Answers to supplementary Questions by Hon. Kaspar Kaspar Mmuya (5 total)
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Hata hivyo, nimweleze kwamba kuna changamoto kubwa katika eneo la Bwakila Chini, kwa maana ya Kijiji cha Ngwade, Serikali imepima maeneo kwa ajili ya kuwamilikisha wananchi na wananchi wamelipa fedha zote, lakini hadi sasa hawajapatiwa hati zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika Kijiji cha Msonge pia wananchi walijiunga katika kikundi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo, wakawa na makubaliano na Serikali ya kujenga zahanati katika eneo husika, wananchi hawa waliahidiwa kupimiwa viwanja na Wizara ya Ardhi na kumilikishwa na tayari wamefanya wajibu wao kwa kujenga jengo lile, lakini hadi sasa Serikali haijatimiza wajibu wake wa kuwapimia na kuwapatia hati ili waendeleze shughuli za kilimo katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari sasa kuambatana nami jimboni kuwasikiliza wananchi na kujionea changamoto hizi ili aweze kuzitolea majibu? Ninafahamu Mheshimiwa Naibu Waziri kwa muda mchache aliohudumu katika ofisi yake ni bingwa wa utatuzi wa migogoro ya ardhi, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza Morogoro Kusini kwa kweli wamechagua Mbunge ambaye anafuatilia changamoto mbalimbali za wananchi wake. Wakati ni mgeni kabisa katika nafasi hii alishawahi kunipigia na tuliwahi kuzungumza juu ya changamoto mbalimbali na hatma yake na leo hii ameleta jambo hili na anazidi kuwatetea kujua haki ambazo wanastahili katika maeneo hayo, hongera sana Mbunge na hongereni wananchi wa Morogoro Kusini kwa kupata mwakilishi mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji alivyovitaja na alivyozungumza kuhusu haki yao ya kupatiwa hati, huo ni wajibu wa Wizara kwa sababu tayari mpango ulishapangwa na upimaji umeshafanyika, ni suala la kutoa hati tu. Nikuahidi, nitaambatana na wewe katika ziara ambayo tutakubaliana, tutaenda maeneo husika na siku hiyo nikuhakikishie kama kutakuwa na hati ambazo wanastahili kupewa watu hao katika vijiji hivyo tutazitoa na wewe ukiwemo na wananchi wako wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na sheria, sera, kanuni na taratibu ambazo amezieleza hapo Mheshimiwa Naibu Waziri, maeneo ya wazi na yale yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za michezo bado yanavamiwa, na bado yanabadilishwa matumizi. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ni hatua gani ambazo Serikali inachukua kwa yale maeneo yote ambayo yamevamiwa na yale ambayo yamebadilishwa matumizi mpaka tunavyozungumza sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa baadhi ya maeneo ya wazi hasa maeneo yanayoenda kwenye masoko yaliyo karibu na shughuli za watu yamevamiwa na yamejengwa holela kiasi cha kuzuia hata magari ya zimamoto kwenda kuzima moto inapotokea dharura, na maeneo mengine ya michezo yamevamiwa na shughuli za michezo haziendelei katika maeneo hayo. Je, Serikali kwa nini pamoja na sheria nzuri ambazo amezitaja Mheshimiwa Naibu Waziri, wameshindwa kuzisimamia ili Bunge liweze kuchukua hatua na kuweza kusaidia jambo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninamshukuru sana kwa kuwa ameonyesha kuelewa matumizi ya maeneo haya yaliyotengwa ambayo tunaweza kusema kwa ujumla yake ni maeneo ya wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ninaomba niseme maeneo yote ambayo kisheria yametengwa kwa matumizi maalum, au maeneo ya wazi, yatabaki hivyo kwa kutumia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yeyote aliyeweza kumilikishwa maeneo hayo ya wazi bila kufuata utaratibu uliowekwa, utaratibu na sheria zinazungumza, haijalishi kuwa una hati sasa hivi, lakini Wizara ya Ardhi kupitia Kamishna wa Ardhi ana uwezo wa kufuta hati hiyo endapo itathibitika kuwa utaratibu wa kumiliki eneo hilo haukufuatwa kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwaagiza kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Wakurugenzi ambao ndio wenye dhamana ya kusimamia maeneo hayo kote nchini kuhakikisha maeneo hayo yanalindwa, na malalamiko yote yanayotolewa mtu kumilikishwa eneo la wazi, kuhakikisha yanashughulikiwa kwa kuangalia taratibu kama zilifuatwa. Ikithibitika kama hazikufuatwa, basi Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Mkoa ana dhamana ya kufuta hati ya umiliki wa eneo hilo ili libaki wazi kama ilivyotarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Husna. Kwanza Serikali haijashindwa. Licha ya jibu langu la msingi nililolitoa kwenye swali la msingi kuhusu uwepo wa sheria, sera, kanuni na miongozo, lakini pia licha ya uwepo wa mfumo wa usimamizi na utekelezaji wa sheria hizi, uwepo wa Wizara na watumishi katika ngazi ya Wizara na pia ugatuaji uliofanyika wa uwepo wa watumishi mpaka ngazi ya halmashauri, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imenuia kusimamia suala hili kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilijulishe Bunge lako Tukufu kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imenuia kwamba ardhi yote ya Tanzania yenye kilometa za mraba 948,740 yote itapimwa. Ardhi hii ina vijiji 12,333. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo, na Mheshimiwa Waziri wetu anasimamia. Hivi ninavyoongea, mpaka sasa hivi tumepima vijiji 4,873 Tanzania nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tu, amewezesha kupima vijiji 2,697 sawa na 55% ya vijiji 4,873 vilivyopimwa tokea uhuru. Hii ni dhamira ya dhati ya kufanya vijiji vyote vilivyobakia 7,460 viwe vimepimwa ndani ya awamu hii ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti huo ndio mkakati wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Upimaji wa vijiji hivi maana yake itaainisha maeneo haya ya wazi, yatajulikana na tutashirikisha mifumo yote ikiwemo mamlaka za upangaji ili kubainisha maeneo hayo na yalindwe kama nilivyoeleza kwenye rai niliyoitoa kwenye jibu letu la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. MARYAM USSI YAHYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali la nyongeza. Pamoja na kwamba kuna uvamizi wa ardhi, lakini bado tuna migogoro mingi ya ardhi hapa nchini. Je, Serikali sasa haioni ni muda muafaka wa kuanzisha mfumo maalum kama vile ilivyo Samia Legal Aid, sasa uanzishwe mfumo maalum wa kusikiliza changamoto ya migogoro ya ardhi ili kuweza kutatulika kwa haraka?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Mariam kwa swali zuri na nia yake njema ya kuwafanya wananchi wetu waishi bila migogoro kwenye maeneo yao wanayoishi na kufanya shughuli za kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwapongeze sana Mamlaka ya Serikari za Mitaa hususan Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya mpaka Wakurugenzi waliopo katika halmashauri zetu, wamejiwekea utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi, na kila wiki wamepanga siku moja au siku mbili mahususi kusikiliza na kupokea kero za ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu nitoe rai yangu kwa Watanzania wote kwanza, nimesema Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa sababu tunao Maasifa wa Ardhi waliomo kwenye maeneo hayo ambao nao ni sehemu ya timu ambayo Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa wanatumia katika kusikiliza changamoto hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Wizara ya Ardhi imejitanabahisha kabisa, tutaweza kutatua changamoto hizi kwa mfumo niliyoeleza, huu wa kusema vijiji vyote vipimwe. Licha ya hivyo, tuna utaratibu wa kuwa na kliniki maalum ya kusikiliza zile kero ambazo zimeshindikana katika ngazi ya wilaya au ngazi ya mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi wenyewe ni mashahidi, tumetoka juzi tu hapa kufanya kliniki ya wiki moja Tanzania nzima, hii ambayo tuliita jina kubwa kabisa, Samia Ardhi Kliniki, tuliweza kusikiliza wananchi wengi na tuliweza kutatua changamoto nyingi na tukawapatia wengine hati za umiliki wa maeneo ambayo wameomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wabunge wakiwa sehemu ya wananchi ambao wanawatumikia, tuungane na Serikali hususan Wizara yetu ya Ardhi kuweza kuwasikiliza wananchi katika mikutano yetu tunayokwenda kuongea nao na kutatua matatizo. Kwa kuwa matatizo mengine ni ya kiutawala, lakini yale mengine sisi kama Wizara ya Ardhi, tuko tayari kusaidiana kwenye mikutano au ziara ambazo tutaziweka.
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Wapo baadhi ya wawekezaji wamehodhi maeneo makubwa ya ardhi na wameshindwa kuyaendeleza kwa 100%, na wengine kubadilisha matumizi. Nini kauli ya Serikali katika kufanya tathmini na kurejesha maeneo hayo ili kupangiwa matumizi mengine Serikalini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mfumo ndani ya Serikali wa kuwezesha wawekezaji hawa wapatiwe ardhi, na ardhi yao ilindwe ili waweze kufanya shughuli ambazo wameombea. Tunashirikiana vizuri na hawa TISEZA na mamlaka nyingine kwa ajili ya kuwapatia ardhi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba na ninatoa tu angalizo kuwa maeneo haya yalitolewa kisheria na wanatakiwa wayatumie kulingana na walivyoomba. Ila Wizara ya Ardhi ina utaratibu wa kufanya ufuatiliaji wa kutekeleza matumizi ya ardhi waliyoomba kutokana na hati ambayo tumepewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi pale tunapogundua mwekezaji ameshindwa kutimiza masharti ya upatikanaji wa ardhi hiyo na kuyaendeleza, huwa tunampata taarifa na kufuata utaratibu wa kuyachukua na kuweza kuwakabidhi watu wengine ambao wana mahitaji ya ardhi. Hivyo, Mheshimiwa Sara, kama ana mwekezaji ambaye ameshindwa, hivyo, tuwasiliane na Wizara ya ardhi ili tuweze kufuata utaratibu tuweza kuyachukua maeneo hayo.
MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Tunalo suala la double allocation, na hili limeleta migogoro mingi kwa wananchi. Serikali imejipangaje ku-solve tatizo la double allocation?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yote ambayo yamepatikana pasipo kufuata utaratibu wa kisheria, mamlaka zinaturuhusu kusikiliza changamoto hiyo na kumfutia yule ambaye amepata ardhi hiyo bila kufuata utaratibu, na yule ambaye amethibitika kuwa ni mali yake anapewa. Kwa hiyo, tunamfutia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama kuna makosa yametendeka, huwa tunaongea kwa utaratibu wa kiutawala na kufanya umilikishaji wa maeneo mengine, lakini la msingi ni kufuta umiliki wa yule ambaye amepata pasipo utaratibu.