MHE. BARAKA A. U. MWAMENGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona na kunipa nafasi hii. Ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi cha Kasumulu kilichopo border ya Kasumulu ndani ya Jimbo la Kyela kwa kuwa kiliathirika na vurugu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge wa Kyela na nimpongeza vilevile kwa kuona umuhimu, na ninadhani kwa sababu ya ufafanuzi wangu wa hoja ya msingi ya kwa nini tunajenga vituo vya Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye swali la msingi tulilojibu la Jeshi la Polisi kwa mara ya kwanza Bungeni, tulikuja na mpango wa dharura wa maeneo ambayo yana uhitaji wa kujenga vituo vya Polisi na tuliainisha wastani wa maeneo 698 nchi nzima. Hayo ndiyo maeneo ya dharura kujenga vituo vya Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo hayo 698 ambazo ni karibu kata zaidi ya 600 zilikuwa hazina kabisa vituo vya Polisi na kata 77 zilikuwa zimeanza ujenzi kwa maboma, lakini hawajakamilisha. Nataka kumwambia tu Mheshimiwa kwamba tunaona umuhimu wa kujenga kituo cha Polisi eneo hilo, lakini lini? Mpango ule tumeugawa katika awamu tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza tutakuwa na vituo 196, awamu ya pili tutakuwa na vituo 212 na awamu ya tatu tutakuwa na vituo 211. Kwa hiyo, kukamilika kwa Mpango huu, basi na eneo lake litakuwa tayari limeingia kwenye ujenzi.
MHE. BARAKA A. U. MWAMENGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza, na ninashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande hiki cha Barabara cha kutoka Ibanda kwenda Itungi Port kwa sasa kimeharibika sana na hasa section ya kutoka Kyela Mjini mpaka Itungi Port na Wananchi wa Kajunjumele wanapata shida sana. Je, Waziri atakuwa tayari kufika Kyela kutembelea hicho kipande ili kuweza kujionea hali iliyopo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, niishukuru Serikali kwa jinsi ilivyotoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Border Post pale Kasumulu kwenye mpaka wetu na Malawi. Ninaishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia. Je, Serikali itakuwa tayari kutoa fedha za kujenga barabara inayounganisha ile Border Post ya Kasumulu ili kuonesha nia njema ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia ametoa fedha kwa ajili ya kile kituo cha border ya pamoja ikiwemo barabara za kuingia stendi na taa za kufanana na kile kituo kilichojengwa, kile cha border ya Kasumulu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ikishakuwa na mkandarasi, mara nyingi mkandarasi ndiye anahusika, kwa hiyo, nina uhakika kwa kuwa alisimamishwa, kutakuwa kuna mahitaji makubwa yanahitajika ya kutengenezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba tu kutumia Bunge hili Tukufu kumwelekeza Meneja wa Mkoa wa Mbeya ambapo nilisikia wanamsifia sana, na kweli ni mchapakazi mzuri, aweze kuwasiliana na TANROADS Makao Makuu, kwa kuwa mkandarasi hayupo, basi aweze kupata fedha ya dharura ya kuitengeneza barabara hiyo iweze walau kupitika na kuondoa hiyo adha kwa sababu mkandarasi hayupo kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kufanya matengenezo ama ujenzi wa barabara ya kwenda stendi na kuweka taa kwenye ile eneo la OSBP ili kupata sura nzuri ya nchi; ninajua hiyo ndiyo sehemu ambayo wananchi wetu wanapokwenda Malawi, ndiyo njia ya kutokea, na pia wananchi wa kutoka Malawi ndipo wanapoingilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwelekeze Meneja wa Mkoa wa Mbeya aweze kuangalia hizi barabara, afanye tathmini na kuleta mahitaji. Nina uhakika atashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kuona nini wangetamani kifanyike katika ile OSBP ambayo ndiyo mpaka wa kwenda Malawi, waangalie namna ya kuboresha halafu walete tathmini tuweze kutafuta fedha, na kufanya watu wanapoingia katika nchi yetu kuwe na sura ambayo wanasema sasa wanatoka Malawi, wanaingia Tanzania.