kwamba tunapata watalamu katika vituo hivi vitatu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kituo cha Afya Budushi hakina gari la kubeba wagonjwa inapotokea dharura ya kupeleka wagonjwa hao kwenye Hospitali ya Wilaya iliyoko kilometa 33. Je, Serikali itatupatia lini gari la kubeba wagonjwa Kituo cha Afya Budushi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza maswali mawili ya nyongeza na ninaomba niyajibu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu upungufu wa madaktari na ndiyo maana tulipata vibali vya kuajiri madaktari 5,000 nchi nzima na baadhi ya madaktari wameshafika maeneo yao ya kazi. Ninawaomba madaktari waliopangiwa kwenda kwenye vituo vyetu vya afya ili wafike kwa wakati, lakini kama haitoshi nimwelekeze Mkurugenzi kuendelea kutoa ajira zile za lazima hasa kwenye maeneo ambayo tuna upungufu kama alivyoainisha Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu magari ya kubebea wagonjwa, tayari tulishapeleka magari zaidi ya 594 katika maeneo yetu kwa Halmashauri zote nchini, lakini pia tunaendelea kuomba magari. Kadiri tunavyoyapokea kutoka Wizara ya Afya, tutaendelea kuyaelekeza katika vituo vyetu vya afya. (Makofi)