MHE. ZUBERI Y. MFAUME aliuliza:-
Je, lini Serikali itaingilia kati na kudhibiti migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wawekezaji wa Morogoro Sugar?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwa ruhusa yako, kwa sababu leo ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa, ninaomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na pia kwa moyo wangu wa dhati niwashukuru wapiga kura wetu au wapiga kura wangu wa Jimbo la Ruangwa waliofanya maajabu ya kupiga kura nyingi kwa Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamemchagua Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kura nyingi, lakini Mbunge wao kwa kura nyingi na wameweka historia kwa mara ya kwanza wamekichagua Chama Cha Mapinduzi kwa Madiwani wote wa Chama Cha Mapinduzi. Ninawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeniwezesha niwe sehemu ya Serikali yake kumsaidia katika nafasi ya Naibu Waziri, ninamshukuru sana. Vinginevyo, ninaendelea kuwapongeza Wabunge wote kwa kuteuliwa na kuchapa kazi ambazo leo hii Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ninaomba sasa nijibu swali namba 32 la Mheshimiwa Zuberi Yahya Mfaume, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Morogoro Sugar inamiliki eneo lenye mashamba tisa katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro yaliyopo Vijiji vya Gomero, Nyarutanga, Dakawa, Bwakila Chini, Mngazi, Vigolegole, Msonge, Tanunguo na Tulo yenye ukubwa wa jumla ya hekta 3,632.25. Eneo hilo limepangiwa matumizi ya kilimo cha miwa kwa ajili wa kiwanda cha kuzalisha sukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba hayo yametolewa kwa TISEZA kwa hati zilizosajiliwa kwa Namba 7312, 7315 na 7311 kwa ajili ya shughuli za uwekezaji. Mgogoro katika eneo hili unatokana na baadhi ya wananchi kuingia na kuanza kufanya shughuli mbalimbali katika ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Morogoro Sugar kupitia TISEZA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua mbalimbali za kutatua migogoro ya ardhi baina ya mwekezaji, wakulima na wafugaji katika maeneo hayo niliyoyataja, Serikali imechukua hatua zifuatazo:-
(i) Mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vyote vinavyozunguka mashamba hayo imeandaliwa na wananchi wameanza kupewa Hati za Hakimiliki za Kimila;
(ii) Kamati iliyowashirikisha wananchi wa vijiji husika na viongozi iliundwa kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa mrejesho kwa wananchi kuhusu hatua zilizofikiwa katika utatuzi wa migogoro;
(iii) Wananchi wameendelea kupewa elimu kuhusu umuhimu wa kuheshimu mipango ya matumizi ya ardhi iliyopitishwa; na
(iv) Mwisho lakini si kwa umuhimu, viongozi wa vijiji wanaowauzia wananchi ardhi ndani ya eneo lililotolewa kwa shughuli za uwekezaji wameendelea kuwajibishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka mashamba haya, Serikali inawaagiza kuzingatia sheria na kanuni za umiliki wa ardhi ili kuondoa migogoro hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -
Je, zipo sheria zinazolinda maeneo ya wazi na viwanja vya michezo kwenye majiji na miji nchini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba sasa nijibu swali Na. 93 la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalumu Tanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upangaji na usimamizi wa matumizi ya ardhi unaongozwa na sera, sheria na kanuni mbalimbali za usimamizi wa maeneo ya wazi ambayo yanajumuisha maeneo ya viwanja vya michezo. Sera na sheria hizo ni pamoja na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya Mwaka 2000, Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 (Toleo la Mwaka 2023) na Sheria ya Mipango Miji, Sura ya 355 na Kanuni zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 4(3)(9) ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya Mwaka 2,000 imeelekeza kulindwa kwa maeneo ya wazi kwa ajili ya matumizi ya umma. Aidha, Kanuni ya 6(3)(a) ya Kanuni za Mipango Miji iliyochapishwa katika Gazeti la Serikali Na. 91 la Mwaka 2018 inazuia kubadilisha matumizi ya maeneo ya wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika, Sheria ya Mipango Miji, Sura ya 355 kama ilivyorekebishwa mwaka 2023 ilizipatia Mamlaka za Upangaji jukumu la kupanga, kupima, kutunza na kusimamia maeneo ya wazi kwa kuzingatia mipaka yao ya kiutawala. Vilevile, Kanuni ya 4(7) ya Kanuni za Sheria ya Mipango Miji za Mwaka 2018 zilizotangazwa kupitia Gazeti la Serikali Na. 88 la Mwaka 2018 imetoa utaratibu wa udhibiti na usimamizi wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, ninaomba kutoa rai kwa Mamlaka za Upangaji kuhakikisha maeneo ya wazi nchini yanatengwa, yanalindwa na kuendelezwa kwa kuzingatia sera, sheria na kanuni zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.