Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dotto Jasson Bahemu (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DOTTO J. BAHEMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, ninaomba niungane na Mwenyekiti wetu, kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama kijana nimejua kwamba, vijana wote wanafarijika pale ambapo vijana wenzetu wanapata nafasi, wanazitumia vizuri na wanazitendea haki. Mheshimiwa Waziri Anthony Mavunde anaitendea haki sana nafasi yake, ambayo Mheshimiwa Rais amemwamini. Tunampongeza, sisi vijana wenzake na anazidi kutu-inspire katika maeneo mengine na tunamtakia kila la heri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tunajua kwamba, hakuna kijiji kisicho na wazee, kaka yetu pia, Naibu Waziri, tunampongeza sana kwa msaada mkubwa anaoutoa kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na Menejimenti nzima ya Wizara. Baada ya pongezi hizo, sisi katika Jimbo letu la Ngara tuna Mradi wa Kabanga Nickel; kama ambavyo maeneo mengine yana dhahabu, mengine yana almasi, sisi katika Jimbo la Ngara na Wilaya ya Ngara Mwenyezi Mungu ametujalia tumepata nickel, lakini imekuwa ni story ya muda mrefu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa takwimu ama kumbukumbu inaonesha kwamba, utafiti wa kwanza ulianza kufanyika mwaka 1976 pale Kabanga Nickel. Hii ni kwa mujibu wa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano wakati wakisaini mkataba na kampuni ambayo inatakiwa kuendesha huu mradi, alisema yeye mwenyewe kwamba, utafiti wa kwanza ulianza mwaka 1976.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi chote hicho ambacho sisi watu wa Ngara tumekuwa tunasubiri kwa muda mrefu kuweza kunufaika na ile rasilimali ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia, mpaka leo hakuna namna ambavyo tunaweza tukasema kwamba, tupo tumenufaika au tunaona dalili za kunufaika. Kwa bahati mbaya ni kwamba, hata jitihada zote ambazo zinafanywa na Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Rais kwa sasa hivi, mimi Bahati nzuri nimekuwa ninazungumza na Mheshimiwa Waziri mara kwa mara, ameniambia jinsi ukweli ulivyo na ninauona mwanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa siku ya leo ninamwomba Mheshimiwa Waziri, kwa mdomo wake, aongee na watu wa Ngara atuambie Mradi wa Kabanga Nickel ni lini unaanza? Kauli moja tu! Atuambie Mradi wa Kabanga Nickel ni lini unaanza? Hilo tu litakuwa limetosha; sisi hatuna kitu kingine ambacho tunataka kusikia kwa siku ya leo kutoka kwa Waziri zaidi ya kwamba, Mradi wa Kabanga Nickel unaanza lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, siyo kwamba hatuamini, tunaamini kwamba ni kitu kinakuja kutokea, lakini kwa bahati mbaya sisi watu wa Ngara tulishang’atwa na nyoka huko nyuma, sasa hivi tukiona majani tunakuwa na wasiwasi. Kuanzia mwaka 1976 mpaka leo ambavyo tunaendelea, tumekuwa tunaona zinakuja kampuni; inakuja kampuni hii inatoka, inakuja kampuni nyingine inatoka, inakuja kampuni inatoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi uelewa wetu, wananchi wa kawaida, ni tunajua kwamba, tayari pale shughuli zinaendelea. Hayo mambo ya kitaalam wanayajua wao kwamba, sijui ni utafiti! Sijui ni nini, lakini sisi wananchi wa kawaida ambao tumezunguka eneo lile, ambao tunategemea tuwe tunanufaika na eneo lile, tunajua kwamba shughuli zinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mwaka 2021 tunakumbuka ndipo mkataba ulisainiwa, kwa ajili ya kuanza huu mradi rasmi, miaka mitano iliyopita. Ninakumbuka kwenye ile hafla ya kusaini ule mkataba iliyofanyika Bukoba, mgeni rasmi alikuwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano na miongoni mwa watu ambao walitufanya sisi watu wa Ngara tukapata faraja kwamba sasa tunaenda kunufaika ni Mheshimiwa Profesa Kabudi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Profesa Kabudi wakati anaelezea manufaa ya ule mradi, item Namba 7 aliyoitaja, ninaomba niinukuu alisema: “Miongoni mwa faida za huo mradi ni kuendeleza biashara, uchumi na maisha bora kwa Wilaya ya Ngara na Wilaya ya Kahama na wananchi wake kwa ujumla”. Akamalizia kusema, “Ngara Oyee!”, akamalizia kusema “Kahama Oyee!”. Sasa, leo ni miaka mitano imepita tangu kauli zile za kututia matumaini za Mheshimiwa Profesa Kabudi, ambazo alizitoa jinsi ambavyo tunaenda kunufaika na Tembo Nickel, lakini mpaka sasa hivi watu wa Ngara wanaamini kwamba, ni story zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu, tumepita katika vipindi mbalimbali vya kuambiwa hiki kitaenda hivi, hiki kitaenda vile, mpaka leo, hata angekuja nani leo akatuambia, mimi ninajua kwa sababu, pengine angalau nimepata nafasi ya kuwa kwenye Kamati ya Nishati na Madini, ninajua kwamba, kuna kitu kinakuja, lakini watu wa Ngara wanaamini ni story kwa sababu, story za hivyo wameambiwa kwa miaka mingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, leo inawezekana ikawa ni siku ambayo wananchi wa Ngara watafurahi sana watakapomsikia Waziri. Kwa kipindi chote ambacho kimepita Mheshimiwa Waziri, tunaomba basi leo awafurahishe watu wa Ngara, awape matumaini, awaambie Mradi wa Kabanga Nickel utaanza lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijana wengi wa kule Ngara wameomba kazi katika huu mradi ambao wanaamini kwamba, unakwenda kuanza, sasa hata akipata kazi sehemu nyingine anaogopa kwenda kwa sababu, anategemea hapa kwa hiyo, kuna vitu vingi sana vime-stuck. Kuna watu wengine wameanza kutengeneza biashara zao, wameanza kubuni mawazo ya biashara, lakini kila siku kitakuja hiki, kesho kitakuja kitu kingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ilitokea huko nyuma tukawa tunaamini kwamba hiki kitu kinaenda kutokea na kwa sababu hakijawahi kutokea, Mheshimiwa tunaomba atushangaze watu wa Ngara, basi tunaomba itokee. Sisi Ngara mambo ambayo huwa tunayaomba kwa Serikali, ni mengi. Wakati huu ambao tumekuja tumesema vitu vingine, wakitupa vitaenda kupunguza shida nyingine hata hawatapigiwa kelele.

Mheshimiwa Naibu Spika, watakapotupa Tembo Nickel kuna mambo mengine automatically yataanza kujipeleka. Sisi watu wa Ngara hatutalalamika kwa sababu, tunaamini tutapata ajira, tutapata uchumi kama ambao alisema Mheshimiwa Profesa Kabudi, lakini kama itaendelea kuwa story, kama miaka yote, sisi watu wa Ngara tutaendelea kuwa disappointed. Tunaomba Mheshimiwa Waziri, mimi ninamjua vizuri sana, ninajua jinsi gani ambavyo yuko committed na mara kwa mara amekuwa akiniambia nenda kaa vizuri na Tembo Nickel, kitu kinaenda kuanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba, watu wa Ngara nimewaambia vitu vingi sana, vingine vinatokea vingine vitakuja kutokea, lakini vingine havitatokea. Hili wakilisikia kutoka mdomoni mwa Waziri leo, atapokuwa anahitimisha hapa, atuambie Tembo Nickel inaanza lini na Kabanga Nickel inaanza lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Ngara watamshukuru na sisi tunamwombea kila la heri, tunamtakia utekelezaji mwema wa bajeti yake, ili kuwa na mengi, lakini ninaomba nisichanganye hili la Tembo Nickel na na kitu kingine. Ninaomba leo libaki hilo hilo la Tembo Nickel peke yake, ili kama ananijibu, anijibu hilo peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DOTTO J. BAHEMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara yetu ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mwanzo kabisa kabla sijaanza kuchangia naomba nikutaarifu kwamba, mimi pia, ni mwanahabari. Nimetoka chumba cha habari kwenda kugombea Ubunge kwa hiyo, nimetoka kwenye habari nikaenda kwenye Ubunge moja kwa moja kwa hiyo, masuala yote ambayo yanahusu habari, hata kama siyafahamu kwa kina sana, lakini angalau ninajua vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri amekuwa ni mbunifu katika maeneo mbalimbali ambayo amekuwa akipita na mimi binafsi nimefanya naye kazi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, nimefanya naye kazi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Baada ya pale akaenda benchi tukapotezana kidogo kwa sababu, nilikuwa na kazi yeye hakuwa na kazi. Akatoka akawa Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi, nimefanya naye kazi, lakini vilevile sasa hivi ambapo pia, ni Mheshimiwa Waziri ninashukuru kwamba, nafanya naye kazi nikiwa Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi chote ambacho nimefanya naye kazi, nimeshuhudia jinsi gani ambavyo ni mbunifu. Sisi vijana ambao tulikuwa tunamsaidia katika kutekeleza baadhi ya vitu ambavyo alikuwa anavifanya tunamshukuru kwamba, tulikuwa tunakaa na mtu ambaye unaona anawaza vitu kwa namna ya kipekee, namna kitofauti na hata sisi tunafurahi sana kwenda kutekeleza yale mambo ambayo anakuwa ametuomba twende tukayafanye. Kwa hiyo, ninampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hivyo, ninajua akiwepo Mheshimiwa Waziri Paul Makonda, Mheshimiwa, Naibu Waziri, Hamis Mwinjuma, ambaye naye katika eneo la sanaa amefanya vizuri kwa kipindi cha muda mrefu pamoja na kwamba, anaonekana bado ni kijana mdogo, lakini kwa sanaa ni legend kwa hapa Tanzania. Vilevile wanaye Katibu Mkuu, ambaye anaifahamu vizuri sana sekta na Taaluma ya Habari, ambaye amekuwa ni mwanahabari mwenzetu, ambaye ametokea pia, Chumba cha Habari; mpaka hapa alipo amefika kwa kupitia katika Taaluma ya Habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaamini kwa utatu huu wakisaidiwa na watu wengine wanaosaidia katika Wizara. Ninaamini Wizara yetu sisi, kama wanahabari, itakwenda mbele zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimesikiliza michango tangu asubuhi. Niseme ni kwa bahati nzuri au bahati mbaya kwamba, Wizara yetu ni kubwa, ina habari, utamaduni, sanaa na michezo vilevile, lakini Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza sana upande wa, aidha sanaa au michezo. Sasa sisi ambao ni wachache, wanahabari, ninaomba angalau tupate nafasi hii kuzungumzia kidogo kwenye sekta ya habari.


Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wakati anaingia madarakani sisi ambao tulikuwa ni waandishi wa habari tuliona ni kwa namna gani ambavyo taaluma ile ilibadilika na tukatoka katika kipindi ambacho tulikuwa tunafanya kazi katika mazingira magumu na tukaenda katika kipindi ambacho tulikuwa tunafanya kazi katika mazingira ambayo ni rafiki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoka katika kipindi ambacho tulikuwa tunaitwa kwenda kutoa maelezo unaamini kwamba, ninaenda kufungwa pingu, ninaenda kufungiwa, lakini tukaenda katika kipindi ambacho ukiitwa kwenda kutoa maelezo TCRA, unaenda kupongezwa kwa kazi nzuri, ambayo umeifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni mabadiliko makubwa sana ambayo yamefanywa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge kuna watangazaji wengi sana ambao mlikuwa mnawasikia katika kipindi cha nyuma, ambao sasa hivi inawezekana hamuwasikii; wapo ambao wametoka kwenye taaluma zao ama kwenye hii kazi kwa sababu mbalimbali, lakini wapo ambao wametoka kwa kulazimika kutoka kulingana na Sheria ambayo ilitungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ile siyo mbaya ni nzuri na sisi, kama Waandishi wa Habari, tunaipongeza kwa sababu, inatengeneza mazingira ya taaluma yetu ya habari kwenda kuheshimika siku za usoni. Leo ninavyozungumza ninaamini baada ya miaka mitano ijayo mwandishi wa habari atakuwa akisimama akizungumza anaonekana kweli mtu amezungumza, ambaye ana kazi yake ambayo inaeleweka kwa sababu ya ile sheria, ambayo inakwenda kutulinda sisi waandishi wa habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ambapo wameingia katika kipindi hiki ninawashukuru sana. Waziri amezungumza vizuri kwamba, wale waandishi wa habari wenzetu ambao sasa hivi hawapo kwa sababu ya matakwa ya kisheria ya kutokuwa na ithibati, ni kwa namna gani ambavyo atakwenda kuona siku za usoni watarudi kujiunga na sisi, ili waendelee kufanya kazi wapate vipato na waweze kuendesha familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwe na namna ya kutengeneza mazingira ya kwenda kuwasaidia kwa sababu, wale ambao wametoka siyo muda mrefu kuna waandishi wamefanya kazi kwa miaka mingi, lakini sasa hivi hatuko nao. Waziri amezungumza vizuri kwamba, wanatengeneza utaratibu wa kwenda kuwasaidia, kwenda kuwarudisha katika ajira zao baada ya kuwa wamewatengenezea utaratibu mzuri wa kwenda kuwapa ithibati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tangazo lile lilivyotoka kuna waandishi ambao walilazimika kutoka kwenye ajira zao, vyombo vyao vikawaondoa kwamba, waende sasa wakapambane, kwa ajili ya kutafuta ile ithibati kwa hiyo, wakatolewa kwenye payroll na mikataba yao ikasitishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Waziri anavyozungumza kwamba, wanaenda kutengeneza mazingira mazuri ya kwenda kutafuta namna ya kuwarudisha lazima pia, wakumbuke kwamba, zile ajira walizokuwanazo huku nyuma sasa hivi hazipo tena. Kwa hiyo, watakapotafuta namna ya kwenda kuwapa ithibati, Mheshimiwa Waziri tunajua Waziri na wasaidizi wake wote ni wabunifu, basi watafute namna ya kuwasaidia wale wengine ambao sasa hivi wako benchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ambao wamefanya kazi miaka 30, miaka 25, wengine hawana taaluma ya uandishi wa Habari, lakini wana taaluma nyingine. Watafute namna ya kuwasaidia kwenda kulinda zile ajira zao ambazo zimepotea. Sote tunaamini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kipenzi cha wanahabari na angependa kuona hakuna ajira ya Mtanzania yeyote ambayo inapotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotuona sisi waandishi wa habari tunavaa vizuri, tunapendeza, tunajipenda sana na huwa tunakaa hata sehemu ambazo wanakaa watu wa juu, tunakaa meza moja, lakini haimaanishi kwamba, tuna maisha mazuri, kama waliyonayo wale ambao tunakaa nao meza moja. Waandishi wa habari hali zetu ni ngumu sana kiuchumi kulingana na zile sehemu ambazo tunafanyia kazi. Vyombo vya habari ambavyo tunavifanyia kazi hali zao za kiuchumi ni mbaya sana kwa sababu mbalimbali, lakini moja ya sababu kubwa ambayo tunaizungumza ni, vyombo vyetu vya habari havijatengenezewa mazingira mazuri ya kufanya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile ambavyo vimetengenezewa mazingira mazuri ya kufanya biashara vinakopwa na Serikali, lakini Serikali hiyo hiyo inachelewa sana kwenda kulipa yale madeni. Kwa bahati mbaya, ukichelewa kulipa chombo cha habari madeni TRA hatajua kwamba, unaidai Serikali, umechelewa kulipa, NSSF hatajua kwamba, unaidai Serikali umechelewa kulipa, yeye atakuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wewe ambaye unamiliki chombo cha habari ni lazima utengeneze mazingira ya kuilipa Serikali, lakini katika mazingira ya kuilipa Serikali ambaye utamdanganya ni mwandishi wa Habari, yule ambaye umemwajiri kwa hiyo, atakaa mwezi wa kwanza, mwezi wa pili, mwezi wa tatu hajalipwa. Kwa hiyo, ninakuomba Mheshimiwa Waziri, wakati wa nyuma kidogo kuna kamati iliundwa, ambayo ilikuwa mahususi, kwa ajili ya kupitia uchumi wa vyombo vya habari na kwenda kutoa mapendekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile kamati ilimaliza kazi yake na yale mapendekezo yalitolewa. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri arudi kule Wizarani akaombe taarifa ya ile kamati, ambayo ililetwa. Akaangalie ni vitu gani ambavyo vilikuwa vimeandikwa ama vilikuwa vimependekezwa katika ile kamati, ili aende akaifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa mambo ambayo yalipendekezwa ni kwenda kulipa madeni ya vyombo vya habari ambavyo vinadai, lakini vilevile vyombo vya habari kwenda kukopeshwa mikopo rafiki, mikopo ambayo haina ugumu kuipata, ambayo itakuwa na riba nafuu, ili vyombo vya habari vikope viende kufanya kazi na wananchi, sisi Watanzania waandishi wa habari tuweze kulipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana Mheshimiwa Waziri. Kama ambavyo Waziri amepambana amepata shilingi bilioni 20, kwa ajili ya kuwakopesha watengeneza maudhui, anashindwa nini kutafuta fedha nyingine, kwa ajili ya kwenda kutafuta mikopo ya kuvikopesha vyombo vya Habari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, hivi vyombo vya habari ndivyo ambavyo vinakwenda kufanya au vinakwenda kuelezea yale mazuri ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyafanya. Wanafanya kwa uzalendo wao, lakini tunatengeneza mazingira ya kuvidhibiti vyombo vya habari vya ndani, wakati huo tunasahau kwamba, kuna vyombo vya habari vya nje ambavyo vinaweza vikatufikia kirahisi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano tu ni vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi. Vyombo vya habari vya ndani tunashukuru walikuwa wazalendo wakakaa upande wa Taifa, lakini ukija kuangalia kuna vyombo vya habari vya nje ambavyo ndivyo vilileta taarifa ambazo ni za uongo, ambapo tumetengeneza mazingira ya kuwadhibiti hawa ambao watakuwa wazalendo, lakini wale wengine ambao watakuja kuleta taarifa za uongo hatuna access ya kuweza kuwadhibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, yeye amekuwa ni rafiki wa wanahabari, Mwana-FA, Mheshimiwa Naibu Waziri, amekuwa ni rafiki wa wanahabari na Katibu Mkuu ni mwanahabari mwenzetu kwa kipindi cha muda mrefu. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alivyoingia watu ambao aliwatengenezea mazingira ya kunyosha vitu haraka haraka walikuwa ni waandishi wa Habari kwa hiyo, tunaamini hata haya mambo mengine hawawezi kushindwa kwenda kuyafanya. Tunaamini, muda siyo mrefu basi angalau hata sisi wanahabari tutakuwa tunashukuru kwamba, maisha yetu yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia ninaomba nitoe pendekezo moja la mwisho kabisa. Vyombo vya habari vya kielektroniki, kwa maana ya televisheni na redio, wao wanawajibika kwenye Kamati ya Maudhui ya TRA...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. DOTTO J. BAHEMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono moja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DOTTO J. BAHEMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusiana na maendeleo ya vijana. Nami nikiwa kama kijana, basi ninashukuru angalau nimepata nafasi hii ya kuzungumza na Serikali, na vilevile kuzungumza na vijana wenzangu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu sisi kama vijana tumekuwa tuna changamoto nyingi ambazo kwa bahati mbaya zilikuwa hazipati ufumbuzi wa haraka kwa sababu zilikuwa zinashughulikiwa na idara. Tulikuwa ni idara ya vijana ambayo ilikuwa katika ofisi ambayo inashughulikia matatizo mengine mengi. Kwa hiyo, sisi vijana tulikuwa ni kama idara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwa mara ya kwanza katika uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, sisi vijana tumetolewa kuwa kama idara, sasa tumekwenda kupewa Wizara rasmi ya kwenda kushughulikia matatizo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na tunampongeza sana kwa sababu tunaamini kwamba pamoja na matatizo mengi tuliyonayo sisi kama vijana, lakini hili la kutupa Wizara ambayo ita-deal na vijana pekee yake, angalau inatoa mwanga kwamba yapo mazuri mengi ambayo yanakuja kwa ajili ya vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso kaka yangu huwa anasema kwamba “Asiyeshukuru kwa kidogo, hata kwa kikubwa hawezi kushukuru.” Kwa hiyo, vijana tunashukuru angalau kwa hili tu la kutupa visa. Sisi vijana, hili tu peke yake, tunashukuru, tunajua mambo mengine mengi yanakuja, Mheshimiwa Rais atakwenda kuyamaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninaomba kumpongeza kaka yangu Mheshimiwa Waziri, ameeleza katika hotuba yake mambo ambayo ameyafanya tangu amekabidhiwa hii Wizara. Ni Wizara mpya, lakini ameeleza mlolongo wa mambo mengi sana ambayo yamefanyika ndani ya kipindi kifupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunampongeza yeye pamoja na watendaji wake. Tumekuwa tukiona vilevile ambavyo anaenda katika maeneo mbalimbali, anakunywa chai na bodaboda, anakula maandazi na mamalishe. Hii inaonyesha jinsi gani ambavyo Mheshimiwa Rais hakukosea kumpa Mheshimiwa Joel kuwa msimamizi wa sekta yetu sisi vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zote ambazo zinahusu vijana, mwisho wa siku zinaongea katika eneo moja. Vijana inawezekana tunaambiwa tunahitaji vitu vingi, lakini tunahitaji kitu kimoja tu, fedha. Tunahitaji fedha, siyo kitu kingine chochote kile. Sasa fedha inapatikana kupitia njia mbalimbali; kuna ajira, kuna ujasiriamali, na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata mipango mingine yote ambayo tutakuwa nayo, kama kijana hatakuwa na fedha ina maana hatuna uhakika kama vijana tutakwenda kuridhika, kwa sababu changamoto nyingine kubwa sana ambayo inatajwa ni ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama vijana tukitendewa haki katika eneo hili kwenye hii Wizara yetu ya Vijana, vijana tukapata yale ambayo tunahitaji, ina maana hata tatizo la ajira kwa nchi yetu litakwenda kupungua kwa kiasi kikubwa sana, kwa sababu vijana wengi ndiyo ambao wanahitaji ajira. Ni kwa bahati mbaya kwamba ukiangalia jinsi ambavyo mambo yanaenda, hatuoni kama kuna mwanga wa tatizo la ajira kumalizika kwa siku za karibuni. Kwa hiyo, ambacho kinaweza kikafanywa na Serikali ni kutuwezesha sisi vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia Mheshimiwa Waziri amekuja na jambo zuri kuhusiana na Benki ya Vijana, tunapongeza sana kwa hili, lakini kabla Benki ya Vijana haijaanza, sisi vijana hapa katikati tunaishije?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona tulipewa shilingi bilioni 200, lakini naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wengine wote ambao wamesema kwamba zile shilingi bilioni 200 zimeenda tofauti na vile ambavyo sisi vijana tulikuwa tumetarajia, zimeenda katika maeneo mengine mengi ambayo wengine hatuwezi kukajua huku kuna kiasi gani wala utatuma kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa kipindi hiki ambacho bado tunasubiri Benki ya Vijana ianze, tumeshuhudia majanga mbalimbali ambayo yametokea kwenye nchi yetu, tumeshuhudia sehemu nyingi ambazo zimekuwa na changamoto, Serikali imepeleka ruzuku. Kwa hiyo, changamoto ya ajira kwa vijana, changamoto ya ukosefu wa kipato kwa vijana sasa hivi tunaomba Serikali basi ichukulie kama ni suala la dharura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikichukulia kama ni suala la dharura, ina maana hata ile shilingi bilioni 200 ambayo tumepewa, ambayo imeenda katika maeneo mengine tofauti, Serikali tunaomba ituongezee sisi vijana. Tunaomba Serikali itukopeshe twende tukapambane kutafuta fedha, tutarudisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo ambayo Serikali inapeleka ruzuku ili mambo fulani yafanyike vizuri, lakini sisi hatutaki ruzuku, ninaomba mtukopeshe hizo fedha, na tutengenezewe mazingira mazuri ya kuzirejesha. Vilevile ninaomba tutengenezewe mazingira mazuri ya sisi kukubalika tuweze kukopesheka, kwa sababu changamoto kubwa ambayo inatukabili vijana ni kwamba ukienda utaambiwa njoo na dhamana, au vitu mbalimbali ambavyo lazima upeleke kwa ajili ya kupata mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali ikitudhamini yenyewe, Serikali ina watu mpaka ngazi ya kijiji, mpaka ngazi ya kitongoji ina watu ambao ni wasimamizi. Kwa hiyo, nikiomba mkopo, itajulikana Dotto anakaa sehemu fulani, Mwenyekiti wake wa Mtaa ni fulani, Mtendaji wa Kijiji ni fulani. Kwa hiyo, siwezi kutoroka na hizo fedha hata kama sina dhamana, lakini niaminiwe kwa kitambulisho cha NIDA, kwa vyeti vyangu vya shule, kwa uongozi wa Serikali ambao uko pale. Mniamini mnikopeshe ile fedha halafu mwone baada ya muda mrefu kama sitakuja kurejesha. Tukirejesha na wenzetu watapata; na mkitupatia, changamoto ya ajira itabaki ni historia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama leo mwanafunzi ambaye amemaliza chuo kikuu anaweza akaenda Kariakoo pale, akaongea na mtu mwenye duka akamwambia naomba tisheti 10 niende nikauze nikishauza nitakurejeshea fedha yako nami nipate cha kwangu, mtu mwenye duka anamwamini yule mwanafunzi, kwa nini Serikali isituamini sisi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imani tuliyonayo kwa Serikali yetu ni kubwa sana na haya mambo ambayo tunayaomba, tunayaomba tukiamini kwamba yanawezekana. Tumesikia fedha ambazo zimeenda sijui content creators, sijui nini, kila sehemu ambazo fedha zimeenda unaanza kuona watu wanakuwa wengi katika lile eneo. Siyo kwamba watu wanafanya vile vitu, lakini ndiko wameona ambako kuna fedha. Kwa hiyo hata zile fedha shilingi bilioni 200 zingebakizwa kwa vijana, sisi vijana ndiyo tunajua tunataka tufanye nini? Msitulazimishe kwenda sijui kufanya hiki, kufanya hiki, au kufanya hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wangepeleka kwa vijana pale, sisi tutajua zile shilingi bilioni 200, Mheshimiwa Joel atajua yeye na vijana wenzake tuzigawane vipi twende tukafanye kazi tuweze kurudisha marejesho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, changamoto kubwa ambayo inatukabili sisi vijana, ni kuwa walalamishi. Tunakuwa walalamishi kwa sababu kuna kikundi kidogo cha watu ambao wamejipa usemaji wa vijana kwamba wao ndio wasemaji wa vijana, lakini kile kikundi siyo kikundi sahihi, ni kikundi ambacho hakina suluhisho la vijana lolote. Ni kikundi ambacho kinatufundisha sisi vijana kulalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kuongea na vijana wenzangu Waheshimiwa Wabunge. Vijana wenzangu Tanzania, tusikubali kuingizwa kwenye huo mkenge wa kuwa walalamishi kwa sababu ya watu wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaye Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye tayari ameshaonesha mwanga kwamba matatizo ya vijana yanawezekana. Tusikilize sauti zinazotoka kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kijana mwenzetu ambaye ameaminiwa, huyo ndiye awe msemaji wetu vijana. Tusikubali wahuni wengine wakabeba ajenda ya kutusemea sisi vijana wakati sisi vijana tupo, na tunajua kwamba matatizo yetu yanatafutiwa ufumbuzi kwa jinsi ambavyo Dira imeoneshwa na Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba kuwaasa vijana wenzangu Wabunge pamoja na vijana wenzangu kote kule walipo, tukatae wahuni, tumsikilize Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Waziri wetu. Hao ndio wamebeba maono ya Sekta ya Vijana na siyo mtu mwingine yeyote yule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)