MHE. LUCY E. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Ni utaratibu gani unaotumika kwa kutumia mkongo wa Taifa katika kupeleka mawasiliano kule Zanzibar ili kufikisha huduma kwa wateja kwa haraka sana na kwa maeneo ambayo hayafikiki?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu unaotumika katika kupeleka mawasiliano Zanzibar kupitia mkongo wa Taifa, huwa kwanza inafanyika tathmini, kuangalia uhitaji wa maeneo husika, ikishafanyika, Shirika la Mawasiliano Nchini hupeleka mawasiliano hayo kulingana na uhitaji wa eneo husika.
MHE. LUCY E. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Tanzania imepata bahati mwaka 2027 kuendesha michezo ya AFCON katika upande wa Bara na Zanzibar, ninataka kujua, kwenye upande wa utalii, wafanyabiashara ndogo ndogo na wajasiriamali nao ni sehemu ya fursa ambayo wameipata kwa ugeni utakaoingia. Je, ni elimu gani imetolewa mpaka sasa, au Serikali imejipanga vipi kutoa elimu kwa wafanyabiashara ndogo ndogo pamoja na wajasiriamali, hususan wanawake?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, imejipanga vya kutosha kupokea mashindano hayo ya AFCON. Hivi ninavyokwambia, wataalamu wetu wako site, wameshaanza mafunzo na taratibu mbalimbali za wajasiriamali wetu ili kusudi waweze kupokea vizuri, na wanapokuja watu kutoka nje kwa ajili ya michezo, wasiwe wameondoka tu na michezo, bali waende kwenye vivutio vyetu na wajasiriamali wetu nao wawe wanufaika kupitia mashindano hayo ya AFCON.