Supplementary Questions from Hon. Dr. Yahaya Esmail Nawanda (3 total)
MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kujenga minara katika Kata za Mtunguru, Mkwedu, Chilangala pamoja na Mikumbi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Nawanda, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Wizara inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Minara 280 katika bajeti hii na katika bajeti ijayo tutatekeleza tena mradi wa kujenga minara mingine 280 ambayo katika mradi huo Kata alizozitaja Mheshimiwa Mbunge nazo tutazipatia kipaumbele. (Makofi)
MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Mfuko wa Barabara umekuwa unagharamia zile barabara ambazo ziko rasmi na umekuwa unajenga Barabara kutoka Mkoma Sokoni hadi Lihanga. Je, ni lini sasa Serikali itatenga fedha maalum kwa ajili ya kumalizia sasa kutoka Lihanga mpaka Chikalule, ambayo ni kama kilometa moja?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Barabara ya Mchemo hadi Mahuta imekuwa ina changamoto kubwa sana. Je, ni lini Serikali sasa itapandisha hadhi ya barabara hii kutoka udongo kwenda kutengenezwa kuwa barabara changarawe ili wananchi wa maeneo haya waweze kupita kwa usalama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, ninatambua kuwa jiografia ya Mji wa Newala Vijijini ina miinuko mikali na barabara hii ambayo imetajwa na Mheshimiwa Mbunge, Barabara ya Chikalule kwenda Makao Makuu ya Kitangali wananchi wetu kwenye maeneo yale wakati mwingine wamelazimika kupitia Lindi ili kufika makao makuu ya wilaya. Kwa kutambua umuhimu huo pia zipo taasisi kwenye eneo hilo, ikiwemo Shule yetu ya Msingi Chikalule ambayo inafanya vizuri sana; na ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya wananchi wale.
Mheshimiwa Spika, Serikali itakwenda kuijenga barabara hii kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Tumepanga, kwenye Mwaka wa Fedha unaofuata wa 2026/2027 tutaweka fedha kwa ajili ya barabara hii.
Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, kwenye swali lake la pili ameitaja Barabara ya Mchemu hadi Mahuta na Mheshimiwa Nape wakati ameanza kuuliza alitaka kuitaja barabara hii. Tunatambua kuwa barabara hii imebeba uchumi mkubwa wa zao la korosho kwenye maeneo ya Newala pamoja na Tandahimba na ina urefu wa kilometa 17.
Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha ujao ninawaelekeza mkoa waiangalie barabara hii vizuri ili waihuishe kwenye mipango yetu ya kitaifa na hatimaye iweze kujengwa na kuinua uchumi na kufungua uchumi wa Wananewala pamoja na Wanatandaimba.
MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza Serikali maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza, je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara zote zilizopo katika Mji wa Kitangari? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara za lami kutoka katika Kijiji cha Maputi hadi Ndanda, na pia, katika Kijiji cha Chiwonga, Pacha Nne, hadi Nanganga? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imeshaanza kujenga barabara zilizopo katika Mji wa Kitangari. Tumeanza na barabara ya kutoka kwa Mzee Lada mpaka kwa Mzee Twalibu, ambayo ina urefu wa kilomita moja, na siyo tu kwamba tumeishia kuijenga, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amehakikisha barabara hiyo imewekewa taa pia, na inatumika.
Mheshimiwa Spika, kadiri fedha zitakavyoendelea kupatikana tutaendelea na ujenzi wa barabara za mji huo. Barabara ya kutoka Msikiti Mkubwa kwenda kituo cha afya karibu na stendi, na vilevile Barabara ya Mnakute hadi Halmashauri na Barabara ya VETA hadi Nachirindima.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Barabara ya Maputi – Ndanda, Chuonga – Pacha Nne kwenda Mkongi hadi Nanganga njia panda ya kwenda Ruangwa, Serikali itatekeleza kama ilivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2025/2030. Nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia barabara hizi kwa umakini mkubwa. (Makofi)