MHE. ORAN M. NJEZA K.n.y. MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza:-
Je, lini Serikali itazipandisha hadhi Barabara ya Isenyela - Sangambi - Lupa - Lualaje na Chunya Godima - Sangambi kuwa chini ya TANROADS?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, suala la kupandisha hadhi barabara ni la kisheria kwakuzingatia vigezo vilivyowekwa. Ikiwa kuna barabara ambayo inakidhi vigezo kutoka daraja la barabara ya wilaya kwenda daraja la barabara ya mkoa inatakiwa barabara hiyo ijadiliwe kwenye Kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa husika na ikionekana inakidhi vigezo ndipo bodi hiyo kupitia Mwenyekiti itamshauri Waziri mwenye dhamana na barabara kuwa barabara husika imekidhi vigezo vya kuwa na hadhi ya barabara ya mkoa na hivyo ipandishwe daraja na kuwa barabara ya mkoa chini ya TANROADS.
Mheshimiwa Spika, TARURA kwa kushirikiana na Bodi ya Barabara ya Mkoa itaanzisha mchakato wa kuzipandisha hadhi barabara hizo katika mwaka 2025/2026 ili ziweze kuwa chini ya TANROADS.