Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Adonis Alfred Bitegeko (2 total)

MHE. ADONIS A. BITEGEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kuniona na kunipa nafasi. Jimbo la Muleba Kaskazini, Wilaya ya Muleba ina miradi miwili ya maji, Mradi wa Makongora na Mradi wa Iroba ambayo kwa muda mrefu inasubiri Serikali kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji. Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo ili kusaidia wananchi takribani 9,000 kupata huduma ya maji salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera yetu ya Maji, kwanza kabisa ni kuhakikisha kwamba maji yawe safi, yawe salama na yawe ya kutosheleza. Ujenzi wa chujio ni sehemu ya sera kwa sababu ni lazima chujio hilo liweze kutumika katika kuhakikisha kwamba maji yanakuwa safi, na pia yanatibiwa vizuri ili yawafikie wananchi yakiwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima chujio hilo liweze kutumika katika kuhakikisha kwamba maji yanakuwa safi na yanatibiwa vizuri ili yawafikie wananchi yakiwa salama. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge na kwa kazi kubwa. Ninafahamu ana miezi michache tangu ameingia, lakini amekuwa mfuatiliaji mzuri sana wa miradi hii ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wizara ya Maji tunaahidi kuendelea kumpa ushirikiano Mheshimiwa Mbunge ili kuhakikisha kwamba fedha zinapelekwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba chujio hili linajengwa ili likamilike na kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi. Ninakushukuru sana.
MHE. ADONIS A. BITEGEKO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tunashukuru Wilaya ya Muleba tumejengewa Mahakama ya Mwanzo katika Kata ya Izigo, lakini tuna Mahakama ya Wilaya ambayo ina changamoto ya ufinyu wa nafasi, ni chakavu na imejengwa miaka mingi na haiendani na ukubwa wa Wilaya ya Muleba yenye idadi ya watu karibu 650,000 na majimbo mawili ya uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mpango gani kujenga jengo jipya la Mahakama ambalo litakidhi mahitaji ya Wilaya ya Muleba?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu kabisa kuhakikisha kwamba kwenye jimbo lake utoaji wa haki unaendelea kuimarishwa. Ninaomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kama nilivyotangulia kusema kwamba, Mahakama kwa wakati huu inatekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu, mpango wa pili ambao umegharibu wastani wa bilioni 524.9.

Mheshimiwa Spika, mpango huu haujikiti tu kwenye kuboresha miundombinu kwa maana ya majengo ya Mahakama pekee, lakini pia hata katika kujenga mifumo ya kidijiti. Ndiyo maana mtaona kwa wakati huu mwananchi anaweza akafungua shauri kidijiti kupitia mfumo wa Mahakama wa ECMS, pia mwananchi anaweza akahudhuria shauri lake kupitia mifumo ya kidijiti kupitia Mahakama Mtandao.

Mheshimiwa Spika, pia kuna mifumo mingi ambayo inamwezesha mwananchi kupunguza gharama kusafiri kufika Mahakamani na kupata huduma zilizo bora na za kisasa. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Mahakama itafika na kuhakikisha kwamba jengo katika Wilaya hii ya Muleba inakuwa ni bora na la kisasa kwa sababu ndiyo mpango uliopo na ndiyo mpango unaotekelezwa.

Mheshimiwa Spika, jengo litajengwa na wananchi wa Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo hili la Muleba watapata miundombinu iliyo bora katika upatikanaji wa haki.