Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Daniel Godfrey Chongolo (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa mara ya kwanza kuchangia ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, pili, nimshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuniamini na kunipa heshima ya kusimamia sekta muhimu ya kilimo nchini. Nimhakikishie imani hii itazaa imani.

Mheshimiwa Spika, pia niwashukuru Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa miongozo ambayo wanaendelea kutupatia sisi wasaidizi wao. Nitakuwa ni mchoyo wa fadhila nisipokushukuru wewe binafsi kwa namna unavyotuongoza ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja. Ninaunga mkono hoja kwa nini? Kwa sababu, kwanza Waziri Mkuu ameonesha kwa kina katika mapendekezo ya bajeti inayohusu ofisi yake kuwa, dhamira ya Serikali ni kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika, ninasema ameonesha kwa kina kwa namna gani? Kwanza, kabla ya kuiwasilisha kwa muda mfupi amefanya kazi kubwa sana, ameshatembea katika mikoa mbalimbali nchini na huko ametufundisha wasaidizi wake namna ya kuwajibika na changamoto za wananchi moja kwa moja kwa wananchi kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, leo ukienda kwenye maeneo ambayo tayari Waziri Mkuu amepita na sisi askari wake wa mwavuli Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao tuliambatana naye kwenye maeneo kadhaa unaona tabasamu ambalo Rais aliliahidi kwa Watanzania likianza kuonekana.

Mheshimiwa Spika, katika kuchangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wabunge 27 walitoa hoja mbalimbali zinazohusu sekta ya kilimo nchini, nami ninawashukuru sana Wabunge wote kwa michango yenu. Tumeichukua michango yote na niwahakikishie kwamba kupitia bajeti ya Wizara ya Kilimo nitaonesha namna yale ambayo wameyachangia hapa yanavyokwenda kutafutiwa majawabu.

Mheshimiwa Spika, maeneo makubwa yaliyokuwa yamegusiwa ni manne, eneo la kwanza kwenye michango ya Waheshimiwa Wabunge ilikuwa ni kuhusu pembejeo za kilimo, kwa maana ya mbolea, mbegu na viuatilifu. Eneo la pili lilikuwa ni umwagiliaji na tatu lilikuwa ni masoko na uongezaji wa thamani ya mazao, eneo la mwisho ni ushirika na mitaji inayotokana na vyama vya ushirika, lakini pia benki zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa pembejeo za kilimo, ushauri wa Wabunge tumeuzingatia sana, niwahakikishie tutaendelea kuimarisha utoaji wa ruzuku za pembejeo za kilimo nchini na kuweka mifumo itakayowezesha pembejeo za kilimo kuwafikia wananchi katika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, pembejeo za kilimo ndiyo zinazojenga msingi wa kutafuta matokeo ya kilimo chenyewe na wananchi kwa muda mrefu wamekuwa wakisema kilimo ni uti wa mgongo, lakini ukiangalia uti wa mgongo ni sehemu ya mgongo, kuita kilimo ni uti wa mgongo ni kupunguza ukubwa wa kilimo chenyewe, kwa sababu uhalisia kwa kweli kilimo ndiyo mgongo wenyewe.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ijayo ya Wizara ya Kilimo maeneo ya msingi ambayo tumeyapa kipaumbele na tutayapa kipaumbele ni kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo. Pia, kutenga fedha kwa ajili ya kulipa madeni ya fedha za ruzuku ambazo zimekuwa bado hazijakamilika kulipwa kwa mawakala, lakini pia na kwa suppliers wa mbolea na pembejeo nyingine. Pia kupanua wigo wa upatikanaji wa pembejeo karibu na wananchi, kwa sababu tukiwasogezea karibu tutawasaidia kupunguza usumbufu wa kufuata kwenye maeneo ya mbali na kuongeza gharama.

Mheshimiwa Spika, jambo kubwa ni kuhakikisha tunawekeza kwenye upatikanaji wa mbegu ili kupunguza changamoto ya mbegu feki. Katika hili moja ya kazi kubwa ambayo tumefanya ni kuimarisha na kuiongezea uwezo taasisi yetu ya mbegu ya ASA ili iweze kutumia mashamba yake kwa kiwango kikubwa kuzalisha mbegu.

Mheshimiwa Spika, katika hili tumetengeneza mfumo wa contract farming. Mwanzo ASA alikuwa anatafuta fedha kwa ajili ya kwenda yeye mwenyewe kulima na changamoto alikuwa akilima mvua ikiwa chache au kukiwa na changamoto yoyote, mavuno yakiwa machache matokeo ya mbegu yatakuwa hivyo hivyo mwishoni. Ili kuepukana na hilo sasa tumejielekeza kuisukuma ASA kutoa mashamba kwa wakulima binafsi na kuingia nao mkataba, wao walime halafu waingie mkataba wa kuuziana mbegu na ASA, ili ASA kwa bajeti yake ya mbegu aweze kupata asilimia 100 ya mbegu alizozipangia kwenye bajeti.

Mheshimiwa Spika, hilo linalenga kuhakikisha matokeo yake ya upatikanaji wa mbegu kwa wananchi, tena mbegu bora yanaongezeka na kuwaondoa wananchi kwenye changamoto ya kupata mbegu maarufu feki.

Mheshimiwa Spika, moja ya eneo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge waligusia ni kuhusu nafaka, ununuzi wa nafaka na hasa mahindi ambapo kila msimu tumekuwa tukinunua kupitia taasisi yetu ya NFRA. Tuwahakikishie mwaka huu tumefanikiwa kununua mahindi yenye thamani msimu uliopita shilingi bilioni 95.3 na mpaka sasa tumeshafanikiwa kulipa shilingi bilioni 93.1 bado bilioni mbili kasoro kidogo ambayo mpaka mwezi huu mwishoni tarehe 30 tutakuwa tumekamilisha kulipa ili wakulima waendelee kujibidiisha kwenye kilimo na siyo vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, kikubwa niwahakikishie Wabunge kwamba dhamira ya Wizara ya Kilimo na Serikali ni kuhakikisha inaendeleza kilimo kuwa mgongo kamili lakini kuwa ndiyo sehemu ya msingi ya watanzania walioamua kujielekeza kwenye shughuli za kilimo kunufaika na kujikwamua na umaskini.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo tutahakikisha kila linalotustahili kulifanya tunalifanya ili kutafuta matokeo yanayokusudiwa, kwa yote ambayo nilisema mwanzo yanahitaji kuingia kwenye bajeti yakiwemo ya masoko na hasa masoko ya mipakani ambayo kwetu ni muhimu, yakiwemo maeneo ya kukusanyia na vituo vya kukusanyia nafaka pamoja na matunda, nitayaonesha kwa kina kupitia bajeti ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha na ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsanteni kwa kunisikiliza. (Makofi)