Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Mohammed Mahmoud Ayoub (26 total)

MHE. IBRAHIM S. MZIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa vituo hivi vinahudumiwa na ndugu zetu wa polisi ambao wanafanya kazi kubwa sana ya kulinda nchi yetu. Je, Mheshimiwa Waziri, yupo tayari kuambatana nami kwenda Jimbo la Mtambile kujionea hali halisi ya makazi ya polisi wetu hawa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa swali la nyongeza la Mheshimiwa Said Ibrahim; na ombi lake la kwenda Mtambile nimelipokea na nipo tayari kuambatana naye kwenda Mtambile.
MHE. ASHA OMAR RASHID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ninashukuru kwa kunipatia fursa hii nami kuuliza swali langu la nyongeza. Pale Mkoani kwangu Kaskazini Pemba pana Kituo cha Polisi cha muda mrefu. Kituo kile kilizinduliwa tarehe 25 Juni, 1979. Kwa kuongezeka wananchi katika Mkoa ule wa Kaskazini Pemba. Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya polisi katika Wilaya ya Micheweni na Wilaya ya Mkoa wa Kaskazini Pemba pamoja na jengo la RPC wa Mkoa wa Kaskazini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Asha Omar, Mbunge wa Viti Maalum, Kaskazini Pemba, kwa swali lake zuri; na nimpongeze sana kwa kuwa karibu sana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama hasa Jeshi la Polisi na kubaini pia changamoto zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilieleza katika majibu yangu ya msingi wakati nikijibu wiki iliyopita, kwamba kwa upande wa ujenzi wa vituo vya polisi vya mkoa tulikuwa tunakiri kwamba tuna mikoa mitano ambayo ilikuwa haina vituo vya polisi; lakini kwa upande wake alikuwa anaongelea zaidi kuhakikisha kwamba anafanya ukarabati wa jengo la RPC katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambalo hilo nalo lipo kwenye mpango wa ukarabati kama ambavyo tunaendelea nao. Kwa sasa tuna miradi 56 ya ukarabati nchi nzima katika ngazi na maeneo mbalimbali. Kwa hiyo ninaamini kwamba tukienda kwenye hatua ya pili ya mpango wa kukarabati jengo hilo nalo litaingia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa yale majengo mawili ya wilaya kwa maana Wilaya ya Wete na Wilaya ya Michiweni Kaskazini Pemba nayo yapo kwenye majengo 75 ambayo kwa sasa ama yapo kwenye hatua ya ukarabati ama ujenzi upya kwa wilaya zetu 75 za nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali kupitia Jeshi la Polisi tupo kwenye hatua ya kukamilisha mpango mkakati wa miaka mitano ijayo. Wakati tukiendelea na hatua hiyo, tunaendelea vilevile kutathmini hali ya majengo ya vituo vya polisi, makazi ya askari na maeneo mengine yakiwemo hospitali na majengo ya mazoezi ya vikosi vyetu vya Field Force na mengineyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitambue, wapo Wabunge wengi ambao wamehitaji ama kujengewa ama kufanyiwa ukarabati vituo vya polisi. Kwa ruhusa yako ninaomba niwatambue Mheshimiwa Florence George Samizi, Mheshimiwa wa Kigoma, Mheshimiwa Joseph Copriano Isack au Kadogo wa Monduli wamehitaji hilo, ninatambua pia hitaji lake, Mheshimiwa Anne Kilango Malacela naye na nimemwahidi nitakwenda pia kwenye eneo lake, pamoja na Mheshimiwa Ester Bulaya naye pia alihitaji pale Bunda Mjini, naye nimemwahidi pia nitakwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nina swali dogo la nyongeza. Kama ikimpendeza Mheshimiwa Naibu Waziri atalijibu au atalichukuwa. Wilaya yetu ya Malinyi tumekuwa tuna shida ya gereza la mahabusu kwa muda mrefu sana. Eneo limepatikana lakini kumekuwa kuna ucheleweshwaji wa kukamilisha ambayo inawafanya wahusika kusafiri umbali mrefu sana kwenda Wilaya ya Ulanga. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha suala hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimfahamu ili niweze kujibu vizuri; amekusudia mahabusu ya polisi au ya gereza?NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge.

MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, mahabusu ya gereza.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunaongelea kuhusu suala la Jeshi la Polisi lakini kwa sababu Magereza na yenyewe ni sehemu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, lakini ninaomba tu nimjibu Mheshimiwa Kapoma kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yapo baadhi ya magereza yamekuwa na changamoto ya uchakavu wa majengo. Hata hivyo, moja ya eneo ambalo amelitaja la jimbo lake kwamba wilaya nzima ya Malinyi hakuna gereza na kupeleka eneo la pili; tunakuja na mpango na tutaueleza kwenye bajeti ya mwaka huu kwamba ni mpango gani kwa upande wa Jeshi la Magereza, tutaenda kuboresha magereza katika maeneo ambayo yana uhaba likiwepo eneo lake la Malinyi.
MHE. MWINYI JAMAL RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa ruksa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja katika Jimbo la Bumbwini, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewekeza nguvu kubwa sana katika uchumi wa nchi na maeneo mengine; je, haioni sasa kuna haja ya kujengwa kituo kikubwa cha polisi katika jimbo hilo kutokana na uchumi wa nchi ulivyokuwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninaomba kumjibu Mheshimiwa Mwinyi Jamal swali lake la nyongeza kuhusiana na jimbo lake la Bumbwini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwamba Bumbwini kwa sasa ni eneo la kimkakati hasa kwa uchumi wa Zanzibar, kwani Bumbwini inaenda kuelekea kujengwa uwekezaji wa bandari kubwa mpya; Bandari ambayo itakuwa na maeneo karibu matano. Katika bandari ile kwa bahati nzuri wakati nilipokuwa Mkuu wa Mkoa wa mkoa ule, niliwahi kupata fursa ya ushiriki kidogo wa maandalizi ya bandari hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango ulioandaliwa wa eneo lile la Bumbwini kumeandaliwa kujengwa miundombinu yenyewe ya bandari, miundombinu ya barabara za kisasa lakini pia kujengwa mji mdogo. Katika mpango uliowekwa wa mji mdogo ndani yake kuna ujenzi wa kituo kikubwa cha polisi ambacho kitaweza kusaidia kuimarisha eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali imewekeza vituo vingi vidogo vidogo na sasa vituo hivyo vyote havifanyi kazi ikiwemo kituo changu cha Jimbo la Shaurimoyo na vituo vingine. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvifufua vituo hivyo vikaanza kufanya kazi ili kuweza kuwasaidia wananchi wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninaomba kumjibu Mheshimiwa Mattar swali lake la nyongeza ambalo linahusu vituo vidogo vya polisi kwa maana ya daraja C1 au police post.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri hasa kwa Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, kulijengwa vituo vingi vya police post katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo, ninaomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza siyo vituo vyote vidogo vidogo kuwa havitumiki, vipo baadhi yake vinatumika. Mfano wa vituo vidogo vidogo vinavyotumika ni Kituo cha Mkunazini, Kituo cha Vuga na vinginevyo. Kwa vile ambavyo kwa sasa havitumiki tumefanya tathmini kupitia Jeshi la Polisi kuona namna gani nzuri ya utumiaji wa vituo vidogo vile vya polisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tukiri vingi ya vituo hivyo vipo maeneo karibu karibu. Kwa hiyo Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeona haja ya kuwatumia Askari wa Ulinzi Shirikishi kwa kushirikiana na Polisi wa Shehia ili wafanye doria badala ya kuweka askari wengi kwenye kituo kimoja na kutoa huduma bila ya ufanisi kama ambavyo ingetarajiwa. Kwa hiyo, bado vituo hivyo tuna mpango wa kuvitumia, lakini kwa utaratibu mwingine kinyume na ule wa awali hadi hapo tutakapokuwa na askari wa kutosha wa kuweza kuwaweka vituoni na wengine kufanya doria.
MHE. TIMOTH G. ANYOSISYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tarehe 29 Oktoba, 2025 Jimboni Kawe vilichomwa Vituo vya Polisi vitatu. Kwetu sisi Wanakawe jambo hili tunalichukulia kama jambo la dharura. Je, ni lini Serikali itajenga vituo hivi ili kurejesha hali ya huduma ya kipolisi katika maeneo husika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninaomba nimjibu swali lake Mheshimiwa Timoth kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tarehe 29 Oktoba, 2025 kulitokea uharibifu wa mali mbalimbali za Serikali ikiwepo baadhi ya Vituo vya Polisi katika baadhi ya maeneo. Ninaomba nimwambie Mheshimiwa Timothy kwamba Serikali inaendelea kukamilisha kazi ya tathmini na kuja na mpango wa dharura wa kuona namna gani ya kuweza kurejesha huduma kwenye maeneo husika. (Makofi)
MHE. ALI VUAI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninapokea ushauri, pia nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, Serikali ina mpango gani wa kuwapeleka askari wa doria katika eneo hilo ambalo liko mbali na kituo cha Polisi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, je, yuko tayari kutembelea Kijiji hicho kwenda kuona matatizo halisi ya umuhimu wa ujenzi wa kituo cha Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Khamis kwa kufuatilia kwa karibu hali ya ulinzi na usalama katika Ukanda wa Mkwajuni hasa katika eneo la Matemwe, eneo ambalo ni ukanda wa utalii na lina ongezeko kubwa la idadi ya watu kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ninaomba kujibu hoja zake mbili. La kwanza, tuna mpango gani wa doria, kwa ukanda wote wa kuanzia Matemwe, Pwani Mchangani, Kiwengwa hadi Nungwi. Kwa sasa Jeshi letu la Polisi linaendelea na doria kwa sababu eneo lote hilo ni la kimkakati kwa ajili ya uwekezaji wa utalii, na kila siku Jeshi la Polisi kupitia Kituo Kikuu kilichopo Mkokotoni wanaendelea kufanya doria na Kituo Kidogo kilichopo Kiwengwa katika ukanda wote wa Pwani ambao amezungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa pili wa ombi lake la kutembelea hilo na kuona umuhimu wa kujenga kituo katika eneo hilo, napenda kukubaliana naye kimsingi kwamba eneo la ukanda wa Matemwe ni eneo la utalii, na kwa sababu ni eneo la utalii, kasi kubwa ya uwekezaji pamoja na ujio wa watalii na wageni mbalimbali kutembelea maeneo hayo, kunaakisi hoja aliyoileta ya kuweza kujengwa kituo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninaomba nimjibu tu Mheshimiwa kwamba niko tayari kutembelea eneo hilo. Pili, tunaona umuhimu wa kujenga kituo cha Polisi katika eneo hilo.
MHE. MWINYI JAMAL RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa heshima hii ya kuuliza swali moja la nyongeza. Ninaomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri, je, ni sababu zipi zinafanya kujengwa kwa kituo cha Polisi? Ni wingi wa watu, idadi ya uhalifu, kilometa, nyumba au ni nini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nimemwelewa vizuri alichotaka hasa ni elimu ya kufahamu kwamba tunapokwenda kufanya maamuzi ya kujenga vituo vya Polisi, ni vigezo gani vinavyotusababisha kufanya maamuzi hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hivyo ndivyo, nataka kumwambia tu Mheshimiwa Mwinyi Jamal Ramadhan kwamba kwenye vyombo vya ulinzi na usalama kuna kitu kinaitwa security audit kwa maana ya ukaguzi wa kiusalama. Eneo ambalo linaonekana lina matishio zaidi ya kiusalama, ndilo eneo ambalo tunalipendekeza kuweza kuliwekea miundombinu ya kiulinzi vikiwemo vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wingi wa watu au idadi ya watu ni moja ya sababu, kasi ya ukuaji wa uchumi inaweza ikawa moja ya sababu, uhamiaji unaweza ukawa pia ni sehemu ya sababu.
MHE. ASHA S. MOTTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali haioni haja ya kujenga nyumba za ghorofa kwa wafanyakazi wa Kituo cha Polisi Fuoni pamoja na kununua gari la doria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Serikali inaona umuhimu wa kujenga nyumba za Polisi nchi nzima. Katika eneo la Fuoni hivi sasa zipo nyumba za Polisi, na baadhi yake ni za ghorofa, isipokuwa tu ninajua Mheshimiwa Asha amekuwa karibu na wananchi wake katika eneo la Fuoni na anafuatilia mwenendo wa hali ya usalama kwenye eneo lile na hasa kufuatilia ukamilishaji wa kituo cha Polisi pamoja na ujenzi wa nyumba za makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati, eneo hilo tumeshatembelea mimi na Mheshimiwa Asha, tumeshaliona na kubainisha baadhi ya maeneo yenye uhitaji wa kujengwa hizo nyumba na tayari tumetoa maelekezo kwa wenzetu wa Jeshi la Polisi kuweka mpango wa kujenga nyumba hizo kama ambavyo Mheshimiwa amependekeza.
MHE. BARAKA A. U. MWAMENGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona na kunipa nafasi hii. Ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi cha Kasumulu kilichopo border ya Kasumulu ndani ya Jimbo la Kyela kwa kuwa kiliathirika na vurugu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge wa Kyela na nimpongeza vilevile kwa kuona umuhimu, na ninadhani kwa sababu ya ufafanuzi wangu wa hoja ya msingi ya kwa nini tunajenga vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye swali la msingi tulilojibu la Jeshi la Polisi kwa mara ya kwanza Bungeni, tulikuja na mpango wa dharura wa maeneo ambayo yana uhitaji wa kujenga vituo vya Polisi na tuliainisha wastani wa maeneo 698 nchi nzima. Hayo ndiyo maeneo ya dharura kujenga vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo hayo 698 ambazo ni karibu kata zaidi ya 600 zilikuwa hazina kabisa vituo vya Polisi na kata 77 zilikuwa zimeanza ujenzi kwa maboma, lakini hawajakamilisha. Nataka kumwambia tu Mheshimiwa kwamba tunaona umuhimu wa kujenga kituo cha Polisi eneo hilo, lakini lini? Mpango ule tumeugawa katika awamu tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza tutakuwa na vituo 196, awamu ya pili tutakuwa na vituo 212 na awamu ya tatu tutakuwa na vituo 211. Kwa hiyo, kukamilika kwa Mpango huu, basi na eneo lake litakuwa tayari limeingia kwenye ujenzi.
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza. Kama ambavyo amekiri mwenyewe kwamba Gereza la Babati ni miongoni mwa magereza yaliyojengwa kwa miaka ya zamani, je, ni nini mpango wa Serikali wa kujenga gereza lingine jipya ambalo pia litakuwa ni gereza la kisasa linaloendana na wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Emmanuel kwa swali lake la nyongeza ambalo ni la muhimu sana. Kwanza tukiri ni kweli tuna uhitaji mkubwa wa magereza nchini, kwani katika hali ya sasa nchi nzima tuna idadi ya magereza 129. Kati ya magereza hayo, magereza 10 yana hadhi ya magereza ya kanda, magereza 76 yana hadhi ya magereza ya mikoa na wilaya na magereza 43 ni magereza ya wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hiyo, tuna upungufu wa takribani wilaya 50 ambazo hazina magereza, lakini kazi inayoendelea sasa ya ujenzi wa magereza katika maeneo mbalimbali ambayo kwa kweli kwa baadhi ya maeneo imepiga hatua nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Wilaya ya Karatu gereza limekamilika, Wilaya ya Kilosa limeanza ujenzi, Wilaya ya Gairo linaendelea, Wilaya ya Kingurungundwa kule Mchinga nalo linaendelea. Ninaamini kwamba na maeneo mengine pia tutaendelea na hatua kama ambavyo nimetaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali kwenye ujenzi wa magereza haya ni kuendelea kuweka fedha kwenye bajeti, kwani tayari tumeshafanya tathmini ya uhitaji wa magereza hayo kwamba kila gereza moja linahitaji wastani wa shilingi bilioni nane kulijenga. Hivyo, kwa magereza 50 tunahitaji wastani wa shilingi bilioni 40 ili tuweze kujenga magereza hayo. Sambamba na hilo, tunafahamu pia ipo changamoto kubwa ya makazi ya Askari Magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo hilo, pia Serikali imeandaa mpango wa muda mrefu ambao utajenga wastani wa nyumba 6,368 za magereza zitakazoweza kukaliwa na wastani wa kata 21,187. Bajeti ya fedha hizo zinahitajika zaidi ya shilingi trilioni 2.88 kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.
MHE. MDOWE HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa ruhusa yako. Kwanza ninaomba niishukuru na kuipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kazi kubwa ambayo inaendelea kuifanya katika nchi yetu. Pia ninashukuru kwa majibu yao ambayo wamenipa, kwa sababu majibu haya yametoa mwongozo mzuri katika suala letu hili. Hata hivyo, ninayo maswali mawili ya nyongeza katika jambo hili: -

(a) Je, ni vigezo gani vya kiulinzi, kiutawala na kimiundombinu vinavyotakiwa kukamilika ili kituo cha Polisi kiweze kupandishwa hadhi?

(b) Je, ni jukumu la nani hasa kukamilisha vigezo vya kiulinzi na kimiundombinu katika vituo vya Polisi nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Mdowe Haji Kombo, Mbunge wa Jimbo la Nungwi kwa maswali yake mawili ya nyongeza, ambayo ni muhimu sana. Ninapenda kumfahamisha Mheshimiwa Mdowe kwamba, vigezo vya kimiundombinu ni madaraja ya majengo ya Jeshi la Polisi ambayo yapo kwenye daraja la C1, C, B na E, kutegemeana na aina au eneo linalotaka kujengwa kituo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ombi ambalo wamewasilisha wao kwa Kituo cha Polisi cha Nungwi, kwa sasa kipo kwenye daraja C. Kwa hiyo, kinaomba kupandishwa hadhi kwenda kwenye daraja B. Ili kufikia kiwango cha daraja B, basi ni lazima miundombinu hiyo ya jengo la kituo cha Polisi iwe imekidhi vigezo vya daraja B la vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika vigezo vya kiulinzi ni kuangalia parameter za eneo ambalo linaombewa kupandishwa daraja la eneo hilo. Kwa mfano, hivi sasa Jeshi la Polisi linayo maeneo ambayo yamepewa hadhi ya mikoa, lakini kiutawala yapo hadhi ya wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano halisi ni kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambao umepewa kanda maalum, na ndani yake zile wilaya zimepewa hadhi ya mikoa. Hiyo inatokana na hali ya kiutawala, na pia mahitaji ya kiulinzi katika eneo la Mkoa husika wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa vigezo hivyo, watakapowasilisha maombi yao kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kwa maana ya Kamati ya Usalama ya Wilaya, itaweza kuchakata na kutathmini hali ya vigezo vyote vitatu kama vitakuwa vimefikiwa na kushauri ipasavyo kwenye ngazi inayofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili kwamba, ni nani ambaye ana jukumu hilo, nilieleza kwenye majibu yangu ya msingi kwamba, ninauomba uongozi wa Jimbo la Nungwi kwamba uwasilishe pendekezo hilo kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kwa maana ya Kamati ya Usalama ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. IMAMU MTUMWA VUAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia teknolojia ya kisasa kama CCTV Camera na mifumo ya kidigitali katika kuboresha ulinzi nchini badala ya kutegemea vituo vya Polisi pekee?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninampongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Imamu Vuai, Mbunge wa Magomeni kwa swali lake la msingi na muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba, dunia kwa sasa imekua kwa kiasi kikubwa kwenye eneo la teknolojia. Kutokana na kukua huko, hata Dira yetu ya Maendeleo ya 2050 imeelekeza kwamba tutumie teknolojia katika kukuza uchumi na kuimarisha ufanisi. Hivyo nikubaliane na rai yake inayosema kwamba sasa Jeshi la Polisi au vyombo vya ulinzi na usalama vijielekeze zaidi kwenye teknolojia katika kuimarisha mifumo ya kiulinzi, na huko ndipo ambapo kwa sasa dunia ipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kujielekeza huko kuna faida nyingi, zikiwemo kupunguza idadi ya makosa (crime rates) kwenye maeneo mbalimbali, vilevile kuna kupatikana kwa usahihi wa taarifa za kiusalama au kwa wale wanaotenda makosa na bila ya kumwonea mtu kwa sababu tumetumia teknolojia. Aidha, tunaweza kupunguza matumizi makubwa ya rasilimali watu na kutumia mifumo na vifaa badala ya idadi kubwa ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo hili, na kwa kuona umuhimu huu, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanza mchakato wa kuliangalia upya jambo hili. Kwa bahati nzuri, kwa upande wa Zanzibar jambo hili lilishaanza kwa muda kidogo. Tumeona katika eneo la Mji Mkongwe limeondoa au kupunguza kwa kiasi kikubwa sana crime rate kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeliangalia jambo hili katika maeneo makuu matatu. Kwa kuanzia, kwanza, Serikali inataka kwenda kwenye miji salama (safer city), na itaanza miji mikubwa; pili, tunataka kwenda kwenye barabara salama kuhakikisha kwamba tunapunguza ajali kwa kutumia mifumo; na tatu, katika ukaguzi wa magari kwa maana vehicle inspection, nalo hilo tuko katika mwelekeo wa kuelekea huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa, Kituo Kikukuu cha Polisi cha Wilaya ya Tunduru ni kikongwe na kidogo, katika mazingira ambayo yanalazimisha sisi akina Ado ambao huitwa mara kwa mara pale kuhojiwa, tumewashuhudia makamanda wetu wakiwa wanaendesha mahojiano ndani ya chumba kimoja kwa watuhumiwa zaidi ya mmoja, hali ambayo inaondoa kabisa weledi, je, ni lini, Serikali itafikiria kujenga kituo kipya cha Wilaya ya Tunduru ili makamanda wetu wafanye kazi kwa weledi na utaratibu unaohitajika, ikiwemo faragha?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru na kumpomgeza sana Mheshimiwa Ado Shaibu, lakini ninaomba nimkumbushe tu kwamba kituo cha Polisi alichokitaja na vituo vyote vya Polisi nchini, uwepo wake siyo kwa ajili ya akina Ado Shaibu, ni kwa ajili ya wale wote ambao watakuwa wanahalifu sheria za nchi hii. kwa hiyo, Serikali inaendelea na hatua mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa vituo vya Polisi vya ngazi ya wilaya, ambavyo kwa taarifa yetu ya awali tulisema kwamba tuna vituo vya Polisi 75 vya ngazi ya wilaya, ambavyo ama vinahitaji ukarabati au vinahitaji kujengwa upya kwa lengo la kufikisha hadhi ya daraja B, kwa maana ya kituo cha wilaya, kwa hiyo, na kituo cha wilaya ambayo Mheshimiwa Ado Shaibu amekitamka, nacho kipo kwenye mpango huo. Kadiri ya hali ya upatikanaji wa fedha tutaendelea kujenga vituo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. SALUM KHAMIS SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwenye Jimbo langu la Bububu kumejengwa kituo cha ghorofa kwa kuzingatia matumizi ya eneo husika kabla ya uhuru. Je, ni kigezo gani kilichotumika kujenga nyumba ya chini ilhali matumizi yamekua na pia unyeti wa eneo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Salum Salim, Mheshimiwa Mbunge ambaye amesema kwamba, kwenye jimbo lake kumejengwa kituo cha Polisi kabla ya uhuru na ni cha ghorofa. Sasa, anataka kujua ni kigezo gani kilichotumika kujenga nyumba ya chini badala ya ghorofa kama ambavyo kwa wakati huo vituo vimejengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba za makazi kwa ajili ya Askari ni moja kati ya hitaji kubwa tulilonalo katika Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama. Tunakiri kwamba kadiri siku zinavyoendelea na ongezeko la idadi ya watu linakua kubwa na matumzi ya ardhi yanazidi kuwa makubwa. Hivyo, inapendekezwa na kushauriwa kwamba, kadiri iwezekanavyo, tujenge nyumba za ghorofa badala ya nyumba za chini kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya hali ya kibajeti na kwa mujibu wa uharaka na uhitaji wa makazi katika eneo hilo, ndiyo sababu kuu inayosababisha kujenga nyumba za chini katika baadhi ya maeneo. Vilevile kuendelea na ujenzi wa nyumba za ghorofa kwenye yale maeneo ambayo tayari fedha zipo, na pia kule ambapo wamekosa maeneo ya kujenga nyumba za chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Mkoa wetu wa Dodoma hapa tulipo, tayari tunaendelea na ujenzi wa zaidi ya nyumba sita za ghorofa kwa ajili ya makazi ya Askari. Kabla ya ukoloni kulikuwa kuna nyumba za chini ndogo ndogo ambazo hazina hadhi na hali nzuri. Kwa hiyo, kazi ya ujenzi wa nyumba za ghorofa inaendelea nchi nzima kwa kadiri ya hali ya fedha, kwa maana ya bajeti, itakavyoruhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Maaskari wa Polisi katika Jimbo la Ulyankulu, wafanyabiashara wa Kata ya Uyowa Kijiji cha Mwamnange, pamoja na wafanyabiashara wa Kata ya Kona Nne Kijiji cha King'wangoko walijenga kituo cha Polisi kwa ajili ya malengo ya kuimarisha usalama wao. Hata hivyo, vituo hivi vimeshindwa kukamilika. Mbaya zaidi, Kituo cha Polisi cha Kona Nne kimepanga kwenye nyumba ya mtu, ambapo zaidi ya miaka tisa hajalipwa. Je, Serikali ina kauli gani kuhusiana na kukamilika kwa vituo vya Polisi hivi viwili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Lufungija kwa hoja yake ya kukamilisha vituo vya Polisi katika eneo la Ulyankulu kama ambavyo ameainisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati najibu swali la msingi na la awali katika Bunge hili, nilieleza kwamba vipo vituo 77 vya Polisi katika kata mbalimbali ambavyo bado havijamalizika, na vipo katika ngazi ya maboma. Tulieleza kwamba kwenye awamu ya kwanza ya ujenzi wa vituo, vituo 77 hivi vitaingia kwa ajili ya kumaliziwa na vile vipya kuweza kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Ulyankulu kwamba, mara baada ya kutenga fedha na kupata bajeti hiyo mwaka wa fedha 2026/2027, tutaanza kukamilisha maboma haya ya vituo vya Polisi ambavyo bado havijakamalika.
MHE. NURU I. KASHAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kigoma Kusini lina vituo vya Polisi vitano ambavyo ni Kituo cha Polisi Kazuramimba, Kituo cha Polisi Sigunga, Kituo cha Polisi Ilagala, na Kituo cha Polisi Buhingu. Vituo hivi havina majengo, badala yake wamekodi majengo binafsi kwa watu. Je, ni lini Serikali itajenga vituo hivi vya Polisi ili kuleta hadhi ya Jeshi la Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Nuru, Mbunge wa Kigoma Kusini kwa hoja yake ya kuimarisha vituo vya Polisi na kujenga vituo vya Polisi kwenye maeneo aliyoyatamka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyoeleza kwamba kimsingi, maswali yanayoongezeka tayari majibu yake tulishayatoa, sasa na hili swali kuhusu lini; maana yake ni kwamba tutaanza mwaka wa fedha wa 2026/2027 kama mpango wetu tulivyoutoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na ninaomba kuwasilisha.
MHE. ASHA OMAR RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii na mimi niulize swali la nyongeza. Ninaishukuru sana Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kutujengea Kituo cha Polisi pale Matangatuani, lakini pale bado hatuna makazi ya Polisi. Je, ni lini Serikali itajenga makazi bora ya nyumba za Polisi pale Matangatuani Wilaya ya Micheweni Pemba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, makazi ya Askari yanaendelea kujengwa hivi sasa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Kaskazini Pemba. Eneo la Matangatuani lipo kwenye mpango. Sasa, kwamba ni lini, itategemea na hali ya upatikanaji wa fedha ili tuweze kukamilisha ujenzi na pia kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Maswa hatuna kabisa kituo cha Polisi kwa ajili ya OCD wa wilaya yetu. Mwaka 2025 tuliambiwa Serikali ilikuwa imetenga fedha kwa ajili ya kuanza kujenga Kituo cha Polisi cha Wilaya. Je, mpango huo umeishia wapi, kwa sababu mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Mashimba, Mbunge wa Maswa kwa swali lake la msingi na muhimu kama ambavyo imeelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa fedha zilitengwa mwaka wa fedha 2025/2026 na bado tunaendelea na muda wa utekelezaji wa bajeti hiyo. Ninapenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutampa taarifa rasmi ya kwamba lini kazi ya ujenzi wa kituo chake kwa mujibu wa hali ya upatikanaji wa fedha katika kipindi kilichobaki itaweza kuanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. MAHESH SHAH AKLUSHA BOLISHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Wizara ina mpango wowote wa kujenga kituo kidogo katika Wadi ya Kiuyu karibu na eneo la Mabutu kwa kuwa eneo hili limewekwa kwa ajili ya uwekezaji, na ni prime location kwa ajili ya wawekezaji kutoka nje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafikiri tuna kituo kikubwa kinajengwa cha Polisi ndani ya Jimbo la Micheweni, lakini patakuwa ni mbali kidogo kutoka Mabutu mpaka hapo kituo kinapojengwa. Je, tuna mpango wowote wa kujenga kituo kidogo katika eneo la Mabutu karibu na eneo la uwekezaji kwa ajili ya security? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Mahesh, Mbunge wa Micheweni kwa swali lake ambalo ameomba kujengewa kituo kidogo katika eneo la Kiuyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulieleza kwenye mpango wa jumla wa ujenzi wa vituo vya Polisi kwamba, azma ya Serikali ni kufikisha huduma za kiusalama katika kila kata kuwe na kituo cha Polisi, lakini utekelezaji wa azma hiyo utategemea sana hali halisi ya upatikanaji wa fedha, na vile vile mpango wa hali ya usalama katika maeneo husika. Ndiyo maana tukaja na ule mpango mkuu wa kwamba tutaanza na maeneo ambayo yamebainika kiusalama yana uhitaji wa haraka zaidi halafu baadaye twende kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwahidi tu Mheshimiwa Mahesh kwamba hoja yake tunaichukua, na ikiwa Kituo cha Kiuyu kipo kwenye mpango wa dharura, basi kitaweza kujengwa katika utaratibu wa mpango huu.
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Katika Jimbo la Moshi Vijijini, wananchi wamekuwa mstari wa mbele sana kujenga vituo vya Polisi kwa kujitolea na hapa tunapoongea vituo vingi vya Polisi vimekamilika kikiwemo Kituo cha Polisi cha Kata ya Okaoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali ina mpango gani kuongeza Askari katika vituo hivi katika Jimbo la Moshi Vijijini kwa kuwa vituo vyote ambavyo vimejengwa na wananchi vina Askari mmoja mmoja na wakati…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Makoi, jambo la kwanza unauliza swali la pili. Sasa ni sababu majina hatuyashiki vizuri, kwa hiyo, ungeuliza kifupi zaidi.

MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi ninaomba niulize moja. Serikali ina mpango gani kuongeza Askari katika vituo mbalimbali vya Polisi katika Jimbo la Moshi Vijijini ambavyo wananchi wamejenga kwa kujitolea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Morris, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini kwa swali lake la msingi. Kwanza ninampongeza na kuwapongeza wananchi wa Moshi Vijijini kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuunga mkono Serikali kwa ujenzi wa vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimhakikishie kwamba maeneo yote nchini ambayo yatakuwa yamekamilika ujenzi wa vituo na vikawa vimefikia katika vile viwango ambavyo nimevieleza katika majibu ya awali, basi tutaendelea kupeleka Askari kwa mujibu wa uhitaji katika maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Jimbo la Mpanda Mjini, Kituo cha Polisi cha Wilaya kilikuwa katikati ya Mji wa Mpanda na baadaye Jeshi la Polisi wakajenga kituo kipya nje ya mji. Nilitaka kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini sasa pale katikati ya Mji wa Mpanda ambapo ndiyo kuna shughuli nyingi za kiuchumi watatuwekea kituo kidogo ambacho kitaendelea kusaidiana na kile kituo kikubwa ambacho kiko umbali wa kilometa sita mpaka 10 kutoka kwenye baadhi ya kata?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge wa Mpanda Mjini kwa hoja yake ya msingi na muhimu. Kwanza ninadhani tumshukuru kwa kupongeza jitihada za Serikali za ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Jimbo la Mpanda Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuhusu ni lini kituo kidogo kitajengwa kwenye karibu na maeneo ya makazi ya watu ambapo kuna mkusanyiko, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakaa pamoja, tuone namna gani tunaweza kushirikiana na wananchi kwenye eneo hilo, kwa vile ni kituo kidogo cha daraja C ili kusudi tuweze kukijenga kwa haraka zaidi.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Kituo cha Wilaya ya Masasi kilijengwa mwaka 1958 na hakina hadhi ya kuwa kituo cha wilaya, je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kituo kipya cha Polisi chenye hadhi ya wilaya ya Masasi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake la kuimarisha Kituo cha Masasi ambacho kimejengwa kwa muda mrefu na kipo katika hadhi au ngazi ya wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili nimeshalijibu, lakini naomba niongezee kwamba Kituo cha Masasi ni miongoni mwa vituo 75 vya ngazi ya wilaya ambavyo ama tutavifanyia ukarabati au kuvijenga upya katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuanzia mwaka wa fedha 2026/2027 tutaendelea na mpango wetu wa utekelezaji wa kuimarisha vituo hivi 75 vya wilaya kikiwepo Kituo cha Wilaya cha Masasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Liwale katika Mkoa wa Lindi haina kituo rasmi cha Polisi na wilaya hiyo ilishatenga eneo kubwa na zuri kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya. Je, ni lini sasa Serikali itatujengea kituo cha Polisi cha daraja A?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Zainab kwa swali lake la msingi la kuomba Kituo cha Polisi cha Wilaya ambapo kwa sasa hakipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuweke vizuri kumbukumbu; kwa kuwa ni Kituo cha Polisi cha Wilaya, maana yake hakitakuwa daraja A, kitakuwa ni daraja B. Kwa hiyo, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunachukua hoja yake, na kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi ni kwamba katika vituo 75 vya wilaya na cha kwake kipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutatoa umuhimu kwenye maeneo ambayo hayana kabisa vituo vya Polisi vya wilaya ili kusudi naye tuweze kumjengea.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Tumbi ni moja kati ya kata za pembezoni katika Jimbo la Tabora Mjini, lakini haina kituo cha Polisi kabisa, hivyo kusababisha Askari watoke mjini kwenda Tumbi kwa ajili ya kushughulikia matukio ya kihalifu. Nini mpango wa Serikali kuhakikisha wanajenga Kituo cha Polisi katika Kata ya Tumbi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Hawa, Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, kwa swali lake la msingi. Niseme tu kwamba nilivyokuwa nikieleza mpango wetu wa Serikali wa kujenga vituo vya Polisi, nilisema kuwa tuna uhitaji wa ujenzi wa vituo vya Polisi kwenye kata 3,900 na kata hii aliyoieleza Mheshimiwa Mbunge ni miongoni mwa kata hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lini? Itategemea na mpango ulivyoelekeza na hali ya upatikanaji wa fedha tuweze kumpatia kituo cha Polisi kwenye kata hiyo. Ahsante
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa wilaya ambazo hazina kituo cha Polisi na halmashauri ya wilaya ilianzisha ujenzi, na mimi kama Mbunge, nimechangia kwenye hicho kituo; na Serikali iliahidi kutoa shilingi milioni 20, lakini mpaka sasa ni mwaka wa tatu. Ni lini Serikali itakamilisha Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Tanganyika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Selemani kwa swali lake la msingi na ninawapongeza sana kwa kuchangia fedha kwenye ujenzi wa vituo vya Polisi ambao ni uhitaji mkubwa kwa usalama wa raia na mali zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumpongeza Mheshimiwa Selemani, nimjibu tu kwamba vituo ambavyo havijamalizika nilitoa maelezo ya jumla hapa kwenye maboma 77 na nimeeleza kwamba tutaendelea kusaidia ili kukamilisha vituo hivyo kikiwemo kituo chake Mheshimiwa Selemani na tumhakikishie tu kwamba tutajitahidi mwaka wa fedha 2026/2027 tuweze kumsaidia na kukamilisha hiyo fedha ambayo tumeahidi kutoa ili tuweze kukamilisha kituo hicho. Ahsante sana.