Supplementary Questions from Hon Zacharia Paulo Issaay (5 total)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Kwa kuwa ni miaka mitatu sasa taarifa ya Wizara ya Mazingira na Wizara zingine mtambuka kuhusu Maziwa ya Babati, Basutu, Tlawi kule Mbulu na Mkoa wa Manyara kwa ujumla haijarudishwa na kazi haijafanyika; je, ni lini Waziri atakwenda Mbulu kutembelea hayo Maziwa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi hii. Ninaomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya maswali yote mawili ya Waheshimiwa Wabunge. Vilevile, nimshukuru Mheshimiwa Mattar na Mheshimiwa Spika wewe pia, pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunipongeza jana na leo kwa kuweza kuchaguliwa kwenye nafasi ya Makamu wa Rais wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa.
Mheshimiwa Spika, ninaomba niongezee sasa kujibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza ni dhahiri kabisa nafasi hii ambayo tumeipata inachangiwa na kazi kubwa na mafanikio makubwa na heshima kubwa ambayo Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan na nchi yetu iliyojenga katika Jumuiya ya Kimataifa ndiyo ikawezesha kuweza kupata heshima hii ya kuweza kupata nafasi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kupitia nafasi hiyo tunaweza kunufaika katika masuala mengi; moja ni kuhakikisha kwamba tunapenyeza vipaumbele vyetu kama Taifa katika kukabiliana na changamoto za mazingira ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa Bioanuwai, masuala mengine mbalimbali yanayohusu ikiwemo nishati safi na kadhalika. Hiyo pia itatusaidia kuweza kunufaika na fedha mbalimbali (fursa za kifedha) kupitia Mifuko ya Mazingira kwenye Jumuiya ya Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge wa Mbulu aliuliza swali la Ziwa Babati. Ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba yeye pamoja na Mheshimiwa Mbunge wa Babati Mjini tulizungumza nao kuhusiana na jambo hilo. Hivi sasa ninavyozungumza leo kuna timu ya wataalam imekwenda kule Babati kufanya tathmini ili kuhakikisha kwamba tunafanya nini kwa kupata hatua za dharura za kuweza kukabiliana na tatizo hilo.
Mheshimiwa Spika, wakati huo huo, Serikali ina mkakati wa muda mrefu ikiwemo kununua mitambo ya kukabiliana na changamoto ya magugu maji katika maeneo yote yaliyoathirika na magugu maji katika nchi yetu. Kwa hiyo, hatua za kwanza za dharura tayari tumeanza nazo leo, lakini baada ya muda siyo mrefu tayari tutapata fedha kupitia Serikali Kuu (kupitia Hazina) ili tuweze kupata mitambo ya kukabiliana na tatizo hilo.
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Serikali ilikusudia kujenga stendi ya mabasi, soko, dampo na machinjio katika Mji wa Mbulu kwa kupitia Mradi wa TACTIC. Hadi sasa Serikali imefikia hatua gani katika kutekeleza mradi huu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, ujenzi wa stendi katika Mji wa Mbulu ni sehemu ya Miradi ya TACTIC tutakayoitekeleza katika awamu ya tatu. Hivi sasa Serikali inaendelea na ukamilishaji wa Usanifu wa miradi yote 18, kwa maana ya miji yote 18 iliyomo kwenye awamu ya tatu. Mara tu baada ya usanifu kukamilika, taarifa zote tutazikusanya na tutakwenda hatua inayofuata ya kutangaza zabuni kumpata mjenzi, pamoja na mkandarasi mshauri. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itatekeleza ujenzi wa barabara ya Magara – Mbuyuni – Mbulu kwa kiwango cha lami ambapo ni ahadi ya Makamu wa Rais kwa miaka mitano sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara ni kweli inapita kwenye escapement ambapo tunachokifanya sasa hivi ni kujenga kiwango cha zege kwenye ile miinuko mikali ili magari yaweze kupita wakati tunatafuta fedha, lakini kikubwa atakubaliana na mimi kwamba lile Daraja la Magara tulishalikamilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tunaendelea kutafuta fedha kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami, lakini kikubwa sasa ni kujenga kwa kiwango cha zege kwenye ile miinuko mikali. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Kimsingi masuala haya ya kuchangisha wazazi kupitia shule zetu nchini hayawezi kuepukika kwa baadhi ya maeneo. Kwa mfano, walimu wanaojitolea sasa hivi katika shule zetu nchini ni wengi sana ambao hawajaingia kwenye mfumo wa ajira na ile michango yao inachangwa na wazazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka wa kufanya mapitio upya ya maeneo ambayo yangeruhusiwa kwa mfumo usio rasmi kuchangia ama kwa namna nyingine yoyote ili kuleta uwiano wa kutoa huduma hii ya nafasi ya kufundisha kwa wanafunzi wetu nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilishapitia na itaendelea kupitia kwa kadri itakavyohitajika na kutoa miongozo na maelekezo ya maeneo ambayo Kamati, Bodi na Vikao na mikutano rasmi ya wazazi inaweza ikafikiria kuchangisha ikiwa kutakuwa kuna ulazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujaacha dirisha wazi kwamba kila mchango uchangishwe, na ndiyo maana tumeweka utaratibu na Mkuu wa Wilaya na Serikali yake wanajiridhisha kwamba mchango huu ni sehemu ya michango ambayo inaweza ikawa na tija zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Issaay kwamba, tutaendelea kuboresha, na ikiwa kuna maeneo, kuna michango holela na isiyokubalika, tutachukua hatua ili kudhibiti michango holela katika maeneo hayo.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Ninaishukuru sana Serikali kwa kazi kubwa na kumlipa mkandarasi wa barabara ya Mbulu - Garbabi - Haydom. Je, kwa kuwa mkandarasi huyu hadi sasa hajarudi site, ni lini mkandarasi wa Mbulu - Garbabi - Haydom atarudi na kuanza kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna vipande viwili Mbulu - Garbabi na Labay - Haydom ambapo mkandarasi anayetekeleza ni mkandarasi mmoja na tumeshamlipa fedha aliyokuwa anatudai. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mkandarasi atarudi site kwanza kufanya kazi ya kuhakikisha kwamba zile njia za diversion zinapitika, lakini pia kuendelea na kazi ya ujenzi kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumwagiza Meneja wa Manyara ahakikishe mkandarasi anarudi site na kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yalikuwa na changamoto za kutopitika yanapitika wakati anaanza kuijenga hiyo barabara yote kwa kiwango cha lami katika vipande hivyo viwili.