Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon Joel Arthur Nanauka (2 total)

MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza:-

Je, kipi kipaumbele cha Wizara ya Vijana kwa vijana wa Tanzania?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ninapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuniteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana. Pia kwa namna ya kipekee kwa kuunda Wizara mpya inayoshughulikia maendeleo ya vijana ikiwa ni dhamira yake ya kuwaweka vijana katikati ya maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kipaumbele kikuu cha Wizara ya Maendeleo ya Vijana kwa vijana wa Tanzania ni kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa lengo la kuboresha ustawi wao na kuchangia kwa tija katika maendeleo endelevu ya Taifa. Katika kutekeleza kipaumbele hicho, Wizara inajielekeza katika maeneo makuu yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, Wizara inaendelea kuimarisha uwezeshaji wa vijana kiuchumi kwa kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa mitaji, mafunzo ya ujasiriamali, ukuzaji wa biashara na ajira. Pili, Wizara inaweka mkazo katika uendelezaji wa ujuzi kwa vijana ili kuwaandaa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira na kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, pia Wizara inaendelea kuimarisha ushiriki wa vijana katika maamuzi na masuala ya utawala bora, kwa kuanzisha na kusimamia majukwaa rasmi ya ushiriki wa vijana. Mwisho, Wizara inatekeleza afua za ustawi, malezi na ulinzi wa vijana, ikijumuisha masuala ya afya ya akili, maadili, uzalendo, amani na mshikamano wa kitaifa, kwa kushirikiana na Wizara, taasisi pamoja na wadau mbalimbali.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukuza Vipaji na Ujuzi wa Vijana wa Tanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO (MHE. RAHMA R. KISUO) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, Toleo la Mwaka 2023 na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007, Toleo la Mwaka 2024. Aidha, Serikali inakamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Ajira ya Mwaka 2008. Lengo la kufanya mapitio hayo, ni kuimarisha utekelezaji wa sera hizo kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuanzishwa kwa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa lengo la kukuza ujuzi wa nguvukazi ya Taifa, ili kumudu ushindani katika soko la ajira, ambapo hadi sasa Watanzania 168,657 wamenufaika. Vilevile, kuendeleza vituo vya ubunifu na atamizi, mashindano ya sayansi na teknolojia, pamoja na programu za kuibua na kukuza vipaji katika sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.