Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kenneth Ernest Nollo (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hoja ambayo iko mbele yetu leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunatambua kwamba mawasiliano hasa ujio wa internet na simu hizi za kiganjani ni mapinduzi makubwa ambayo tumeyashuhudia katika miongo hii na kwa sasa tuna generation ambayo iliishi kabla hakuna simu za kiganjani, hakuna internet na sasa iko kwenye generation ambayo tuko katika mukhtadha huu wa mawasiliano ambayo ni jambo ni dunia nyingine kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Waziri kwenye ripoti yake na kwa mujibu wa ripoti ya TCRA ya mwezi Machi, 2025 jumla ya laini za simu zilizopo ni milioni 90 ambayo ikiwa ni ongezeko zaidi ya Watanzania ambao wako miliomi 60, kwa hiyo iko zaidi milioni 30 mbele ya laini nadhani na ile mtu anakuwa na mitandao kama mitatu yote anakuwa na laini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, internet users wako karibia nusu ya ile milioni 49. Ukija wamiliki wa simu (handset) wako kama milioni 56 na simu janja ni milioni 24 yaani simu zile ambazo si simu janja ni milioni 56 na hizi simu janja ziko milioni 24.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa nina hoja na hoja yangu ni kwamba kuwepo kwa upungufu mdogo wa kuwepo kwa simu za kawaida nyingi milioni 56 inaonesha kwamba bado Watanzania wengi hawatumii internet katika shughuli zao za kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la internet kama nilivyosema na uwepo wa simu janja ni suala la muhimu zaidi. Mimi ninachoamini kwamba simu janja kwanza ni muhimu katika suala zima la usalama. Mtu anayetumia simu janja ana address kuliko yule ambaye hatumii simu janja. Kwa hiyo, Serikali kwanza inatakiwa na inapaswa kuona namna gani tunaweza tukawapongeza watumiaji kwanza wa internet, vilevile kuongeza idadi ya simu janja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Waziri amesema kuna kampuni kule Mkuranga tayari imekuja inataka kuja kuanza kutengeneza simu janja. Mimi nadhani tujitahidi ikiwezekana mwekezaji huyo apate incentives za kutosha ili kwamba tuweze kupata simu nyingi janja ambazo ni za bei rahisi ili kuondoa hii gap iliyopo kati milioni 56 na milioni 24 iweze kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile simu zinazoingia kutoka nje nazo tupunguze kodi lengo letu tuweze kupata Watanzania wengi wanaoweza kutumia simu janja na hivyo hivyo tutakuwa tume-boost kutumia internet.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi labda tupate maelezo ya kitaalamu Waziri kama atashauriwa na wataalamu, ubaguzi uliopo kati ya wananchi wanaoishi vijijini watumie 3G wa mjini watumie 4G na 5G ni Watanzania wale wale, discrimination gap hii ya internet inatokana na nini? kwa nini mitandao sisi wa vijiji inaona tutumie 2G ambayo 2G hupati internet, 3G inakuwa kama unapika ugali kwa kutumia kuni mbichi, internet ile unahangaika nayo sana. Kwa nini ubaguzi huo upo? Naomba Waziri aje atueleze namna ya ku-fill hiyo gap.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TCRA itusaidie, kuna mitandao mingine internet yake ni nzuri, nyingine internet yake ni kama kuni mbichi unapopika chakula nayo ituambie na kama hivyo kwa nini hawa-comply?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilikuwa naona tusiuziwe internet bundle kwa muda, kama nimenunua kifurushi kile acha nitumie. Kwa akili ya kawaida unavyosema nitumie kwa wiki halafu ikifika wiki kimeisha, mimi naona si sawa. Jambo hili na nadhani TCRA hii naomba iondoke katika financial year hii mimi sidhani kama kuna haja ya kwamba kuwe kuna muda wa matumizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naishukuru sana Serikali kwa maana ya minara tumepata katika majimbo yetu lakini mimi naona haitoshi. Kwa kasi ya matumizi ya simu na shauku ya wananchi, UCSAF imefanya kazi kubwa na najua inapata hela kutoka kwa operators ili minara iweze kujengwa. Mimi nadhani Serikali iangalie vyanzo vingine ili tuweze kupata ujenzi wa minara na ikiwezekana maeneo mengi yaweze kupata minara na hivyo kuimarisha na kuleta utengamano kwa ajili ya upatikanaji wa internet.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine zipo fedha zinapatikana kwenye simu za kimataifa wanaita international terminating, lakini kwenye internet nako kuna fedha. Nilitaka Waziri atuambie kwamba Serikali inapata kiasi gani kupitia huduma ya international calls vilevile na kwenye mitandao hii ya internet pia na mkongo. Mimi najua kwa mfano nchi ya Rwanda na Burundi sisi ni gateway yao how much do we get kutokana na huduma hiyo? Kwa hiyo na mkongo wetu wa Taifa je, unatupa faida gani ambapo kama ni gateway ya nchi zingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu wenzangu walivyoiongelea habari ya stock exchange kwa kampuni moja ya simu kuwepo mle. Mimi nadhani hii ni sheria ya Wizara ya Fedha, TCRA naye ni kama regulator. Jambo hili mukhtadha wa Serikali iliangalie kwa mapana zaidi kwamba kama Wizara ya Fedha je, 25% ile ambayo inataka iwe kwenye Initial Public Offer (IPO) ina maana na inaathiri vipi kama uwekezaji wa makampuni mengine yanayotaka kuja kuingia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali ituambie kwa nini Vodacom wameingia, hao wengine wamechukua miaka kumi na mbili hawajaingia? Hayo ni masuala yote yanaweza kuja kuelezewa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja na nashukuru sana, ahsante sana. (Makofi)