MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA aliuliza:-
Je, lini Barabara za Chikalule hadi Lihanga na Lochinu hadi Mkwiti zitajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Yahya Esmail Nawanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutenga bajeti na kujenga barabara katika miinuko mikali kulingana na upatikanaji wa fedha ambapo hadi sasa imeshajenga Barabara ya Miyuyu hadi Hospitali ya Rufaa ya Ndanda yenye urefu wa kilometa 4.5 kwa tabaka la lami kwa gharama ya shilingi bilioni 2.25. Aidha, ujenzi wa kilometa 0.6 kwa kiwango cha zege kwenye eneo la mwinuko mkali katika Barabara ya Namdimba - Chiwata kwa gharama ya Shilingi Milioni 975.98 unaendelea kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ambazo zipo kwenye maeneo ya milima mikali katika Jimbo la Newala Vijijini, zikiwemo Barabara za Lihanga na Chikalule kilometa 1.5 na Barabara ya Mkwiti - Lochino - Nyangao kilometa 11.1 kulingana na upatikanaji wa fedha. (Makofi)
MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA aliuliza:-
Je, lini Stendi ya Mabasi ya Mji wa Kitangari, Newala, itajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Esmail Nawanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Newala ina stendi ya mabasi iliyopo katika Mji wa Kitangari, ambayo imepangwa kutengewa fedha katika Mpango wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 kupitia mapato ya ndani ya halmashauri. Kutokana na stendi hiyo kutokidhi mahitaji ya sasa ya usafiri, halmashauri imepanga kufanya maboresho ya awali kwa kiwango cha changarawe ili kuboresha utoaji wa huduma za wananchi.
Mheshimiwa Spika, sambamba na maboresho hayo halmashauri imeanza kutafuta eneo mahsusi, kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa itakayokidhi mahitaji ya Mji wa Kitangari na maeneo ya jirani.