Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Mohammed Mahmoud Ayoub (4 total)

MHE. SAID I. MZIMBA aliuliza: -

Je, lini Serikali itatenga Bajeti kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya Polisi Mtambile na Kengeja kwa kuwa vimechakaa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Said Ibrahim Mzimba, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekwishafanya tathmini ili kubaini gharama halisi za ujenzi wa Kituo kipya cha Polisi cha Kengeja baada ya kituo kinachotumika sasa kuwa kichakavu na kwamba hakiwezi kufanyiwa ukarabati. Kiasi cha fedha shilingi milioni 165 zinahitajika. Tathmini kwa ajili ya kubaini gharama halisi ya ukarabati wa Kituo cha Polisi Mtambile zimefanyika na kiasi cha fedha cha shilingi milioni 90 zinahitajika. Fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Polisi vya Kengeja na Mtambile zinatarajiwa kutengwa toka kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027.
MHE. ALI VUAI KHAMIS aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga kituo cha Polisi katika Kijiji cha Matemwe Jimbo la Mkwajuni Unguja kutokana na uwekezaji mkubwa uliopo katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kumjibu swali Mheshimiwa Ali Vuai Khamis, Mbunge wa Mkwajuni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la Matemwe Jimbo la Mkwajuni, hakuna sehemu iliyotengwa rasmi kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Polisi. Napenda kutumia fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu, kumshauri Mheshimiwa Mbunge pamoja na Kamisheni ya Ardhi Zanzibar kupitia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili kutenga eneo kwa ajili Kituo cha Polisi Matemwe, ili Serikali iweze kutenga fedha kutoka kwenye bajeti yake kwa ajili ya kujenga kituo hicho cha Polisi.
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY aliuliza: -

Je, lini Serikali itafanya maboresho ya makazi ya askari pamoja na kununua magari mapya Gereza la Babati Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Emmanuel John Khambay, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Gereza la Babati ni miongoni mwa Magereza yaliyojengwa miaka mingi tangu mwaka 1974 hali iliyosababisha uchakavu wa miundombinu ya gereza pamoja na majengo ya makazi ya Askari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Magereza limeanza kutekeleza mpango mkakati wa muda mfupi na muda mrefu ambapo kwa Gereza Babati ziko nyumba tatu zinaendelea na ujenzi kwa kutumia mapato ya vyanzo vya ndani vya ubunifu. Aidha, katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imetenga shilingi 5,380,000,000/= kwa ajili ya ununuzi wa magari 31 kwa shughuli za Utawala na kusafirisha Mahabusu. Pindi magari hayo yatakapofika, Gereza la Babati litapatiwa gari moja mpya kwa matumizi ya kituo.
MHE. MDOWE HAJI KOMBO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukipandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi kutokana na ukuaji wa mji huo kiutalii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mdowe Haji Kombo, Mbunge wa Nungwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inauomba uongozi wa Jimbo la Nungwi na kuuagiza kwamba unapaswa kuwasilisha hoja yao ya kutaka kupandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi kwenye Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja, ambayo itashauri na kutoa mapendekezo yake kwenda Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapendekezo na ushauri wa Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kupitia Ofisi ya Kamishna wa Polisi Zanzibar yatawasilishwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya utekelezaji wa kupandisha hadhi Kituo cha Polisi Nungwi iwapo vigezo vya kiulinzi, kiutawala na miundombinu vinavyotakiwa vitakuwa vimekamilika.