Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dotto Jasson Bahemu (2 total)

MHE. DOTTO J. BAHEMU aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Nyakahura – Rulenge – Murugarama kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Nyakahura – Rulenge – Murugarama yenye urefu wa kilometa 85.6 unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa sasa maandalizi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kuanzia Keza yanaendelea, ambapo tayari mkandarasi amepatikana na taratibu za malipo ya awali zinaendelea ili aweze kuanza kazi. Mara baada ya taratibu za malipo ya awali kukamilika kazi za ujenzi zitaanza. Kwa sehemu iliyobaki, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuijenga barabara yote. (Makofi)
MHE. DOTTO J. BAHEMU aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanzisha Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Sekondari Ngara Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dotto Jasson Bahemu, Mbunge wa jimbo la Ngara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikijenga shule mpya za kidato cha tano na sita au kuongeza miundombinu katika shule za sekondari zilizopo ili kuzipandisha hadhi kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 hadi 2025/2026, Serikali imepeleka shilingi bilioni 2.08 katika Halmashauri ya Ngara kwa ajili ya kuongeza miundombinu katika Shule saba za Sekondari za Rusumo, Kabanga, Lukole, Muyenzi, Murugamba, Ndomba na Ngara High School na kuzipandisha hadhi ambapo kwa sasa zina jumla ya wanafunzi 6,881 wa kidato cha tano na sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Shule ya Sekondari ya Ngara Mjini, shule hii kwa sasa haina mahitaji makubwa ya kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita. Shule ya Sekondari Ngara Mjini ipo katika Tarafa ya Nyamiaga yenye shule tatu za kidato cha tano na sita ambazo ni Rusumo, Lukole na Ngara High School zenye jumla ya wanafunzi 2,915. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha za ujenzi wa miundombinu ya kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita kwa kuzingatia tathmini ya mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.