Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Lucy Edward Mwakyembe (2 total)

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. LUCY E. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi jioni hii kuweza kuongea ndani ya Bunge hili Tukufu kwa mara yangu ya kwanza nikisimama hapa kama Mbunge wa Viti Maalum kupitia kundi la wafanyakazi kutokea Mkoa wa Mjini Unguja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda sana kuwashukuru Wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa wa UWT ukiongoza na Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wa Taifa UWT, Mama Mary Pius Chatanda. Wajumbe hawa walisababisha mimi kuonekana na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi kwa kuniteua na kuniamini kuona ninaweza kuungana na Wabunge kupitia Bunge hili la Kumi na Tatu ili niweze kuwawakilisha wanawake wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda sana pia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushindi wake wa kishindo wa 97% kupitia Chama Cha Mapinduzi. Pia ninapenda kumpongeza Spika ambaye yuko ndani ya Bunge hili pamoja nawe Naibu Spika pamoja na Wenyeviti, Waheshimiwa Wabunge wote waliomo ndani ya Bunge hili kwa ushindi wa kishindo mlioupata na kuhakikisha mmeteuliwa kuwa Wabunge wa Bunge la Kumi na Tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kumpongeza Dkt. Emmanuel Nchimbi, Msaidizi wa Mama Samia Suluhu Hassan, Msaidizi wa Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri Mkuu ambaye aliteuliwa na kuchaguliwa kwa kishindo kuwa Mtendaji Mkuu wa Serikali. Ninawapongeza pia Mawaziri na Waheshimiwa Manaibu Waziri wote ambao wanamsaidia Rais katika kufanya kazi zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwa upekee kabisa, ninapenda kuwapongeza sana Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, ambaye aliwasilisha Mpango Elekezi wa Maendeleo wa muda mrefu, muda wa kati na Mpango pia wa mwaka 2026/2027. Pia, ninapenda kumpongeza kaka yangu Khamis Mussa, Waziri wa Fedha naye aliwasilisha Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027 – 2028/2029. Ninapenda sana kupongeza kwa weledi waliotumia katika kuwasilisha mpango huu pamoja na bajeti hiyo ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uwasilishaji wa mwongozo huo pamoja na bajeti hiyo, ninaomba kujielekeza katika maeneo mawili. Eneo la kwanza ni sekta ya utalii ambapo kwenye sekta ya utalii tumeona imeendelea kuwa nguzo muhimu kwa uchumi wa Taifa na kuchangia 27% ya pato la Taifa kwa mwaka 2024. Mafanikio makubwa hayo, yametokana na ongezeko kubwa la idadi ya watalii kutoka watalii milioni 1.8 mwaka 2023 na kufikia milioni 2.14 kwa mwaka 2024. Mapato pia kuongezeka kutoka dola za Kimarekani bilioni 3.37 kwa mwaka 2023 na hadi kufikia bilioni 3.9 kwa mwaka 2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonesha sekta ya utalii ina nafasi kubwa ya kuendeleza uchumi wa Taifa kufikia malengo ya muda mrefu. Kamati pia ya Bajeti imechambua shabaha mbalimbali na ikapendekeza Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara na viwanja vidogo vya ndege katika maeneo yenye vivutio vya utalii na kurahisisha usafiri wa watalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapenda kumpongeza sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa makusudi kabisa na kwa uthubutu wake mkubwa, aliamua kutengeneza filamu ya “The Royal Tour” katika kuongeza, kuinua uchumi wa Nchi hii ya Tanzania kutokana na sekta hiyo ya utalii. Pia ninaomba kumpongeza Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi ambaye alikuwa bega kwa bega katika kumtia moyo na kumwongezea nguvu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutengeneza filamu hii ya ‘The Royal Tour’.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona viongozi hawa waliitengeneza filamu hii, Dkt. Samia aliitengeneza filamu hii akiwa ardhini, akiwa angani, akiwa baharini kwa kushirikiana na Dkt. Hussein Mwinyi ambapo nilifurahi sana nilipowaona wakiwa baharini, walifikia hatua ya kuvutia kivutio hiki cha utalii kwa kuvua samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemwona daktari huyu uthubutu wake ulivyo mkubwa, walimtoa samaki kwenye maji wakamleta juu; ni Rais wa pekee ambaye alifanya tukio hilo, mimi sijawahi kuona. Tumpongeze sana Daktari Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kusema nini katika eneo hili? Katika eneo hili ninaendelea kusisitiza kwamba, Serikali ihakikishe utekelezaji wa mikakati wa kukuza na kuhamasisha aina mbalimbali za utalii ikiwemo utalii wa picha, michezo, matibabu, mikutano, fukwe za bahari, utamaduni na urithi wa kihistoria ambao haujatumika ipasavyo. Vilevile, jumuishi za hifadhi na wanyamapori ziendelee kuimarishwa ili kuongeza thamani ya vivutio vya utalii. Hatua hizi zitasaidia kuongeza idadi ya watalii, mapato ya kigeni na mchango wa sekta ya utalii katika maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ninalotaka kuligusa ni la wakandarasi wazabuni pamoja na watoa huduma. Tumeona katika uwasilishwaji wa mpango huu umeguswa uimarishaji wa mifumo ya kidigitali. Sasa hapa katika uwasilishwaji nimeona changamoto moja kubwa inayoikabili Serikali; ni malimbikizo ya madeni ya wakandarasi; wazabuni na watoa huduma. Changamoto hizi zinatokana na mambo kadhaa ikiwemo ucheleweshaji na uhakiki wa madai, ukosefu wa fedha za kutokana na mapato ya ndani yasiyo thabiti pamoja na urasimu katika utaratibu wa malipo. Hali hii imekuwa ikidhoofisha uwezo wa wakandarasi na wazabuni kuendelea kutoa huduma bora na wakati mwingine kusababisha kusimama kwa miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa sikusimama tu kwa miradi ya maendeleo; tumeona vijana wetu wengi wamekuwa wakipata ajira kwenye eneo hili. Wazabuni na wakandarasi wanapofanya kazi basi wao wanakuwa msaada mkubwa wa kutoa ajira kuisaidia pia Serikali kuwapa vijana wetu ajira. Pale tunapokosa kuwalipa kwa wakati; kumbuka wanajaribu kulipa, wanalipa, lakini mwisho wa siku na wao wanashindwa kuwafanyia malipo vijana. Vijana wanalalamika huko mitaani. Wanapolalamika mitaani inasababisha kuonekana kuwa tatizo kubwa ni kiongozi wa juu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. LUCY E. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninaomba kwenye upande huu kwanza mifumo ya uhakiki wa madai iimarishwe katika teknolojia ya kidigitali ili kupunguza urasimu na kuongeza uwazi; Serikali ihakikishe kuwa bajeti ya miradi zinatengwa kwa uhalisia na fedha za kutosha zinapatikana kabla ya utekelezaji wa miradi hiyo; kuwe na utaratibu wa kipaumbele katika malipo ambapo wakandarasi na watoa huduma wanahusika na miradi ya mkakati ya kijamii watalipwa kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. LUCY E. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nami kwa kunipa nafasi ya kuongea tena katika Bunge lako hili Tukufu kwa ajili ya kuchangia hoja ambayo imewasilishwa na Waziri Mkuu ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2026/2027.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa upekee ninapenda nimpongeze Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutunukiwa shahada ya heshima ya udaktari ambayo imetoka katika Jimbo la Chuo Kikuu Nasarawa Nchini Nigeria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake thabiti; ambapo aliweza kuahidi kabla ya kuingia madarakani; kwamba atakapoingia madarakani ndani ya siku 100 ataweza kuyatekeleza mambo mengi. Mambo hayo ni pamoja na elimu, afya, mambo ya maji, na miundombinu. Pia tumeona kuwa hata kwa upande wa bima ya afya ameweza kuwafikia wananchi zaidi ya milioni moja na laki nne pamoja na kaya laki mbili na sabini na sita elfu na nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende pia kumpongeza Mheshimiwa Rais ameweza kutoa ajira za walimu 7,000 na ajira 5,000 kupitia upande wa afya. Ameweza kuhakikisha kuwa analeta fursa ya vijana kwa kuanzisha Wizara ya Vijana na kuwamwagia mabilioni ya shilingi. Bilioni 200 ameziweka kwa ajili ya vijana ili kuweza kuongeza uchumi katika maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye anamsaidia Mheshimiwa Rais katika kutekeleza majukumu yake. Tunaona kuwa amezindua mpango wa kitaifa wa pamoja kati ya waajiri, vyuo vya ufundi stadi pamoja na vyuo vikuu kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa tisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpongeza Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye ni Waziri Mkuu pamoja na watendaji wote wanaomsaidia kazi, bila kumsahau Profesa Shemdoe ambaye yupo katika Wizara ya TAMISEMI, nami nikiwa mjumbe wa Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie upande wa ajira kwa vijana. Tumeona lengo la Serikali kutaka kukuza ajira kwa vijana na wanafanya kazi kupitia ajira zilizo rasmi na zisizo rasmi, ajira za Serikali na za sekta binafsi. Kwenye upande huu ninaomba Serikali pamoja na sekta binafsi pale zinapotangaza fursa za ajira basi ninaomba kwanza tuangalie vijana wa kizalendo ambao wanajitoa kutumikia sekta hizo, sekta binafsi na sekta za Serikali bila kulipwa posho zozote, wameamua kwa uzalendo wao kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inapotokea ajira kupitia sehemu hii, ninaomba sana nishauri Serikali waangalie vijana hawa, itafute namna ya kuwaingiza kwenye ajira. Idara ambazo wanazitumikia vijana hawa ni idara hizo hizo zinazoletwa katika kuhitaji wafanyakazi. Ni idara zile zile wanazozifanyia kazi lakini kitendo kinachokuja kujitokeza wakati kazi zinapotangazwa wanakuwa hawafai katika idara zile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana Serikali iwasaidie vijana hawa wa Kitanzania ambao ni wazalendo katika kuwaingiza sehemu hizo za ajira. Pia, ninapenda kuipongeza zaidi Serikali; inaendelea kuzitoa fursa za ajira kwa vijana kwa asilimia nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nigusie kwenye 10% zinazokusanywa kwenye halmashauri kupeleka kwa vijana, watu wenye ulemavu pamoja na wanawake. Hapa mimi nitagusia kwa upande wa wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona halmashauri nyingi zinajitahidi kutoa mikopo kwa ajili ya wanawake. Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amehakikisha maisha ya wanawake yanakuwa mazuri. Mama amewatua wanawake ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuwatua ndoo kichwani wanawake, Mama ameamua kuleta tabasamu kwenye familia, lakini kwa upande huu wa mikopo ambao halmashauri inatakiwa itoe kwa ajili ya wanawake, mikopo hii haiwafikii wanawake, tabasamu lile linaishia njiani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lile tabasamu ambalo Mama anataka kulipeleka kwa ajili ya Watanzania hawa linaishia njiani. Maisha ya familia yanakuwa ya kujikokota na tunajua mama ni nguzo muhimu naye kwa Taifa la sasa kwenye familia. Kwa hiyo, tunaomba Maafisa Maendeleo ya Jamii, wamebaki kukaa ofisini, hawawafuati wanawake, wakawapa elimu jinsi ya kuomba mikopo, jinsi ya kufanya biashara kutokana na hiyo mikopo, jinsi ya kutumia hizo pesa kwenda kwenye biashara ili ikuze biashara zao na jinsi ya kurudisha mikopo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sana Serikali na ninatoa ushauri, Maafisa Maendeleo ya Jamii, washuke, wasimame kutoka ofisini, wasibaki ndani ya ofisi. Kazi ya sasa ya Mheshimiwa Dkt. Samia anataka watu kuwafikia wananchi. Tumemwona Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, amefika ndani ya mikoa na wilaya kuwasikiliza wananchi, kusikiliza kero za wananchi na Maafisa wa Maendeleo ya jamii, wanatakiwa wafike kwa wananchi, kwa wanawake hawa wa Kitanzania ili kuhakikisha wanawafikishia mikopo hii ambayo inatolewa na Serikali, lakini bila ya kuwasahau vijana na watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanatakiwa wakatoe elimu kule, wamejifungia na hapa ninaona ule utaratibu wa upimaji malengo ambayo ni PEPMIS inawahusu wafanyakazi ambao ni Maafisa wa Maendeleo ya Jamii, ambao wengine hawatoki katika idara zao kuwafuata wanawake. Tunaomba, tunaomba sana, wanawake hawa wafikishiwe tabasamu ambalo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewaahidi wanawake wa Kitanzania kuwafikishia ndani ya mwaka wa fedha 2026/2027. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nigusie kwenye madeni ya watumishi. Ninajua sasa hivi Serikali inapitia changamoto kubwa, lakini kuna madeni ya watumishi ambayo yapo yanaonekana. Hapa niwapongeze sana baadhi ya halmashauri, wamehakikisha wanafuta madeni ya watumishi pamoja na madeni ya wazabuni. Wamepunguza madeni kwa asilimia kubwa sana madeni haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana na lengo la Serikali ninajua kwenye bajeti yake hii imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kupunguza madeni hayo. Mimi niiombe tena Serikali wasaidie mzigo ule kwa halmashauri kupunguza madeni yale, hususan madeni yasiyokuwa ya mishahara, yafutwe na ikiwezekana yasizalishwe tena au yazalishwe kwa uchache, kwa sababu, madeni yanafutwa, lakini yanaendelea kuzalishwa. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, yanazalishwa vipi? Katika kipindi ambacho watumishi wamepewa ajira ile hamahama ya watumishi, amefikishwa wilaya nyingine anataka kuhama kurudi wilaya nyingine; hii nayo inazalisha madeni ya watumishi. Kwa hiyo, ninaomba hapa kwa kuishauri Serikali iongeze nguvu ya kulipa madeni ya watumishi, lakini iongeze nguvu ya kulipa madeni ya wazabuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa muda huu, nami ninaunga mkono hoja. (Makofi)