Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mohamed Mussa Utaly (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. MOHAMED M. UTALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii muhimu ili niweze kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema mwenye kurehemu kwa kunijalia afya njema na kuwa na uwezo wa kusimama katika Bunge hili kwa mara ya kwanza kutoa mchango wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza, naomba nitumie fursa hii adhimu kumshukuru Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na vikao vyote vilivyohusika katika kupitisha jina langu ili niweze kuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninachukua fursa hii kuwashukuru sana wapigakura wa Jimbo la Lindi Mjini, ambao wamenipigia kura nyingi za kutosha, na hapa ninawaahidi kwamba nitatumia uwezo wangu wote na nguvu zangu zote kuwatumikia ili kukidhi haja ya matarajio yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie fursa hii kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya katika nchi hii. Ninampongeza kwa namna ambavyo amepokea maono na mwongozo wa Mwenyezi Mungu, kuweza kumteua Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, tunamwona namna ambavyo anafanya kazi zake. Ukimwangalia katika utendaji wake wa kazi, ukimwangalia katika ziara zake, unaona ni namna gani matatizo ya wananchi wa Tanzania yanamshughulisha, na yeye anayashughulikia ipasavyo. Hongera sana kwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yake Waziri Mkuu, pamoja na mambo mengine, ameeleza namna ambavyo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya siku 100 ametekeleza ahadi zake zote alizoahidi. Hii ni kuonesha ni namna gani Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mtekelezaji wa ahadi tena kwa wakati. Hili linatupa matumaini kwamba ilani yetu hii ya Chama Cha Mapinduzi, itatekelezwa ipasavyo. Tunampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba nichangie hotuba hii kwa kuyaangazia matatizo au changamoto zilizopo katika Jimbo langu la Lindi. Kwanza tunamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweza kutupatia mambo yafuatayo: ujenzi wa shule mpya za kisasa, ujenzi wa hospitali ya wilaya, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ndaki ya Kilimo Tawi la Lindi, na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wana-Lindi tunamshukuru Rais kwa miradi ambayo sasa hivi inaendelea katika mji wetu. Miradi ambayo inaendelea sasa hivi ni suala la ujenzi wa soko la kisasa, ujenzi wa stendi ya mabasi ya kisasa na ujenzi wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii yote ni miradi ambayo ipo chini ya TACTICS yenye thamani ya shilingi bilioni 19.061. Pamoja na nia njema ya Mheshimiwa Rais, utekelezaji wa miradi hii unasuasua mno. Hili, pamoja na mambo mengine ni utaratibu uliotumika kumpata mkandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi aliingia mkataba tarehe 5 Februari, 2025. Mkataba huu ni wa kutekeleza mradi kwa muda wa miezi 15 na kulipwa malipo yake ya awali shilingi bilioni 2.8 ambayo ni sawa na 15% ya thamani ya mkataba. Miezi mitatu baadaye tarehe 7 Novemba ndipo mhandisi mshauri ambaye moja ya majukumu yake ni kufanya project review alisaini mkataba, lakini mpaka sasa, mradi huu utekelezaji wake ni 15% wakati muda uliotumika ni 60%. Tunaomba TAMISEMI wamhimize mkandarasi huyu ili kuweza kutekeleza mradi huu kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la pili, ambalo ningependa kuelezea ni ujenzi wa Barabara ya Mtange, Kineng’ene hadi Kibaoni. Barabara hii imekuwa ni barabara ambayo ipo kwenye ilani katika vipindi vyote. Mwaka 2022 ilijengwa meta 1,000, mwaka wa fedha 2023/2024 ilijengwa meta 600.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla, barabara hii kwa muda wa miaka miwili imejengwa kilometa 2.3. Hivyo, kama trend ya ujenzi wa barabara itakuwa hivi, maana yake barabara hii ya kilometa 19 itakuwa inajengwa kwa muda wa miaka 25. Jambo ambalo ukiangalia, hata huku kunakojengwa mwanzoni kutakuwa kumeshaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninawasihi, Mheshimiwa Waziri Mkuu, na Ofisi ya TAMISEMI, barabara hii iongezewe kasi ili ijengwe. Barabara hii imeshapewa majina chungu mzima. Kuna eneo ambalo ni bovu kuliko kawaida wanachi wamelipa jina kwamba ni Mashimo 40, eneo hilo. Kuna eneo ambalo limesababisha ajali nyingi sana, wananchi wa Lindi wameita eneo hilo Kadamba Ulumuke ambayo maana yake kwa Kiswahili, Kanyaga uvunjike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana eneo hili liweze kurekebishwa, barabara hii iweze kupitika kila mwaka na sasa iwe ni mara ya mwisho kuoneka katika ilani, iweze kuwa imekamilika, kwa sababu ni muda mrefu sasa tunaomba barabara hii ijengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ningependa kuzungumzia ni suala la afya. Tunalo eneo katika Mji wa Lindi, la Kata ya Kitumbikwela. Eneo hili liko ng’ambo ya barabara. Ili mwananchi wa eneo hili aweze kupata huduma za afya, analazimika kuvuka ng’ambo ya bahari kuja mjini ili aweze kupata huduma za afya, kule hakuna kituo cha afya. Mwaka 2024, kule kulijengwa msingi wa kituo cha afya, lakini tangu wakati huo hakuna kilichoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee na kwa hali waliyokuwanayo watu hawa ambao huduma zao za afya zinawalazimisha wapande pantoni ambayo inafanya kazi kuanzia saa 12.00 asubuhi mpaka saa 12.00 jioni. Tunaomba Serikali ione umuhimu wa kuwajengea kituo cha afya ili kunusuru maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na suala la Shule ya Sekondari Lindi. Shule ya Sekondari Lindi, ni shule ambayo viongozi wengi sana wamesoma pale, akiwemo mama yetu Mheshimiwa Mama Salma Kikwete. Shule hii mwaka 2016 ilipata janga la kuungua moto. Madarasa kadhaa yaliungua, tumefanya harambee, lakini haikukidhi haja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka katika Ofisi ya Waziri Mkuu, tulishauriwa tujenge majengo ya ghorofa mbili. Tumeanza ujenzi, fedha tulizozipata zimetuwezesha kujenga msingi tu. Tunaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na Ofisi yake waone namna ambavyo wanaweza kutusaidia kujenga shule hii ambayo imeungua.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MOHAMED M. UTALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)