MHE. MDOWE HAJI KOMBO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kukipandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi kutokana na ukuaji wa mji huo kiutalii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mdowe Haji Kombo, Mbunge wa Nungwi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inauomba uongozi wa Jimbo la Nungwi na kuuagiza kwamba unapaswa kuwasilisha hoja yao ya kutaka kupandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi kwenye Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja, ambayo itashauri na kutoa mapendekezo yake kwenda Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapendekezo na ushauri wa Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kupitia Ofisi ya Kamishna wa Polisi Zanzibar yatawasilishwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya utekelezaji wa kupandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi iwapo vigezo vya kiulinzi, kiutawala na miundombinu vinavyotakiwa vitakuwa vimekamilika.